
Dar es Salaam. Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imesogeza mbele mchezo baina ya Simba na Dodoma Jiji FC ambao ratiba ya awali inaonyesha ilipangwa kuchezwa Februari 15, 2025 katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Kuahirishwa kwa mchezo huo kumekuja ikiwa ni siku mbili tangu msafara wa Dodoma Jiji ulipopata ajali katika eneo la Somanga, Kilwa, Lindi wakati ulipokuwa ukija Dar es Salaam ukitokea Ruangwa, Lindi ambako timu hiyo ilikuwa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC, Jumapili, Februari 9, 2025 ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Taarifa ya TPLB leo imesema kuwa mchezo huo utapangiwa tarehe nyingine.
“BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imeahirisha mchezo namba 148 wa Ligi Kuu ya NBC (Simba SC vs Dodoma Jiji) ambao ulipangwa kufanyika kwenye uwanja wa KMC Complex Februari 15, 2025 kuanzia saa 10:00 alasiri. Sababu ya kuahirishwa kwa mchezo huo ni baadhi ya wachezaji na maofisa wa ufundi wa klabu ya Dodoma Jiji kutokuwa katika hali nzuri kiafya baada ya basi la klabu hiyo walilokuwa wakisafiria kutoka Ruangwa mkoani Lindi, kupata ajali mkoani humo.
“Ajali hiyo imesababisha athari hasi kwa klabu ya Dodoma Jiji kwa kuchelewesha safari yake ya kuelekea mkoani Dar es Salaam pamoja na kuathiri maandalizi ya kiufundi kwa kuwakosa wachezaji na maofisa wa ufundi ambao walipata majeraha katika ajali hiyo. Bodi itatangaza tarehe mpya ya mchezo huo hivi karibuni,” imefafanua taarifa hiyo ya TPLB.
Mapema leo, Dodoma Jiji FC imetoa taarifa kupitia kurasa zake kuwa msafara wake umerejea Dodoma.
“Kikosi chetu kimewasili salama Jijini Dodoma na kupokelewa na menejiment ya Halmashauri ya Jiji ambapo baada ya Mapokezi taratibu za kitabibu zitaendelea kwa majeruhi wote katika hospital ya Benjamin Mkapa wa baadae leo,” imefafanua taarifa ya Dodoma Jiji.
Tukio la Dodoma Jiji ni la pili msimu huu ambapo timu ya kwanza kupata ajali ilikuwa ni JKT Tanzania, tukio lilitokea Oktoba 27, 2025 ambalo lilipelekea mchezo baina ya Simba na JKT Tanzania uliokuwa uchezwe Oktoba 29, 2025 kusogezwa mbele.