Sababu Ikangalombo, Maxi na Mwenda kubadili kikosi Yanga

Dar es Salaam. Kuna wachezaji watatu ndani ya kikosi cha Yanga ambao wanaweza kubadilisha upepo ndani ya timu hiyo siku chache zijazo wakati Ligi Kuu itakaporejea.

Yanga inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 39 inatarajiwa kucheza mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara wikiendi ijayo dhidi ya Kagera Sugar baada ya hapo itavaana na KenGold

Watatu hao ni beki Israel Mwenda, winga Jonathan Ikangalombo na kiungo Maxi Mpia Nzengeli.

Mchezaji wa kwanza ni beki wa pembeni Israel Mwenda ambaye amesajiliwa na Yanga katika dirisha dogo la usajili akitokea Singida Black Stars.

Mwenda ana uwezo mkubwa wa kucheza nafasi zote mbili za beki wa pembeni kwa maana ya beki wa kulia na beki wa kushoto.

Kama Ramovic ataamua kumtumia Mwenda upande wa beki wa kulia, maana yake mmojawapo kati yake, Kibwana Shomari na Yao Attohoula atajikuta katika wakati mgumu wa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Yanga.

Uhalisia kwamba hakuna uwezekano wa kocha kuwatumia wachezaji watatu wa nafasi ya beki wa kulia kwa wakati mmoja maana yake utasababisha mmoja kukaa jukwaani na wengine wawili kutumika katika mchezo mmoja kwa mmoja kucheza na mwingine kuwepo benchi.

Kungekuwa na uwezekano wa Mwenda au Yao mmojawapo kutumika katika nafasi ya winga wa kulia lakini uwepo wa idadi kubwa ya wachezaji wanaomudu kucheza katika nafasi hiyo, unazidi kuweka kikwazo kwa hilo kutokea.

Ni kama itakavyokuwa katika upande wa beki wa kushoto ambako pia Mwenda anamudu kucheza kwani kuna Nickson Kibabage na Chadrack Boka ambao kabla hata ya dirisha dogo la usajili walikuwa wanagawana dakika za kucheza ndani ya timu hiyo.

Usajili wa winga Jonathan Ikangalombo unaweza kuibadilisha Yanga katika namna mbili ambazo ni upangaji wa kikosi na mfumo wa kiuchezaji iwapo mchezaji huyo atafanikiwa kulishawishi benchi la ufundi la timu hiyo.

Ikangalombo ambaye alikuwa anasumbuliwa na homa lakini amerejea mazoezini anaweza kupata nafasi ya kucheza kwa kupishana na ama Maxi Nzengeli au Stephane Aziz Ki lakini pia anaweza kuifanya Yanga icheze katika mfumo wa 4-4-2 ili kumpa uhuru zaidi mchezaji huyo ambaye sifa yake kubwa ni kucheza kwa spidi.

Kupona kwa Maxi Nzengeli ambaye amekuwa akitajwa kuwa mchezaji mwenye ufanisi zaidi mazoezini, kunaweza kugeuka shubiri kwa mmojawapo kati ya Clement Mzize au Prince Dube.

Kipindi Nzengeli alipokuwa akikosekana, kocha Ramovic alikuwa akimtumia Mzize kama kiungo mshambuliaji wa pembeni katika mfumo wa 4-2-3-1 huku Prince Dube akisimama kama mshambuliaji wa kati.

Kurejea kwa Maxi na akiwa katika ubora wake uliozoeleka maana yake utalazimisha Mzize arudishwe katika nafasi ya mshambuliaji wa kati na kwa vile mfumo wa 4-2-3-1 unahitaji mshambuliaji mmoja wa kati, hapana shaka yeye au Dube mmoja hatojikuta akianza kikosini.

Kiungo wa zamani wa Yanga, Hussein Swedi alisema kuwa ana faurahia kuona wachezaji wa timu hiyo wanavyotengenezewa ushindani.

“Timu haitakiwi kuwa na wachezaji wachache ambao wanaamini watacheza kila siku kwa sababu ya kukosa ushindani. Kukiwa na vita ya kugombea nafasi ndio timu inafanikiwa kwa sababu kila mchezaji atacheza kwa kujituma na kuonyesha kiwango bora ili kumshawishi kocha kumpa nafasi.

“Ukiangalia hao wachezaji uliowataja, wanaweza kucheza katika nafasi tofauti uwanjani na sio wao tu bali wapo wengi kwenye kikosi cha Yanga ambao ni viraka na wana viwango vizuri,” alisema Swedi.