
Ubalozi wa Russia mjini Tehran umekosoa hatua ya nchi za Magharibi dhidi ya Iran katika Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA).
Ubalozi wa Russia mjini Tehran jana Jumapili ulitoa taarifa na kukosoa hatua za kichochezi za Marekani, Uingereza, Ujerumani na Ufaransa dhidi ya Iran katika kikao cha Bodi ya Magavana ya IAEA na kutangaza kuwa, azimio lililopendekezwa na nchi tatu za Ulaya yaani Uingereza, Ufaransa, Ujerumani pamoja na Marekani dhidi ya miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani na kupasishwa na Bodi ya Magavana ya wakala wa IAEA ni jitihada za kuzidisha mivutano na kupotosha mazingitio ya walimwengu kuhusu mgogoro wa Gaza.
Taarifa ya ubalozi wa Russia mjini Tehran imeeleza kuwa, Russia inapinga wazi azimio la uchochezi wa Marekani, Uingereza, Ujerumani na Ufaransa katika Bodi ya Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki. “Azimio hilo halifai kabisa na halina manufaa yoyote katika kujenga maelewano mazuri kati ya pande za Iran na wakala wa IAEA,” imeongeza taarifa ya ubalozi wa Russia nchini Iran.
Azimio hilo lililopasishwa na Bodi ya Magavana ya IAEA bila ya kuashiria ushirikiano wa Iran na wakala huo limeitaka Tehran kuchukua hatua za dharura na haraka ili kupatia ufumbuzi masuala ya ulinzi yanayodaiwa.