
KIKOSI cha Simba kimeshatinga visiwani Zanzibar tayari kwa maandalizi ya mechi ya pili ya fainali za Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco, lakini kabla ya kuondoka jijini Dar es Salaam kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids amefanya jambo moja na mastaa na kutoa msimamo.
Fadlu aliyeweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza wa kigeni aliyeifikisha Simba fainali za CAF, amefanya kikao cha saa mbili na wachezaji wa timu hiyo ili kupeana madini kabla ya kuivaa Berkane iliyoizidi ujanja kwa kuwalaza mabao 2-0 na kisha kutoka na maamizio mazito ili kupindua meza.
Simba inarudiana na Berkane Jumapili hii Uwanja wa New Amaan uliopo Unguja ikihitaji ushindi wa mabao 3-0 ili kuweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kutwaa taji la CAF, baada ya awali kushindwa kufanya hivyo mwaka 1993 katika fainali ya Kombe la CAF ikipoteza kwa mabao 2-0 mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast.
Watani wao wa jadi, Yanga ilichemsha msimu wa 2022-2023 wa michuano ya Kombe la Shirikisho kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria baada ya matokeo ya jumla baina ya timu hizo kuwa sare ya mabao 2-2, Yanga ikilala nyumbani 2-1 na kushinda ugenini 1-0.
Inadaiwa, Fadlu aliamua kuitisha kikao hicho jana, ili kuwaweka sawa wachezaji na kuwakumbusha makosa waliyoyafanya yaliyochangia kupoteza mechi ya kwanza ugenini, Simba ikiruhusu mabao mawili ya haraka ndani ya dakika 15 za kwanza na V.A.R ikawaokoa isfungwe la tatu kipindi cha pili.
Simba iliyoondoka na wachezaji karibu wote, akiwamo kipa Aishi Manula ambaye safari ya Morocco hakuwepo katika msafara, itacheza Zanzibar baada ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kuwa kwenye matengenezo yaliyoizuia Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuruhusu mechi hiyo kuchezwa hapo.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imepenyezewa ni, saa chache kabla Simba haijaanza safari hiyo ya Zanzibar, Fadlu alifanya kikao kizito akizungumza na wachezaji wote, huku akiwapa akili mpya kwa kubadilisha saikolojia zao kujiandaa na mechi hiyo ili wakafanye kweli.
Kocha huyo akitumia takribani ya saa 2, aliwataka wachezaji kurudisha akili vitani ili kupigania heshima kwa kuhakikisha wanashambulia kwa nguvu na kujipanga eneo la ulinzi, ili kupindua meza baada ya kupoteza ugenini kwa mabao 2-0.
Inaelezwa kocha aliwaeleza wachezaji, Berkane licha ya kuwa timu bora, lakini mabao iliyoruhusu ugenini yalitokana na makosa yao wenyewe kwa kushindwa kuidhibiti mwenyeji mapema dakika 20 za kwanza, ndiyo maana kipindi cha pili walitulia na kuibana bila kuruhusu bao.
“Kocha anaamini bado Simba ina nafasi kubwa ya kushinda nyumbani, lakini haiwezi kuwa kazi rahisi kama wachezaji watashuka uwanjani wakiwa na hofu na kutojipanga vyema, ndiyo maana alikaa nao kwa muda huo na kupeana mbinu, mbali na kuwashusha presha ya matokeo yaliyoyopita,” kilisema chanzo kutoka Simba.
Hata hivyo, kocha huyo alipotafutwa alithibitisha juu ya kikao hicho na maazimio yaliyotolewa hapo kwa ni ya kuwapa raha mashabiki wa klabu hiyo na kupeperusha vyema bendera ya Tanzania katika fainali hiyo ya kwanza ya CAF kupigwa visiwani Zanzibar tangu michuano hiyo ilipoasisiwa 2004.
Michuano ya Kombe la Shirikisho iliasisiwa mwaka huo kwa kuunganishwa kwa ile ya Kombe la CAF na Kombe la Washindi Afrika tangu Tanzania ipate uhuru hakuna klabu iliyowahi kubeba taji lolote la michuano hiyo mikubwa kwa ngazi za klabu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu alisema, licha ya uamuzi wa CAF wa kuitoa mechi Kwa Mkapa na kuipeleka Zanzibar, lakini amewaambia wachezaji kuhakikisha wanaacha kuonyesha wameonewa na badala yake wakathibitishe ubora wao kwa kushinda kisha kuchukua taji hilo.
Fadlu alisema, Afrika inajua ugumu wa Simba kufungika nyumbani na msimu huu hawana tofauti na RS Berkane kwa kikosi hicho kimecheza jumla ya mechi sita nyumbani bila kupoteza na Jumapili inapaswa kuhitimisha idadi ya mechi zote za msimu huu kwa heshima.
“Simba inahitaji kutoruhusu bao lolote, lakini inatakiwa kupata mabao mawili ili ikiwezekana waende katika penalti kama ilivyokuwa hatua ya robo fainali dhidi ya Al Masry, lakini kubwa ni ushindi wa 3-0 ili kuchukua taji hilo, jambo linalowezekana tukijipanga vizuri,” alisema Fadlu na kuongeza;
“Nimekutana na wachezaji tumezungumza sisi wenyewe kama timu kwa zaidi ya saa mbili, nimewaambia heshima ni kuwathibitishia wale wanaoona wametumaliza, kwa kushinda mechi hii na kuchukua kombe hili.
