Sababu Bunge kupitisha Sh945. 7 bilioni ya nyongeza

Dodoma. Bunge limepitisha nyongeza ya mapato na matumizi ya jumla ya Sh945.7 bilioni kwa ajili ya nyongeza kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25 kutoka Sh49.346 trilioni zilizoidhinishwa Juni mwaka jana hadi Sh50.291 trilioni.

Bajeti hiyo imewasilishwa leo, Februari 14, 2025 na na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, siku ya mwisho ya Mkutano wa Bunge ulioanza Januari 28, 2025, ikijazia kwenye bajeti iliyoanza kutumika Julai 1, 2024 na itahitimishwa Juni 30, 2025.

Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ya Sh49.346 trilioni ilisomwa bungeni na Waziri Nchemba Juni 13, 2024 na kupitishwa asilimia 92.3 ya kura za wabunge na wabunge 18 hawakuwa na uamuzi.

Akiwasilisha nyongeza hiyo, Dk Nchemba amesema fedha hizo zitaelekezwa kwenye shughuli za sekta za elimu, afya  utalii na programu mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema fedha hizo zimepatikana kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Mgawanyo wake

Akizungumzia mgawanyo wa fedha hizo, Dk Nchemba amesema Sh325.9 bilioni zimetengewa kwa ajili ya Wizara ya Fedha, kwa ajili ya matumizi ya kitaifa, kugharamia malipo ya madeni ya watumishi, wakandarasi na wazabuni wa ndani pamoja na ujenzi wa miundombinu ya Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba.

Waziri Nchemba amesema kati ya fedha hizo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetengewa Sh131.4 bilioni kwa ajili ya kugharamia mahitaji ya mtalaa mpya wa sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi wa shule za sekondari za amali, upatikanaji wa vifaa na walimu.

 “Fedha hizo zitagharamia ukamilishaji wa ujenzi wa vyuo vya Veta, ujenzi wa maktaba ya Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (Muce), ujenzi wa miundombinu ya Chuo cha Nelson Mandela Arusha, ujenzi wa majengo ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima pamoja na ujenzi wa Jengo la Maktaba Mwanza,” amebainisha Dk Nchemba.

Ameongeza kuwa Wizara ya Afya imeongezewa Sh53.7 bilioni kwa ajili ya kugharamia dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

Pia, Waziri wa Fedha amesema Ofisi ya Rais – Tamisemi imeongezewa Sh173.7 bilioni kwa ajili ya sekta ya elimu, afya na kuiwezesha Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) kukarabati miundombinu ya barabara na madaraja iliyoathirika na mvua za Masika, ili iweze kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema Sh260.7 bilioni zimetengwa kwa ajili ya Wizara ya Maliasili na Utalii ili kugharamia uendeshaji na ukarabati wa miundombinu ya barabara katika Hifadhi za Taasisi za Utalii za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa.)

Wakichangia mjadala wa nyongeza hiyo ya bajeti, wabunge wameshauri fedha hizo pia zielekezwe kwenye ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati pamoja na kumalizia maboma yaliyoanzishwa na wananchi.

Mbunge wa Kuteuliwa Shamsi Vuai Nahodha amesisitiza fedha hizo zielekezwe moja kwa moja kwenye ukarabati wa majengo na kumalizia maboma yaliyoanzishwa na wananchi.

“Lakini, kikubwa ni kuangalia namna gani tunavyoweza kuwa na aina moja ya majengo na tuachane na ujenzi wa majengo ya kutambaa, badala yake tuanze kujenga majengo ya kwenda juu, tena yenye mfanano ambayo yatakuwa yakitengewa bajeti,” amesema Nahodha.

Naye Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei amesisitiza fedha hizo kutolewa kwa uwiano mzuri ili zikaguse maisha ya kawaida ya kila mmoja, ikiwemo umaliziaji wa maboma na ujenzi wa vituo vya afya.

Kwa upande wake mbunge wa Kalambo, Josephat Kandege amesema fedha zilizotolewa kwenye fungu la utawala si kwa ajili ya kupeana chai, badala yake ziende kufanya kazi iliyokusudiwa, na ameomba fedha hizo zitolewe mapema kabla ya Machi ili zikafanye kazi hiyo.

Inaongeza uwazi

Akizungumzia hatua ya Serikali na Bunge, Mhadhiri Mwandamizi wa Shule Kuu ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Thobias Swai  amesema huenda Serikali imepata fedha mahali (nje ya Bajeti iliyotengwa) na imezipelekea bungeni ili kuongeza uwazi.   

“Kila mwaka Serikali hutoa makisio ya mapato na matumizi ambayo hutokana na ahadi walizopewa na wadau wa maendeleo ya makadirio ya makusanyo ya mapato, hivyo baada ya kupata zaidi imeona iweke wazi kupitia maombi ya bajeti ya nyongeza, ili kutoibua maswali hapo baadaye,” amesema Dk Swai.

Dk Swai amesema ni bora Serikali imeamua kuwa wazi, kwani kama isingesema, jambo hilo lingeibuka kwenye vitabu vya Bunge na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Pia, amesema huenda kilichotokea ni kuwa Serikali imepata fedha baada ya kupitisha bajeti na badala ya kusubiri izitumie mwaka wa fedha ujao, imeona ni bora kuzitumia sasa.

Amesema jambo jema ni kuwa fedha hizo zinaelekezwa kwenye sekta muhimu ambazo zina mchango mkubwa katika ustawi wa uchumi wa nchi.