
Dar es Saalam. Namna ambavyo muziki wa Bongo Fleva unavyozidi kupaa. Nyuma yake kuna kazi kubwa ya maproduza wanaofanya vizuri akiwamo Salim Rashid Kassim ‘S2Kizzy.
Jina hilo sio geni kwenye masikio ya watu. Kazi zake zinamtambulisha kutokana na muziki mzuri anaoutengeneza kwenye studio yake ya Pluto Records.
Akizungumza na Mwananchi S2Kizzy amesema wimbo uliomtambulisha kwenye gemu ni wimbo wa Country Boy ‘Hakuna Matata’ na Turn Up
Ugumu gani ulipata wakati anaanza?
“Ugumu mkubwa ilikuwa ni mazingira magumu ya kufanyia kazi na kuwapata wasanii. Unajua hizi kazi zetu hadi ukubalike inahitajika sana uvumilivu na umakini wa hali ya juu sana.
“Kikubwa ni kujituma, kufanya kazi kwa bidii na ubunifu. Ili mtu ufanikiwe, lazima utafute vitu vipya.Pia kemistri ya wasanii inafanya hata ngoma zikitoka ziwe na mapokeo makubwa,”amesema
Kuna tofauti gani kati ya kufanya kazi na wanamuziki wa nje ya Bongo na hapa nchini?
“Aisee! utofauti ni mkubwa, kwa sababu kila msanii ana kazi zake na anajua jinsi anavyofanya kazi na ana njia zake za biashara. Hata prodyuza, unajifunza njia nyingi kupitia huyo msanii. Pia kujifunza tamaduni mbalimbali,”amesema
Mambo gani ya kuzingatia ili kuwa prodyuza?
“Kwanza unatakiwa umfanye msanii awe huru kufanya kazi na wewe na upya kwenye kazi zako,”amesema
Umefanya kazi nyingi za wasanii wa Wasafi hasa Mondi, je, koneksheni ipo vipi hapo?
“Ni kuonekana kwa bidii za kazi na siwezi kusema kufanya kazi na Diamond ni kwa sababu ya ukaribu, yule ni msanii mkubwa na anapenda kazi nzuri na mafanikio makubwa,”amesema
Kuna ugumu gani kufanya naye (Diamond) kazi?
“Naweza kusema ugumu upo kidogo kwa sababu anapenda vitu vyake viwe bora, si changamoto sana kwa sababu anapenda vitu vipya na ujitume kufanya naye kazi.”
Tangu umeanza kufanya kazi na Mondi, ni kipi unaweza kujivunia?
“Faida ni nyingi sana, Diamond ni msanii mkubwa, kuwa naye karibu anakufanya ung’are na kuonekana hata nje ya Bongo, maana anafuatiliwa na watu wengi duniani, kufanya naye kazi kumenifanya kujua vitu vingi na hata koneksheni pia maana anajua vitu vingi sana.”
Kitu gani hupendi kutoka kwa wasanii?
“Sipendi bifu za wanamuziki zinaniwia ugumu wa kufanya kazi, yaani utaona msanii huyu ana kemisti na huyu ila hawaelewani na mimi nakuwa nishaona wana kuna kitu wakifanya kazi kwa pamoja, hii huwa inakata sana”
Una mipango gani ya kufanya na wasanii wa kimataifa
“Nina mikakati ni mingi maana wasanii wengi wananitafuta na hiyo inafanya kukua zaidi na kuonekana ni bora kwenye kazi zangu.”
Ni wasanii wangapi wa kimataifa tayari umefanya nao kazi
“Wapo wengi ila kwa Nigeria nimefanya na Davido, Burna Boy na wengine kutoka Rwanda, Afrika Kusini, Burundi na Sudan.”
Umefanya kazi nyingi na wakongwe wa muziki, utofauti uko wapi ukilinganisha na wasanii wa sasa?
“Utofauti ni kwa kila msanii jinsi ya kufanya kazi hasa kwenye ‘sound’”
Kumekuwa na madai ya kazi za nje ‘biti’ kuibiwa na wasanii hasa maprodyuza, kwako ikoje hii?
“Hicho kitu kipo kwa baadhi ya watu, ila kwa upande wangu sijawahi kuiba, ukiona nimepiga biti imeendana, ni kwa sababu ndani yake kuna kitu.”
Kuna changamoto gani kwenye kazi yako?
“Changamoto zipo hasa kwenye haki miliki, ila zingine ni za kawaida tu.”
Unajivunia nini kwenye kazi zako?
“Nafuatiliwa na watu wengi kutokana na kuwa na koneksheni kubwa. Pia nahamasisha vijana, na kuongeza studio nyingine mbili so nina tatu “