
Hadi kufikia Desemba 31, 2024 deni la taifa la Tanzania lilikuwa limefikia Dola za Marekani 46.56 bilioni (Sh121.45 trilioni), huku Serikali ikichangia asilimia 70.7 ya deni lote.
Ripoti ya mwenendo wa uchumi ya kila mwezi inayotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kuwa katika deni lote la Taifa, deni la nje lilikuwa Dola 32.92 bilioni, huku deni ya la ndani hadi Desemba, 2024 likiwa limefikia Sh32.64 trilioni.
Wakati deni la ndani la Taifa likiongezeka hadi kufikia Sh32.649 katika mwaka ulioishia Desemba 2024, benki za biashara, mifuko ya pensheni na Benki Kuu ndiyo zinaongoza kwa kuidai Serikali.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, fedha zinazokopwa na Serikali kutoka Benki Kuu zinaonekana kupungua, huku zile zinazotoka sehemu nyingine, ikiwemo benki za biashara na mifuko ya pensheni zikiongezeka.
Benki za biashara ndizo zinaongoza kwa kuikopesha Serikali kwa kubeba asilimia 30 ya mikopo yote iliyotolewa katika kipindi hicho, ikiwa na thamani ya Sh9.78 trilioni.
Mifuko ya pensheni ilishika nafasi ya pili kwa kukopesha Sh8.98 trilioni hadi Desemba 2024, ikiwa ni ongezeko kutoka Sh8.55 trilioni iliyokuwapo kipindi kama hicho mwaka uliotangulia, hiyo ilikuwa sawa na asilimia 27.5 ya mikopo yote.
Fedha zilizotoka katika vyanzo vingine ziliongezeka kutoka Sh4.407 trilioni Desemba 2023 hadi kufikia Sh5.59 trilioni mwaka uliofuatia, huku zile zilizotoka katika kampuni za bima zikiwa Sh1.76 trilioni Desemba 2023, kabla ya kufikia Sh1.89 trilioni.
Hata hivyo, wakati fedha zinazokopwa katika sehemu hizo zote zikiongezeka, zile ambazo zinatoka Benki Kuu zilipungua kwa asilimia kutoka Sh6.64 trilioni mwaka 2023 hadi kufikia Sh5.92 trilioni katika mwaka ulioishia Desemba 2024.
Nini maana yake
Akizungumzia suala hili, mtaalamu wa uchumi na biashara, Dk Lutengano Mwinuka alisema ikiwa nchi ina uwezo wa kukopesheka hakuna tatizo, kwani inamaanisha kuwa kile kilichokopwa kitalipwa.
“Ikiwa tunakopa na hatulipi hilo ndilo tatizo, lakini kama inalipwa haina shida yoyote,” alisema Dk Mwinuka, ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),
Hata hivyo, anasema kuna umuhimu wa kuangalia vyanzo vizuri vya kukopa ambavyo havina masharti magumu au riba kubwa ambazo zinaweza kuathiri uchumi kwa namna moja au nyingine.
Alitolea mfano wa matumizi ya njia ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) kuwa inaweza kuwa moja ya njia nzuri za kusaidia kuongeza upatikanaji wa mitaji katika miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali.
Hiyo itaisaidia kupunguza ulazima wa Serikali kwenda kukopa fedha katika maeneo mengine ambayo yanaweza kuwa na masharti mengi.
“Ni vizuri kwenda vyanzo vyenye masharti nafuu kama vilivyopo. Mfano kama hii mifuko ya pensheni inakopesha na watu wanaendelea kulipwa pensheni inawezekana kuwa hali si mbaya, kwani wakati mwingine kuna fedha ambazo huwa zipo huko hazina mipango ambayo imewekwa, hivyo Serikali kuzitumia na kuzirudisha kwa wakati sahihi inakuwa haina shida yoyote,” alisema Dk Mwinuka.
Wakati Dk Mwinuka akiweka mkazo suala la PPP, taarifa iliyotolewa Novemba 11, 2024 na kamishna wa kituo hicho, David Kafulila miongoni mwa miradi iliyosajiliwa, mradi pekee uliofikia hatua ya uwekezaji ni wa Shirika la Maendeleo la Dar es Salaam (DDC).
Kafulila anasema chini ya mpango wa PPP, wanahitajika kuhamasisha mtaji wa binafsi wa Dola 9 bilioni (Sh23.47 trilioni) ili kuwezesha baadhi ya miradi ya ujenzi kuanza.
“Miradi chini ya PPP ipo katika hatua mbalimbali, baadhi ziko kwenye makubaliano, uchunguzi wa kina, tathmini, ununuzi na maelezo ya dhana. Ujenzi wa barabara ya Kibaha hadi Chalinze yenye thamani ya Dola milioni 340 na ujenzi wa barabara za mzunguko zenye thamani ya Dola bilioni moja uko katika hatua nzuri,” alisema.
