Rwanda yasindikiza majeshi ya SADC kuondoka DRC

Goma. Jeshi la Rwanda limeisindikiza misafara ya majeshi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yakitoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuelekea Tanzania, kufuatia uamuzi wa kumaliza operesheni ya kijeshi ya SAMIDRC.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Jumanne Aprili 29, 2025 na Msemaji wa Jeshi la Rwanda, Brigedia Jenerali Ronald Rwivanga imesema misafara hiyo ilijumuisha magari takribani 20 yenye wanajeshi na vifaa vya kijeshi kutoka Tanzania na Afrika Kusini, na ilipita salama kupitia mji wa mpakani wa Gisenyi kabla ya kuingia nchini Tanzania.

Hatua hiyo inakuja wakati hali ya usalama mashariki mwa DRC ikiendelea kuzorota, huku waasi wa M23 wakiishikilia miji mikuu kama Goma na Bukavu. Mashambulizi ya mara kwa mara yamewaacha maelfu ya raia wakikimbia makazi yao na mamia kupoteza maisha.

SADC ilianzisha kikosi cha SAMIDRC Desemba 2023 kusaidia Serikali ya DRC kupambana na makundi ya waasi, lakini kufuatia hali ngumu ya kiusalama na changamoto za utekelezaji, mkutano wa viongozi wa SADC ulitangaza kumaliza operesheni hiyo mwanzoni mwa mwezi huu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe katika mtandao wa X ameandika, “Uwepo wa majeshi ya SAMIDRC ulikuwa changamoto katika mzozo huu, na kuanza kwa zoezi la kuondoka leo ni hatua nzuri katika mchakato wa amani unaoendelea.”

Rwanda yashika usukani wa usalama wa kuvuka mpaka

Uamuzi wa Rwanda kusindikiza majeshi hayo umeibua mjadala, hasa kutokana na tuhuma za muda mrefu kuwa inawaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo Serikali ya Rwanda imekuwa ikikanusha vikali.

Hata hivyo, watoa maoni wa kimataifa wameeleza kuwa hatua hiyo inaonesha nia ya Rwanda kulinda usalama wa eneo lake na kushiriki katika mpito wa amani.

Mazungumzo ya amani yaendelea

Wakati wanajeshi wakirejea makwao, juhudi za kutafuta suluhu ya kudumu zinaendelea chini ya usuluhishi wa Angola na Qatar. Makubaliano ya awali yamesainiwa na pande husika, yakiweka msingi wa kuandaliwa kwa mkataba wa amani unaotarajiwa Mei 2, mwaka huu.

Wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema kuwa kuondoka kwa vikosi vya SADC kunaweza kuongeza ombwe la kiusalama mashariki mwa DRC, hasa iwapo hakuna mpango mbadala madhubuti wa kulinda raia na kudhibiti waasi.

Hata hivyo, mashirika ya kiraia na viongozi wa kimataifa wametoa wito kwa mataifa ya Maziwa Makuu kushirikiana zaidi kuimarisha amani, wakisema kuwa changamoto ya DRC siyo ya nchi moja bali ya kanda nzima.

Imeandikwa na Evagrey Vitalis kwa msaada wa Mashirika

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *