Moscow. Mahakama nchini Russia imemuhukumu raia wa Uingereza aliyekamatwa akipigana upande wa Ukraine mkoani Kursk kifungo cha miaka 19 jela.
Raia huyo, James Scott Rhys Anderson (22), alikutwa na hatia kwenye shitaka la kuwa ‘mamluki’ na shitaka la ugaidi katika kesi iliyokuwa ikisikilizwa kwenye Mahakama ya kijeshi nchini Russia.
Anderson alikamatwa Novemba 2024 mkoani Kursk akisaidiana na vikosi vya Ukraine kufanya uvamizi wa maeneo ya Russia. Alikiri mashitaka yote yaliyomkabili kisha kuhukumiwa adhabu hiyo.
Kulingana na hukumu hiyo, Anderson atatumikia miaka mitano gerezani kabla ya kuhamishiwa kwenye eneo lenye kazi ngumu (penal colony) atakakoenda kumalizia kifungo chake.
Video iliyotolewa na mahakama imemuonyesha, Anderson aliyehukumiwa jana (Jumatano) akitikisa kichwa kimya baada ya kusomewa hukumu hiyo.
Baada ya kuanikwa kwa hukumu hiyo, Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza imelaani uamuzi huo wa mahakama ikisema raia huyo wa Uingereza amehukumiwa kwa misingi ya mashitaka ya uongo.
“Kulingana na sheria za kimataifa, wafungwa wa vita hawawezi kushtakiwa kwa kushiriki mapigano,” amesema msemaji wa ofisi hiyo.
“Tunaitaka Russia iheshimu wajibu wake, ikiwa ni pamoja na Mikataba ya Geneva na kuacha kutumia wafungwa wa vita kwa madhumuni ya kisiasa na propaganda,” amesema.
Mwaka 2022, mahakama mkoani Donetsk iliwahukumu raia wawili wa Uingereza na Morocco, adhabu ya kifo kwa kushiriki kama mamluki wa kigeni na kufanya shughuli za kigaidi nchini Russia.

Hata hivyo, wanaume hao watatu waliachiwa baadaye kama sehemu ya mabadilishano ya wafungwa yaliyosimamiwa na Saudi Arabia.
Akizungumza muda mfupi baada ya uvamizi kamili wa Russia nchini Ukraine Februari 2022, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine wakati huo, Dmytro Kuleba, alisema zaidi ya watu 20,000 kutoka nchi 52 walikuwa wamejitolea kuipigania Ukraine.
Tangu Russia itangaze operesheni zake za kijeshi imeyatwaa maeneo ya Mkoa wa Donetsk, Luhansk, Kherson, Zaporizhia, Pokrovisk na Crimea iliyotwaliwa tangu mwaka 2014.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.