Sababu bidhaa nyingi za nje kupita kanda ya ziwa

Kutokana na uwepo wa bandari katika kanda ya Dar es Salaam, Kanda ya Kaskazini, na Kanda ya kusini Mashariki, kunaweza kukufanya ufikiri tofauti, lakini takwimu zimeonyesha uhalisia.

Ripoti ya Uchumi wa Kikanda ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa robo ya mwaka iliyoishia Septemba 2024, Kanda ya Ziwa imeongoza kwa kusafirisha bidhaa kwenda nje ya nchi, ikichukua asilimia 84.5 ya bidhaa zote zilizotumia mipaka ya Tanzania.

Nyanda za Juu Kusini ilifuata kwa asilimia 10, Kanda ya Kaskazini kwa asilimia 4.5, huku mpaka wa Kusini Mashariki ukishuhudia asilimia 0.3 pekee.

Takwimu hizo zinashangaza kidogo, lakini mchambuzi wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude, anasema kuwa sababu kadhaa zimechangia mabadiliko haya, ikiwemo mivutano ya kisiasa katika baadhi ya nchi jirani, hali ya usalama kwenye baadhi ya maeneo, na uwekezaji wa miundombinu katika Kanda ya Ziwa.

Anasema mpaka wa Tunduma pia huwa unatumika kupeleka bidhaa nchi za kusini wa Tanzania kama Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Zambia na hata Msumbiji, lakini hali ya usalama kwa baadhi ya nchi hizi kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni imekuwa ya kusuasua.

“Ikiwa pamoja na mwaka wa ripoti hii, hali ya kiusalama haikuwa nzuri. Hii pia imechangia kwenye msinyao huu wa bidhaa kupitia mpaka wa Nyanda za Juu Kusini,” anasema.

Wakati haya yanaendelea, lango la Mwanza linalolisha nchi za ukanda wa maziwa makuu hali ya usalama iliendelea kuwa na utulivu wa kawaida ikilinganishwa na mipaka mingine.

“Tofauti hii ilichangiwa pia na kuimarika kwa miundombinu ya uelekeo wa ushoroba huu wa Mwanza, ambao umeleta uchangamfu kwenye biashara na naamini umechangia kwenye hali hii iliyoripotiwa,” anasema Mkude.

Mhadhiri Mwandamizi wa Shule Kuu ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Thobias Swai, anasema uwepo wa madini katika Kanda ya Ziwa pia umechangia ongezeko la shughuli za biashara katika eneo hilo. “Sehemu hii ina madini na migodi, huenda ndiyo sababu ya ufanisi huu”.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 61 ya thamani ya madini yote yaliyouzwa nje ya nchi katika robo ya mwaka iliyoishia Septemba 2024, yalitoka Kanda ya Ziwa, yenye thamani ya Sh581.6 bilioni. Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ilifuatia kwa mauzo ya Sh266.4 bilioni, huku Kanda ya Kati, Kaskazini, Kusini Mashariki na Dar es Salaam zikifuata kwa viwango vya chini zaidi.

Pamoja na madini, bidhaa zinazoharibika haraka kama samaki zimechangia ongezeko la biashara kupitia mipaka ya Tanzania.

Hata hivyo, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ndiyo iliyoongoza kwa uuzaji wa samaki kwa tani, ikishikilia asilimia 28.9 ya mauzo yote, huku ikifuatiwa na Kanda ya Kusini Mashariki. Kanda ya Ziwa ilishika nafasi ya tatu kwa kiasi cha tani 5,822, lakini kwa mapato, iliongoza kwa kupata Sh66.5 bilioni, kiasi kikubwa kuliko kanda nyingine zote.

Katika kipindi hicho, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini iliuza tani 7,680 za samaki, ikifuatiwa na Kusini Mashariki yenye tani 6,835.6, huku Dar es Salaam ikiwa na tani 3,052 na Kanda ya Kati ikirekodi tani 966.4.

Changamoto na fursa za kuboresha biashara ya mpakani

Wakati Kanda ya Ziwa ikizidi kuwa kitovu cha biashara, changamoto bado zinabaki kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao wanachagua kutumia Uwanja wa Ndege wa Kenya kusafirisha bidhaa zao, hasa matunda na mboga, kutokana na gharama nafuu na miundombinu bora.

Msaki Mmari, mfanyabiashara wa matunda na mbogamboga nje ya nchi, anasema bado kuna pengo kubwa katika miundombinu ya Tanzania inayowafanya baadhi ya wafanyabiashara kuhamishia shughuli zao nchini Kenya.

“Tumejitahidi kuboresha miundombinu, lakini bado tuna safari ndefu ili kuwashawishi wafanyabiashara wengi kutumia njia za Tanzania,” anasema.

Takwimu zinaonyesha kuwa biashara ya matunda na mboga inaendelea kukua, huku Tanzania ikiingiza Sh777.24 bilioni kutoka kwenye sekta hiyo mwaka 2023. Mwaka 2024, mapato yaliongezeka hadi Sh1.09 trilioni, na inatarajiwa kufikia Sh1.35 trilioni ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Anapendekeza uwekezaji zaidi katika miundombinu ya usafirishaji na upunguzaji wa gharama za huduma ili Tanzania iweze kufanikisha biashara zake kwa kiwango cha juu na kuimarisha nafasi yake katika soko la kimataifa.

Katika hatua nyingine, baadhi ya wafanyabiashara wanasema kuwa bado kuna changamoto za urasimu kwenye usafirishaji wa bidhaa kupitia mipaka ya Tanzania, hali inayosababisha ucheleweshaji wa bidhaa zinazoelekea nje ya nchi.

Anaishukuru Serikali kuongeza juhudi katika kurahisisha taratibu za forodha na utoaji wa vibali, ili kuharakisha usafirishaji wa bidhaa na kuongeza ushindani wa Tanzania katika biashara ya kimataifa. “Ikiwa uwekezaji mkubwa utafanyika kwenye mnyororo wa usafirishaji wa bidhaa, hasa kwa bidhaa zinazoharibika haraka, Tanzania inaweza kuongeza wigo wa masoko yake na kushindana na mataifa jirani kama Kenya,” anasema Mmari.

Ripoti zinaonyesha kuwa Tanzania imefanikiwa katika kukuza sekta ya mauzo ya nje ya matunda na mboga kwa miaka mitatu mfululizo, jambo linaloashiria umuhimu wa kuimarisha miundombinu na kupunguza gharama za usafirishaji ili kuvutia wafanyabiashara wen

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *