
Dar es Salaam. Kunani usiku? Ni swali linaloweza kuulizwa na wengi kutokana na mabadiliko ya mwenendo wa ushindani katika biashara ya usafirishaji abiria kwa njia ya mabasi, wengi wakihamia safari za usiku na kupunguza za mchana.
Hiyo inathibitishwa na uchunguzi uliofanywa na gazeti dada la Mwananchi, The Citizen, uliobaini baada ya ruhusa ya Serikali kwa mabasi kufanya safari za usiku, wasafirishaji wamehamisha ushindani wao katika safari hizo na kupunguza za mchana.
Safari za mabasi usiku, zilianza rasmi Mei 2024, baada ya marufuku ya miongo kadhaa, tangu miaka ya 1990.
Uchunguzi huo uliofanywa kwa kampuni 40 za mabasi ya mikoani yanayotumia mfumo wa tiketi mtandao, umebaini kati ya mabasi 290 yaliyopangwa kusafiri Machi 7, 2025 kwa safari zinazozidi kilomita 450 kutoka na kuingia Dar es Salaam, asilimia 53 yalipangwa kuondoka usiku.
Kwa mujibu wa ratiba ya safari hizo, mabasi hayo yalipangiwa kusafiri kuanza safari saa 10 jioni au saa 5:59 usiku, huku asilimia 47 yakiwa na safari za mchana.
Uchunguzi huo, unaonyesha kampuni nyingi zimeweka kipaumbele muda wa usiku kwa safari ndefu ili kuongeza urahisi kwa abiria na kuboresha ufanisi wa uendeshaji.
Kampuni zenye idadi ndogo ya mabasi zimeonekana kuzingatia zaidi safari za usiku, hali inayoashiria mkakati wa kuboresha matumizi ya mabasi yao na kukidhi mahitaji ya abiria.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) Salum Pazzy, tangu kuanza kwa huduma za usafiri wa saa 24, jumla ya mabasi 1,950 yamesajiliwa kufanya kusafiri muda huo.
“Ili kuboresha usalama wa abiria, tumeweka masharti maalumu kwa madereva na wamiliki wa mabasi. Madereva wanapaswa kuwa na vyeti vya uthibitisho kutoka Latra na kutumia vitufe vya utambulisho (i-buttons).
“Kutofuata masharti haya kunaweza kusababisha adhabu, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya ratiba za asubuhi,” amesema.
Amesema kati ya Oktoba 2023 na Januari 2024, ajali 205 za barabarani zilirekodiwa, kati ya hizo 61 zilihusisha safari za usiku na 144 zilitokea mchana.
Katika kipindi hicho, Pazzy amesema watu 203 walifariki kutokana na ajali za mchana, huku vifo 65 vikirekodiwa kwenye safari za usiku.
Kwa upande wa majeruhi, amesema 490 walijeruhiwa kwa ajali za mchana, ikilinganishwa na majeruhi 194 waliopatikana kwenye safari za usiku.
Hata hivyo, abiria wengi wameonyesha kupenda safari za usiku kutokana na faida kama kupungua kwa vituo vya mapumziko, msongamano mdogo wa magari barabarani na safari zinazofanyika kwa muda mfupi zaidi.
“Ninapendelea kusafiri usiku kutoka Dar es Salaam hadi Mbeya kwa sababu ninafika asubuhi napata muda wa kutosha kufanya shughuli zangu za kibiashara,” amesema Jenifer Mfilinge anayeishi Mbezi Louis, Dar es Salaam.
Kwa upande wa Esau Mrisho, amesema usafiri wa usiku ni mzuri hasa kwa wenye dharura akifafanua: “Tangu safari za usiku zilipoanzishwa, nazipendelea zaidi kuliko safari za mchana. Safari huonekana fupi kwa sababu nalala njiani.”
Abiria mwingine, Nelson Mbewa amesema safari za usiku zinamsaidia katika dharura.
“Usiku mmoja nilipokea taarifa kuwa mwanangu aliyeko Arusha anaumwa. Nilikata tiketi ya usiku, nikafika asubuhi na nikamleta Dar es Salaam kwa matibabu,” amesema.
Meneja wa Uendeshaji wa BM Coach, Gabriel Makundi amekiri mahitaji ya safari za usiku yameongezeka, hasa kwa zile za umbali mrefu.
“Usiku, idadi ya abiria ni kubwa zaidi kuliko mchana. Njia nyingi za umbali mrefu kama Dar es Salaam–Mwanza, Dar es Salaam–Mbeya, na Dar es Salaam–Arusha zina safari za usiku kutokana na mahitaji makubwa,” amesema.
Makundi amesema BM Coach ina mabasi 12 yanayofanya safari za Dar es Salaam–Arusha, sita husafiri usiku na sita mchana, lakini mabasi yanayosafiri usiku hujaa haraka zaidi.
Amesema kampuni hiyo inapanga kuanzisha huduma mpya ya usiku kati ya Dar es Salaam na Mwanza na kuongeza idadi ya mabasi ya usiku kuelekea Mbeya.
Mabasi yao yote ya usiku, amesema yana kamera za CCTV na madereva wawili kwa kila safari ili kuhakikisha mmoja anapumzika baada ya zamu ya saa nane.
Ofisa Usafirishaji wa Shabiby Line, Edward Magawa amesema mabasi ya usiku yanasafirisha abiria wengi zaidi ikilinganishwa na mchana.
“Wasafiri wengi wa usiku ni wafanyakazi, wafanyabiashara na wenye shughuli za dharura. Safari za usiku zinawapa nafasi ya kutumia muda wa mchana kwa kazi na biashara,” amesema.
Ameongeza Shabiby Line imeagiza mabasi mapya 35 yatakayohudumu kwenye njia za Dar es Salaam–Mwanza, Dar es Salaam–Musoma na Dar es Salaam–Kagera na mengi yatafanya safari za usiku huku mengine yakitumika mchana.
“Mabasi yetu ya usiku kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma na kurudi yana safari 12 kwa siku sita kila upande na mara nyingi huwa yanajaa. Hali ni hiyohiyo kwa safari za usiku kwenye njia kama Dar es Salaam–Moshi, Dodoma–Sumbawanga na safari mpya ya Dar es Salaam–Sumbawanga,” amefafanua.
Amesema upanuzi wa huduma za Shabiby umeongeza ajira na ujio wa mabasi mapya 35 utatoa fursa zaidi za kazi kwa Watanzania.