Rwanda yaipinga SADC, yadai Tshisekedi ana mpango wa kumpindua Kagame

Kigali. Nchi ya Rwanda imekanusha taarifa iliyodai kutolewa na mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kuhusu uhusika wake na machafuko yanayoendelea Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC).

Licha ya kukanusha madai hayo, imeinyooshea kidole DRC ikiishutumu kutaka kuipindua Serikali ya Rwanda iliyopo madarakani.

Hayo yameelezwa leo Jumapili Februari 2, 2025 kupitia taarifa iliyotolewa na kupostiwa katika mtandao wa X wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda.

“Rwanda inakana shutuma dhidi ya Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) iliyotolewa katika taarifa ya mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Januari 31, 2025. RDF inatetea mipaka ya Rwanda dhidi ya vitisho na inalinda raia, haiwashambulii.

“SADC imetuma kikosi cha mashambulizi, SAMIDRC, kusaidia vita vya Serikali ya DRC dhidi ya watu wake wenyewe, M23 na wanachama wa jumuiya yao wengi wao wamekimbilia kama wakimbizi nchini Rwanda na katika kanda nzima. Serikali ya DRC pia ina nia ya kushambulia Rwanda na kupindua serikali yake, kama ilivyosemwa mara kwa mara na hadharani na Rais Tshisekedi,”imeeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa SAMIDRC pamoja na washirika wa muungano ambao ni vikosi vya Jeshi la Burundi, FDLR na mamluki wa Ulaya ni kiini cha mzozo huo, na hawapaswi kuwepo kwa sababu wanaongeza matatizo ambayo tayari yalikuwepo.

“Hoja ya kwamba SAMIDRC ilialikwa na Serikali ya DRC imebatilishwa na ukweli kwamba wapo kwa ajili ya kupigana na raia wa nchi hiyo, na kuleta vita kwa Rwanda,”imeeleza taarifa hiyo.

Pia, Rwanda imedai lengo la vurugu zinazoendelea DRC sio kuwashambulia M23 pekee bali kuipiga Rwanda.

“Mashambulizi yaliyopangwa pamoja na majeshi ya kigeni yanayopigana mashariki mwa DRC, ikiwa ni pamoja na FDLR, yanaonyesha kuwa malengo ya mapambano hayakuwa tu kuwashinda M23, lakini pia mashambulizi kwa Rwanda,”imeeleza taarifa hiyo.