Tofauti na kilichosemwa na Kafulila, mwaka 2024 pia ulikuwa wa kufanya mageuzi katika sekta ya usafirishaji, hasa katika upande wa reli, baada ya Serikali kuikaribisha sekta binafsi kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya huduma, ikiwemo katika treni ya kisasa (SGR).
Baada ya kuitwa kuchangamkia fursa kwenye SGR, Kampuni sita za Kitanzania tayari zilionyesha nia, ikiwemo GSM, Bakhresa Group, Mohammed Enterprises Company Limited, Lake Oil, Azania na Jambo.
Mbali na SGR, pia Machi 20, 2024, ilishuhudiwa kampuni binafsi ya Bravo ikiingia makubaliano na Tazara yanayohusisha kuingiza treni mbili za mizigo zenye mabehewa 20 kila moja ambapo kila behewa litakuwa na uwezo wa kubeba mzigo wa tani 50 (sawa na malori mawili).
Athari zake
Mtaalamu mwingine wa uchumi wa biashara, Dk Donath Olomi anasema wakati mwingine Serikali inapokopa sana, hasa benki huweza kuchochea kuondoa hamu kwa benki za biashara kukopesha.
Anasema faida ambayo inatolewa katika dhamana za Serikali inakaribia hadi asilimia 13 ambayo huongezeka kutegemeana na miaka ambayo mkopo utalipwa.
“Ni faida kubwa inatolewa, pia ni kama serikali inalipa riba kubwa ili kukopa kwa dhamana za Serikali, hali hii inafanya benki za biashara zinakuwa hazina kiu ya kukopesha sekta binafsi sana na haiwezi kushusha sana riba inapokopesha sekta binafsi,” anasema Dk Olomi.
Anasema ikiwa benki inaona ikiikopesha serikali inapata faida ya asilimia 15, anaona hana haja ya kukopesha mfanyabiashara ambaye anaweza kumsumbua katika kufanya marejesho na wakati wote Serikali haiachi kulipa kwa wakati kwa sababu wasipolipa kila mtu atajua kuwa Serikali haina fedha za kulipa madeni.
“Serikali inapokopa sana kwa kutumia amana, inaiondolea sekta ya ukopeshaji kiu ya kukopesha sekta binafsi na kuondoa kiu ya kushuka kwa riba,” anasema.
Hata hivyo, anasema wakati mwingine Serikali kukopa kupitia benki za biashara za ndani si jambo zuri, kwani huwa hazina mikopo ya muda mrefu na badala yake huwa kati ya miaka mitatu hadi saba.
“Mikopo mingi unarudisha ndani ya miaka mitatu, sasa unapokopa mkopo wa muda mfupi kwa ajili ya kutekelezea miradi mikubwa, ikiwemo ya kimkakati inakuwa ni changamoto, kwani muda wa kurejesha hufika wakati ambao mradi haujaanza kuleta matokeo.”
Alitolea mfano wa reli ya kisasa inayojengwa na mpaka sasa haijakamilika kwa utimilifu wake, huku akisema ikiwa ni mkopo wa ndani ndiyo ungetumika inakuwa ni ngumu kufikia malengo ambayo yalikuwa yamewekwa.
“Mikopo ya miradi hii itoke katika taasisi zinazotoa mikopo ya muda mrefu kama Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wanayoweza kukupa mikopo ya kulipa miaka 20 hadi 40 na kipindi kirefu kabla ya kuanza kurejesha ambayo wakati mwingine inahesabiwa kama ile ya ujenzi, ambalo halipo katika benki ya biashara za ndani.”
Anasema kukosekana kwa muda mrefu wa kurejesha mikopo katika benki za ndani za biashara kunaweka ugumu katika matumizi ya kiasi cha fedha kilichotolewa, hivyo kama ni miradi ya afya, elimu, maji inashindwa kutekelezeka kikamilifu.
Nini kifanyike
Akielezea namna ambayo inaweza kutumika kama mbadala wa kupata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, Dk Olomi anasema ni muda wa kushirikisha wananchi ili waweze kuchangia.
Anasema ni ngumu kuwaambia wananchi wachange fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, lakini zipo njia kama za uuzaji wa hatifungani za Serikali ambazo huweza kutolewa kipaumbele kwao.
Hilo linawezekana kwa Serikali kuweka ukomo wa kiwango kinachoweza kununuliwa na taasisi za fedha ikiwemo mifuko ya pensheni na kuweka nguvu kwa wananchi.