Mwanza. Ripoti ya ufuatiliaji wa vitendo vya rushwa uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) imebaini ongezeko la vitendo vya rushwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 ikilinganishwa na mwaka 2019.
Kwa mujibu wa Kamusi ya Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) ya mwaka 2022, Rushwa ni mali, pesa au zawadi yoyote apewayo mtu mwenye cheo au nafasi ya utawala, kiuchumi, kijamii au kisiasa ili kukutendea jambo ijapokuwa jambo hilo ni haki yako.

Akiwasilisha ripoti hiyo kwenye kikao cha wadau wa uchaguzi kilichofanyika Aprili 29, 2025, Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa Takukuru, Sabina Seja alisema taasisi hiyo ilipokea malalamiko 135 na kufuatilia matukio 122 kuhusu rushwa na viashiria vya rushwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.
“Malakamiko yalihusu kutoa na kupokea hongo, taratibu za uchaguzi kutozingatiwa, kusafirisha wapiga kura, kushawishi wagombea kujitoa, kuruhusu wasio kwenye orodha ya wapiga kura kuruhusiwa kupiga kura. Malalamiko 110 yalihusu wanachama na mengine 25 yalikuwa dhidi ya wasio wanachama wa vyama vya siasa,” alisema Seja.

Seja alisema baada ya ufuatiliaji imebainika kwamba vitendo vya rushwa kwa kugawa fedha vimeongezeka hadi kufikia asilimia 65 mwaka 2024, ikilinganishwa na asilimia 64.4 kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019.
Alitaja maeneo mengine kuwa ni kugawa vyakula na vinywaji (asilimia 26), kugawa vitenge na fulana (asilimia 7), kununua wagombea (asilimia moja) na rushwa ya ngono asilimia moja).
“Kuwepo kwa vitendo vya rushwa wakati wa kuchagua viongozi, huwanyima haki wagombea na wananchi na kukamisha jitihada za Serikali kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki kwa mwananchi kumchagua kiongozi amtakaye kupitia sanduku la kura,” alisema mkurugenzi huyo wa uchunguzi.

Kuhusu nafasi zilizolalamikiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa , Seja alisema nafasi ya mwenyekiti wa kijiji iliongoza kwa asilimia 51, mwenyekiti wa serikali ya mtaa (24), mwenyekiti wa kitongoji (20) na wajumbe wa ngazi zote (tano).
“Imebainika kwamba mbinu za vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi kuwa ni kugawa fedha kwa wapigakura, kutoa mikopo, bima za afya, kujaza mafuta kwenye pikipiki, kufadhiri vikao kwa posho na malazi, kuchagia katika ofisi za chama cha siasa, kugawa simu, vishikwambi, kofia, fulana, vitenge, pombe, chakula, sukari, majiko ya gesi na vingine,” alisema.
Pia, alitaja kuwa: “Kuna kudhamini michezo, kuchangia shughuli za kijamii ama kidini wakati wa kampeni, kujihusisha na harusi, misiba na matukio ya kijamii. Rushwa ya ngono, kutumia lugha ya vitisho, nguvu au mabavu ili kuwalazimisha wapiga kura au kuwazuia kupiga kura.”

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Chrispin Chalamila alitoa wito kwa waandishi wa habari kuwa kiungo muhimu ili kudhibiti na kufichua vitendo vya rushwa hususan ni wakati wa uchaguzi.
“Hatua madhubuti zimechukuliwa na baadhi ya kesi zimehamishwa kwenda mamlaka zingine, kuripotiwa ngazi za utawala na wahusika kuwajibishwa na kesi zingine zilikamilika ushahidi zimefikishwa mahakamani,” alisema Chalamila.
Mbali na hilo, ripoti hiyo ilibainisha kuwa maeneo yaliyoongoza kwa kulalamikiwa na vyama vya siasa katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024, ni pamoja na barua za utambulisho wa mawakala wa vyama vya siasa kuchelewa kuwafikia wasimamizi wasaidizi kwa baadhi ya vituo vya kupiga kura.