“Simba inastahili kucheza fainali hii, unapoangalia ubora wetu wa kucheza mechi sita bila kupoteza na kushinda zote utaupata kwetu na wao (Berkane), lakini bahati yao ilicheza fainali nyumbani na sisi tukihamishwa.”
Fadlu alifafanua, aliwaambia wachezaji wa timu hiyo, wasahau yaliyiopita na kujipanga upya kwa masilahi mapana ya heshima ya klabu yao wenyewe (wachezaji) na taifa kwa jumla.
“Hatutakiwi kuendelea kuangalia yaliyofanyika, nimewaambia wachezaji wangu bado tunaweza kwenda Uwanja wa Amaan na kushinda kama tulivyofanya kwenye mchezo wa nusu fainali na hata ule tulikuwa na nafasi ya kuweza kufunga mabao zaidi.” alisema Fadlu na kuongeza;
“Kitu muhimu tunatakiwa kwenda kucheza kwa kushanbulia kwa nguvu kama Simba mwenye njaa, pia tuhakikishe hatufanyi makosa ya kuruhusu bao, hiyo itakuwa hatari, tumejipanga siwezi kusema tumefanya nini watu wataona uwanjani.”
DAKIKA 90 NGUMU
Simba ina dakika 90 ngumu mbele ya Berkane, kutokana na rekodi walizonazo kwa mechi za ugenini, kwani imecheza mechi sita, ikishinda nne kutoka sare moja na kupoteza moja tu, huku ikiwa imeruhusu mabao mawili tu katika jumla ya mechi 13 za msimu huu za michuano hiyo ya CAF.
Berkane ilipoteza 1-0 mbele ya CS Constantine ya Algeria katika mechi ya nusu fainali, lakini iliruhusu bao jingine moja ilipoifunga Stellenbosch ya Afrika Kusini hatua ya makundi kwa mabao 3-1, huku kipa wa timu hiyo Munir Mohammed akiongoza kwa cleensheet nane katika mechi 11 alizodaka.
Hata hivyo, rekodi tamu za Simba ikiwa nyumbani na hata kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar unaifanya mashabiki wa klabu hiyo kutokuwa na presha, licha ya kulikosa lile vaibu lililozoeleka Kwa Mkapa kwa mechi zenye maamuzi kama hiyo ya fainali hizo za Shirikisho Afrika.
Simba inatakiwa kuwabana Berkane dakika 20 za kwanza na 20 nyingine za mwisho kwani ndio huwa hatari zaidi na bahati nzuri, Kocha Fadlu analijua hilo na alishazungumza na wachezaji kukaa mguu sawa, huku wakitafuta mbinu za kumdhibiti kiungo Mamadou Camara aliyeivuruga ugenini.
Kiungo huyo ‘ngongoti’ katika mechi ya mjini Berkane aliipelekesha Simba atakavyo, kitu ambacho Fadlu huenda asingetamani kuona kinatokea nyumbani, huku safu ya mbele ikiwa na kibarua cha kutumia kila nafasi itakayotengeneza, kwa vile inacheza nyumbani tofauti na mechi iliyopita iliposhindwa kulenga lango kwa vile ilikuwa ugenini na ilijihami zaidi.
AHOUA NA KIBU
Nyota wa timu hiyo wanaoongoza kwa mabao, Kibu Denis na Jean Charles Ahoua ambao kila mmoja amefunga matatu, hii ni mechi ya kuweka heshima ili kumaliza kama vinara wa ufungaji kurejea kile kilichofanywa na Fiston Mayele msimu ambao Yanga ilifika fainali alipofunika CAF.
Mayele alimaliza michuano hiyo akiwa na mabao saba, mbali na saba mengine aliyofunga hatua ya awali na kuwa Mfungaji Bora, hivyo kwa Kibu na Ahoua aliyefunga bao lililoitupa nje Stellenbosch katika nusu fainali wana deni la mabao mawili dhidi ya vinara wanaoongoza orodha ya sasa.
Lamlioui Oussama wa Berkane na Ismail Belkacemi wa USM Alger, kila mmoja ana mabao matano, huku Ifeanyi Ihemekwele wa Enyimba iliyoaga michuano mapema kama USMA yeye amefunga manne, ikiwa ni moja zaidi na waliyonayo Kibu na Ahoua.
Nyota wengine wa Simba wenye nafasi ya kuweka heshima kama walikomaa Jumapili na Leonel Ateba anayemiliki mabao mawili kwa sasa, lakini kitu ya kila Mwanasimba ni kuona timu hiyo inamaliza kibabe kwa kubeba ubingwa na kujihakikishia kiasi cha Sh 5.4 Bilioni za bingwa wa kombe hilo.
Ukiacha fedha hizo za ubingwa kutoka kwa wadhamini wa michuano hiyo, lakini mastaa hao wa Simba wana kazi ya kutupia mabao ili kuvuna fedha za ‘Goli la Mama’ na kila moja ni Sh30 milioni, mbali na fedha zilizoahidiwa na wadau mbalimbali wa klabu hiyo kwa kila bao litakalofungwa.