Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema mkataba wa ushirikiano wa kimkakati na mpana kati ya nchi yake na Iran utajumuisha pia ushirikiano katika sekta ya ulinzi na usalama.
Akizungumza na shirika la habari la TASS la Russia mapema leo, Andrei Rudenko amesema hatatoa ufafanuzi wa makubaliano hayo ambayo yanatarajiwa kutiwa saini siku za usoni.
“Niashirie tu kwamba utakidhi changamoto na mahitaji ya wakati wetu na utashughulikia karibu nyanja zote za sasa na zinazotarajiwa za ushirikiano wa Russia na Iran, zikiwemo za ulinzi na usalama,” ameeleza Rudenko.
Mnamo 2001, Tehran na Moscow zilitia saini mkataba wa ushirikiano wa muda mrefu, unaojulikana rasmi kama Mkataba wa Msingi wa Mahusiano ya Pamoja na Kanuni za Ushirikiano. Hapo awali mkataba huo ulipangwa kuwa wa miaka 10 lakini ukarefushwa hadi 2026.
Sasa hivi, pande hizo mbili zinakamilisha maandalizo ya mwisho kwa ajili ya mkataba huo wa ushirikiano wa kina, ambao unaweza kuamua uhusiano wa nchi mbili katika nyanja zote kwa miaka 20 ijayo.

Mwezi uliopita, Balozi wa Iran nchini Russia Kazem Jalali alisema mkataba wa ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi mbili utatiwa saini wakati wa ziara ya Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Moscow. Tarehe ya ziara hii bado haijaamuliwa.
Iran na Russia zote mbili zinakabiliwa na vikwazo haramu vya Magharibi. Kwa miaka kadhaa sasa Tehran na Moscow zimeimarisha uhusiano wao katika nyanja mbalimbali, zikiwemo za kijeshi na ulinzi, na kuwa washirika wa karibu…/