Pia, kuna wagombea na wapambe wao kubaki katika vituo huku wakipiga kampeni, waangalizi wa uchaguzi kulazimisha kuingia ndani ya vituo bila kuwa na utambulisho rasmi, orodha ya majina ya wapiga kura kutokuonekana vizuri na kutokupangwa katika mtiririko wa kialfabeti jambo ambalo lilisababisha usumbufu kwa wananchi kutafuta na kuhakiki majina yao katika vituo vya kupigia kura.
“Pia, ilibainika kuwa baadhi ya maeneo, upigaji wa kura ulifanyika chini ya miti na wengine kwenye vibaraza vya nyumba za watu binafsi kinyume na mwongozo,” ilisema ripoti hiyo.
Kauli ya wadau
Askofu wa Kanisa la Tabernacle Gospel Church (TGC), Robert Bundala ameitaka Serikali kupitia Takukuru kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya rushwa na kuhimiza mbinu za kuripoti matukio ya rushwa kwa kuzingatia usiri.
“Wengine wanaijua rushwa ila watu wakishuhudia wakaifanya kuwa siri hata Biblia inasema rushwa inapofusha macho, maana yake inamfanya mwenye haki aikose haki yake lakini kama jamii inafahamu madhara yake wakibaini uwepo wa rushwa watatoa taarifa,” amesema askofu.
Askofu Bundala ambaye pia ni Katibu Kamati ya Amani ya Mkoa wa Mwanza amesema vyombo vya kuzuia na kupambana na rushwa viweke mitego ya siri na mabalozi wa siri kuwanasa wanaotoa na kupokea rushwa ili kuwachukulia hatua za kisheria.
“Kuna sehemu zingine ikiwemo maeneo ya umma kama maduka, daladala, ofisini na hotelini hakuna matangazo ya kuhamasisha kukataa rushwa. Huko nyuma kuliwahi kuwa na namna fedha za Takukuru wakibaini kuna mgombea anayegawa rushwa basi wanapeleke watu wao na kuwashikisha hizo fedha kisha wanawachukulia hatua nadhani warejeshe huo utaratibu,” amesema Askofu Bundala.
Mkazi wa Mirongo Kata ya Mbugani jijini Mwanza, Hasnath Juma amesema mapambano ya rushwa ni mtambuka hivyo Takukuru haipaswi kuishia kutoa takwimu pekee kwenda mbali na kuongeza msukumo kwa jamii kuikataa.
“Kila mwaka tumekuwa tukiletewa taarifa ya hali ya rushwa nchini lakini uchaguzi ukikaribia matendo yaleyale yanajirudia. Nashauri tuone ukomeshwaji wa rushwa kwa vitendo zaidi kuliko hizi ripoti,” amesema Hasnath.
Kauli za wadau vyama siasa
Naibu Katibu Mkuu ACT-Wazalendo, Ester Thomas amesema miongoni mwa mambo yanayoikatisha tamaa jamii kushughulika na rushwa ni kuona inawaibua watoaji na wapokeaji wa rushwa kwa lengo la kuchukuliwa hatua, lakini hawaoni wakishughulikiwa ipasavyo.
“Katika kupambana na rushwa tunahitaji vitendo hasa katika kuhakikisha kwamba wale wote waliohusika kwenye vitendo vya rushwa wanawekwa wazi kwa wananchi kwa sababu wananchi wenyewe wanakuwa wanawasema wale watu ikionekana wamefikishwa kwenye vyombo vya sheria wao wenyewe watachukua hatua,” amesema Thomas.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Eveline Munisi ameiaka Takukuru kutoishia kutoa mafunzo kwa viongozi wa kisiasa na jamii badala yake iwe na meno inapobaini mtu yeyote ametoa ama kupokea rushwa.
“Takukuru wasiishie kutupatia mafunzo na kutoa warsha kwa viongozi wa vyama na taasisi mbalimbali lakini ikibainika hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa yeyote atakayefanya kitendo cha kutoa ama kupokea rushwa,” amesema Munisi.
Akizungumza jinsi ya kuondoka kutoaminika miongoni mwa vyama vya siasa nchini, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amemshauri Rais, Samia Suluhu Hassan (mgombea CCM) kuitisha kikao na wadau wa vyama vya upinzani ili kujenga mazingira ya kuaminiana kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
“Kuna mambo ya sheria ambayo bado hayajakaa vizuri na muda haupo, lakini ikiwa watendaji watakuwa na nia thabiti ya kuweza kutenda haki basi uchaguzi utakuwa bora zaidi kuliko wa 2024 na 2020.