Sababu kukosa morali ya kazi Ijumaa, Jumatatu

Dar es Salaam. Umewahi kuhisi kukosa morali ya kazi inapokaribia mwishoni mwa juma au Jumatatu inayojulikana kwa wengine kama ‘Monday Blues’?

Hali hii huwatokea watumishi wengi, mtu hujihisi uzito, kutojali au kukosa hamasa ya kufanya kazi Jumatatu au hata siku za Alhamisi na Ijumaa.

Zipo sababu nyingi za hali hii kutokea, baadhi zikitajwa kuwa ni uchovu kutokana na kazi za wiki nzima, hivyo ifikapo Ijumaa mwili na akili huanza kudai mapumziko.

Si hivyo tu, inapokaribia mwishoni mwa juma, wapo wanaoanza kufikiria mapumziko, safari au muda wa familia, hivyo ari ya kazi hupungua.

Kwa mujibu wa wataalamu, hali hii pia husababishwa na shinikizo la kuanza juma jipya Jumatatu, likiwakilisha mwanzo wa majukumu mapya kama vile ya mikutano au miradi mipya, hivyo kuzua wasiwasi au uchovu wa kisaikolojia hata kabla ya siku yenyewe haijaanza.

Inaelezwa hali ya kukosa motisha pia inaweza kusababishwa na kukosekana kwa usawa kati ya kazi na maisha binafsi, wengi wakijihusisha zaidi na kazi kuliko maisha yao binafsi, jambo linaloweza kusababisha msongo wakati wa kurejea ofisini.

Utafiti uliofanywa na taasisi inayojishughulisha na masuala ya huduma ya kwanza ya afya ya akili (MHFA) ya nchini Uingereza ulionyesha asilimia 17 pekee ya wafanyakazi walihisi kuwa na hamasa ya kwenda kazini kila siku.

Utafiti huo, uliochapishwa Januari 17, 2025 katika tovuti ya masuala ya afya na usalama ya Uingereza, ulionyesha asilimia 22 ya wasimamizi wa ngazi ya chini waliripoti kutowahi kuhisi msisimko katika kazi yao.

Kwa mujibu wa utafiti huo, mbali na ‘Monday Blues’, mmoja kati ya wafanyakazi 10 alisema havutiwi na kazi anayofanya, huku asilimia 23 wakisema wana hamasa ya kazi kila siku. Utafiti huo ulihusisha waajiriwa 2,000.

Mfanyakazi jijini Dar es Salaam, Kelvin Daniel (si jina halisi) anasema kwake Ijumaa huwa siku ya furaha kwa kuwa ni mwisho wa kufanya kazi, akiwaza kwenda kupumzika.

“Ijumaa huleta hali ya furaha ya kuwa pamoja na marafiki, kushirikiana, kupumzika na kufurahia maisha. Huwa siwekezi kwa kiasi kikubwa kufanya kazi siku hiyo,” anasema.

Mtazamo wa wataalamu

Akizungumzia hali hiyo katika mahojiano na Mwananchi, mtaalamu wa saikolojia, Dk Neema Mwankina anasema Ijumaa ni mwanzo wa wikiendi ambayo baadhi ya watu wamejiwekea kwenye akili zao.

“Suala hili kisaikolojia linakuja pale watu wamefanya kazi kuanzia Jumatatu, hivyo ikifika Ijumaa anawaza kupumzika na kupumzisha akili yake. Mwingine pengine hakufurahia kazi kutokana na matatizo binafsi ya kifamilia au kiofisi, ikifika Ijumaa anawaza kwenda kupumzika,” anasema.

Dk Mwankina anasema mwingine anaona anapunguza mzigo wa kutoa nauli ya Jumamosi na Jumapili, hivyo ni sababu kwake kufurahia Ijumaa.

“Sababu nyingine ni kutothaminiwa kazini, hii inamfanya mtu anakwenda kazini mradi siku ziende, ikifika Ijumaa anafurahi kwa kuwa anakwenda kupumzika,” anasema.

Anasema wengine hufurahia kutokana na mazingira ya kazi kutokuwa rafiki, kutothaminiwa, kutoelewana na bosi au wafanyakazi wenzake.

Vilevile kuchoka kutokana na pilikapilika za kazi za juma zima, anapoona Ijumaa ambayo ni siku ya mwisho ya kazini hufurahi.

Pia, anasema wapo wenye matatizo ya kiafya, wanaokwenda kusimamia miradi yao, ambao mwisho wa juma huwa wenye furaha kwa kuwa wanapata fursa ya kufanya mambo yao.

“Ni kweli ufanisi wa kazi unapungua kutokana na watu kushuka morali kiutendaji siku hiyo,” anasema.

Mwanasaikolojia Charles Kalungu anasema kwa kawaida ubongo unatafsiri unakwenda mapumzikoni, hivyo kwa siku hiyo mtu akipewa majukumu mengi anaweza akakosa umakini.

Anasema hali hiyo husababishwa na mtu kufanya kazi bila kupumzika kwa muda mrefu na siku hiyo hata waajiri wanaitumia kumaliza kazi za wiki na maandalizi ya juma jipya.

“Ukifanya kazi bila kupumzika ufanisi unashuka na kupunguza umakini, kufanya kazi kunahitaji kupumzika kuipa nafasi akili kuongeza umakini. Ukifanya kazi bila kupumzika kuna uwezekano wa kupoteza ufanisi wa utendaji,” anasema.

Nini kifanyike

Ofisa Rasilimaliwatu kutoka kampuni ya Lake Cement, Fred Kiresia anasema Ijumaa huwa na kazi nyingi kwa sababu kuna siku mbili mbele ambazo siyo za kazi.

Hivyo, anasema kila mmoja anapaswa kuwa na mpango wa kazi ili kila siku apunguze wingi na hadi kufikia Ijumaa mzigo utakuwa mdogo na kutoathiri utendaji.

“Siku hii iwe na kazi ndogo-ndogo ambazo hazihitaji umakini mkubwa. Inakuwa rahisi kuzifanya kwa ufasaha tofauti na kukiwa na kazi ngumu,” anashauri.

Mwenyekiti wa Chama cha Maofisa Rasilimaliwatu Wanawake Tanzania (What), Judith Charles anasema kinachopaswa kufanyika ni maofisa rasilimaliwatu kuwa wabunifu kwa kuanzisha programu za kuwavutia wafanyakazi Ijumaa ili wasitamani kukimbilia nyumbani.

Anasema wafanyakazi wanapaswa kutengenezewa mazingira waipende kazi, waifanye kama ofisi ni yao kwa kuweka mazingira bora ya kazi kwa ustawi wa afya ya akili.

“Hayo yakifanyika watu hawatakimbilia majumbani ifikapo siku hiyo, bali watakuwa na shauku ya kuendelea kuwapo kazini,” anasema.

Anasema kupungua kwa hamasa ya kazi kuna athari kwa mwajiri, kwani lengo lake ni kuwapo ufanisi kiutendaji sawa na siku nyingine za juma.

“Katika mwezi kuna Ijumaa nne, kama mtu asipofanya kazi vizuri itaathiri utendaji wake na ofisi kwa sababu anakuwa hajafikia matarajio ya mwajiri wake. Wahusika wanapaswa kuwa wabunifu katika hili,” anasema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *