Ndani ya siku chache tu tangu kuundwa kwa M23, mapigano makali yalizuka kati ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na waasi wa M23 katika wilaya ya Rutshuru.
Katika muda wa takriban wiki tatu baada ya M23 kuanzishwa, vita kati yao na jeshi la DRC vilisababisha zaidi ya raia 30,000 kuyakimbia makazi yao na kuhamia mataifa jirani ya Rwanda na Uganda.
Ijumaa, Juni mosi, 2012, wakati mapigano yakiendelea kati ya waasi wa M23 na jeshi la serikali, wakazi wa jamii ya Watutsi katika mji mdogo wa Kitchanga walianza kuhama makazi yao kwa hofu ya kushambuliwa na waasi wa Kihutu wa Rwanda wa FDLR waliokuwa wakijikusanya katika maeneo ya mji huo.

Ndani ya wiki mbili baadaye, Jumanne ya Juni 12, 2012, Marekani ilisema inaiunga mkono DRC katika vita dhidi ya waasi wa kundi la M23 pamoja na juhudi za kurejesha amani katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo. Wakati huo huo, ripoti kutoka Bunagana, mji uliopo mpakani mwa Uganda, zilidokeza kuwa waasi hao wamevunja bomba linalosambaza maji katika mji huo, uliokuwa na wakimbizi wengi.
Mwezi uliofuata, Jumamosi ya Julai 14, 2012, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) iliyopo The Hague, nchini Uholanzi, ilitangaza kuwa imetoa hati ya kukamatwa kwa Sylvestre Mudacumura, kiongozi wa waasi wa Kihutu kutoka Rwanda aliyekuwa akiishi DRC, na hati mpya ya kukamatwa kwa Bosco Ntaganda, mwanzilishi wa M23.
Wakati huo huo, serikali ya DRC ikaishutumu Rwanda kwa kutoa fedha kwa kundi hilo, pamoja na silaha na vikosi vya jeshi kuwasaidia wanamgambo wa Ntaganda, ambao walikuwa wamekamata miji kadhaa katika jimbo la Kivu ya Kaskazini katika siku chache tangu kundi hilo lilipoanzishwa Jumatano ya Aprili 4, 2012, na sasa lilionekana kuwa linatishia kuukamata mji mkuu wa jimbo hilo, Goma.
Ntaganda, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 39, alituhumiwa na ICC kufanya uhalifu wa kivita pamoja na uhalifu dhidi ya binadamu, kuanzia Jumapili ya Septemba mosi, 2002, hadi Septemba 2003.
Mahakama hiyo tayari ilikuwa imetoa hati ya kukamatwa kwake mwaka 2006 kwa kuwatumia watoto katika jeshi lake, lakini sasa ikaongeza mashtaka mengine na hati nyingine ya kumkamata.
Mahakama ya ICC ilisema Ntaganda alikabiliwa na mashtaka matatu ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na manne ya uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji na utumwa wa ngono, mateso, uporaji na utekaji nyara.
Ntaganda alizaliwa nchini Rwanda Jumatatu ya Novemba 5, 1973, na alikuwamo katika jeshi la Rwandan Patriotic Forces (RPF), lililokuwa linaongozwa na Rais wa sasa, Paul Kagame, ambalo lilimaliza mauaji ya kimbari mwaka 1994 yaliyofanywa na Wahutu wenye msimamo mkali dhidi ya Watutsi walio wachache nchini Rwanda.
Wataalamu wanasema kuwa Ntaganda, ambaye alijumuishwa katika jeshi la DRC pamoja na kundi lake la waasi wa Kitutsi katika makubaliano yaliyoshindwa ya Machi 23, 2009, alijitoa katika jeshi hilo Aprili 4, 2012, wakati serikali mjini Kinshasa ilipokiondoa kikosi chake kutoka katika maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini.
Serikali ya Kinshasa na ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa ilisema kuwa kuna ushahidi mkubwa wa ushiriki wa Rwanda katika uasi wa kundi la M23, dai ambalo Rwanda inakana.
Umoja wa Mataifa na viongozi wa eneo hilo waliwataka viongozi wa Rwanda na DRC kukaa chini na kufikia makubaliano ambayo yatazuia kuongezeka kwa vita hivyo katika eneo la Kivu ya Kaskazini, ambalo tayari limeathirika kwa vita iliyosababisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao.
Jumatano ya Februari 27, 2013, mgawanyiko ulizuka kati ya vikundi vya M23 nchini DRC. Kama matokeo, kiongozi wa kisiasa wa M23, Jean-Marie Runiga Lugerero, alifukuzwa na kushtakiwa kwa uhaini kwa sababu ya ubadhirifu wa fedha, migawanyiko, chuki za kikabila, udanganyifu na kutokomaa kisiasa.
Sultani Makenga alijitangaza kuwa kiongozi wa muda, jambo lililozua mapigano kati ya wale waliomtii Sultani Makenga na wale waliomtii Jean-Marie Runiga Lugerero, ambaye alikuwa akishirikiana na mwanzilishi wa M23, Bosco Ntaganda.
Baada ya wiki kadhaa za mapigano ndani ya M23, mamia ya waasi wa DRC wanaomtii Ntaganda walikimbilia nchi jirani ya Rwanda au kujisalimisha kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa. Huko, Jean-Marie Runiga Lugerero, ambaye pia alikimbilia Rwanda, alikamatwa na kutiwa kizuizini na mamlaka ya Rwanda kwa usalama wake.
Hivyo, Ntaganda alijisalimisha baada ya wanajeshi wake kushindwa na kundi hasimu la M23 la Sultani Makenga Machi 16, 2013, ambao wapiganaji wake waliuteka mji wa Kibumba, yapata kilomita 30 kaskazini mwa Goma, mji mkuu wa jimbo lenye utajiri wa madini la Kivu Kaskazini.
Sultani Makenga alitoroka jaribio la mauaji Februari 22, 2013, ambalo lilikuwa limeandaliwa na Jenerali Ntaganda kutokana na mvutano ulioendelea kati ya waasi wa M23 watiifu kwa kamanda wa zamani wa CNDP, Jenerali Laurent Nkunda, na wale watiifu kwa Jenerali Bosco Ntaganda.
Baada ya mambo kumwendea vibaya, Jumatatu ya Machi 18, 2013, Jenerali Ntaganda, ambaye alikuwa mhimili wa mgogoro wa Kaskazini mwa DRC, alijisalimisha katika ubalozi wa Marekani mjini Kigali, nchini Rwanda.
Ijumaa ya Machi 22, alipelekwa katika mahabusu ya ICC mjini Kigali na kesho yake kusafirishwa hadi katika uwanja wa ndege wa mjini Rotterdam.
Mahakama ya ICC ilisema baada ya Ntaganda kuwasili katika kituo cha kuwahifadhi watuhumiwa cha ICC, akiwa chini ya ulinzi wa polisi wa Uholanzi katika kitongoji cha mji wa The Hague cha Scheveningen. Alikuwa mtuhumiwa wa kwanza kujisalimisha kwa mahakama hiyo.
Jumatatu ya Februari 10, 2014, majaji wa ICC walianza kusikiliza ushahidi dhidi ya Ntaganda katika kikao kifupi ili kubaini iwapo kesi inayomkabili ingeendelea kusikilizwa. Hata hivyo, alikutwa na kesi ya kujibu na hivyo iliendelea kusikilizwa hadi Juni 12, 2017, alipoanza kujitetea.
Alhamisi ya Julai 8, 2019, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilimtia hatiani kiongozi wa zamani wa waasi John Bosco Ntaganda kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), baada ya kupatikana na hatia ya makosa 18 ya uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya binadamu, ikiwamo makosa ya mauaji, ubakaji na kuwasajili watoto jeshini yaliyotekelezwa Ituri nchini DRC kati ya mwaka 2002-2003.
Majaji Robert Fremr, Jaji Kuniko Ozaki na Jaji Chang-Ho Chung walitangaza hukumu hiyo katika kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa hadharani kwenye mahakama ya ICC iliyoko mjini The Hague, Uholanzi.
Majaji hao wamesema Ntaganda, mwenye umri wa miaka 45, “kiongozi mkuu wa waasi alikuwa akitoa amri kuwalenga na kuwaua raia.”
Ingawa huo ulikuwa ni mwisho wa mmoja wa waanzilishi wa M23, haukuwa mwisho wa M23. Nini kilichojiri?
Tukutane kesho katika sehemu unayofuata