Rwanda inadai kuwa DRC ilishirikiana na baadhi ya nchi wanachama wa ECCAS kuizuia kuchukua nafasi ya uenyekiti wa jumuiya hiyo.
Kwa mujibu wa Kigali, nafasi hiyo kwa sasa inashikiliwa na Equatorial Guinea, ingawa muda wake wa uongozi unatarajiwa kumalizika mwaka huu.
Katika taarifa kali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda, serikali ya Kigali imesema kuwa DRC, kwa msaada wa baadhi ya nchi wanachama, ilitumia jukwaa la ECCAS kufanikisha maslahi yake ya kisiasa.
Tuhuma hizi zimekuja kufuatia Mkutano wa 26 wa wakuu wa nchi na serikali wa ECCAS uliofanyika Jumamosi mjini Malabo, Equatorial Guinea.
Kwa mujibu wa Rwanda, wakati wa mkutano huo ilipaswa kuwa zamu yake ya kuchukua uenyekiti wa mzunguko wa ECCAS, kama inavyotambuliwa chini ya Kifungu cha 6 cha Mkataba wa jumuiya hiyo.
Hata hivyo, hatua hiyo ilipuuzwa kwa makusudi na uongozi huo kuongezewa kwa mwaka mmoja zaidi kwa Equatorial Guinea.
DRC yakwamisha mikutano inayofanyika Kigali
Rwanda inasema kuwa wakati wa maandalizi ya mkutano huo, maafisa wa DRC walidai kuwa hawatashiriki mikutano yoyote ambayo ingetakiwa kufanyika Kigali endapo Rwanda ingechukua uenyekiti.
Kwa msingi huo, kikao cha marais na wakuu wa serikali kilipitisha uamuzi wa kuendelea na uongozi wa Equatorial Guinea kwa mwaka mmoja zaidi.
Akizungumza kupitia televisheni ya taifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, alisema:
“Jumuiya ya ECCAS kwa kukubali kutumiwa na nchi moja pekee na kuweka uwezo wake wa maamuzi mikononi mwa nchi moja, ni jambo lisilokubalika.
Ndiyo maana tumeamua kujiondoa katika ECCAS, hatuwezi kubaki katika jumuiya isiyotenda haki.”
Nduhungirehe aliongeza kuwa mfumo wa utawala wa ECCAS una changamoto nyingi ambazo zimeifanya jumuiya hiyo kuwa miongoni mwa zisizofanya kazi barani Afrika.
“ECCAS ni moja ya jumuiya zisizofanya kazi kabisa. Ukitazama miundombinu, ushirikiano, utawala, tuna mwenyekiti wa tume ambaye hafanyi kazi wala kushirikiana na makamishna wengine,” aliongeza Waziri huyo.
Siasa za ndani Rwanda zaiunga mkono serikali
Uamuzi wa Rwanda kujiondoa ECCAS umepokelewa kwa maoni mseto ndani ya nchi hiyo, huku baadhi ya viongozi wa kisiasa na wanazuoni wakiunga mkono hatua hiyo ya serikali.
Evode Uwizeyimana, Seneta katika Bunge la Rwanda, alisema:
“Ni kana kwamba tayari wanajua tarehe ambayo mgogoro wa DRC utamalizika. Uamuzi wao wa kuahirisha uenyekiti wa Rwanda ni kinyume kabisa na sheria za jumuiya hii. Wameharibu kabisa.”
Hatua ya Rwanda kujiondoa katika ECCAS inahatarisha zaidi juhudi za kidiplomasia za kutafuta amani katika eneo la Maziwa Makuu.
Serikali ya Rwanda inasema kuwa wakati juhudi za diplomasia zikiendelea huko Washington, DRC imekuwa ikiendeleza kampeni ya kuiweka Rwanda katika hali ya kutengwa kimataifa.
Kwa upande wake, serikali ya DRC imeshutumu uamuzi wa Rwanda, ikisema kuwa huo ni mkakati wa Kigali wa kukwepa uwajibikaji kuhusu migogoro inayoendelea mashariki mwa Congo.
Katika taarifa yake, Kinshasa imesisitiza kuwa hatua ya Rwanda inaweza kuhatarisha mstakabali wa amani katika ukanda wa Maziwa Makuu, na kwamba jumuiya ya kimataifa inapaswa kuchukua tahadhari juu ya mwenendo wa Kigali.