Rupia kidogo tu asepe Singida Black Stars

MSHAMBULIAJI wa Singida Black Stars, Mkenya Elvis Rupia amesema ilibaki kidogo tu aondoke dirisha dogo la usajili la Januari baada ya kutoridhishwa na baadhi ya mambo japo kwa sasa kila kitu kipo freshi.

Nyota huyo anayeongoza wafungaji mabao katika Ligi Kuu Bara akiwa na manane, alisema kuna mambo ambayo hapendi kuyaweka wazi yalitaka kumfanya aondoke.

“Ni mambo ya kawaida tu ambayo yanaweza kumtokea mtu yeyote. Ni kweli nilitaka kuondoka ili nikatafute changamoto mpya, lakini nimebaki. Niwatoe hofu mashabiki wangu kwamba nimebaki na nitaendelea kuipambania timu ifikie malengo,” alisema.

Wakati nyota huyo akizungumza hayo, chanzo ndani ya kikosi hicho kililiambia Mwanaspoti sababu za kutaka kuondoka ni kutokana na kutaka kuongezewa mshahara baada ya mastaa wapya waliosajiliwa kudaiwa kulipwa vizuri zaidi.

“Aligundua mshambuliaji mwenzake Jonathan Sowah aliyesajiliwa hivi karibuni kutoka Al-Nasr Benghazi ya Libya analipwa vizuri zaidi yake, hakufurahishwa kwa kazi anayoifanya ila kila kitu kimeenda sawa,” kilisema chanzo.

Hata hivyo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, Hussein Massanza alikanusha akidai ni uongo, japo Mwanaspoti lilipenyezewa ukweli wa nyota huyo kutaka kuondoka kwa sababu ya maslahi. Rupia alijiunga na Singida 2023-2024 akitokea Police FC ya Kenya alikofunga mabao 27 na kuvunja rekodi ya miaka 47 Ligi Kuu Kenya ya Moris Aloo Sonyi aliyefunga 26 mwaka 1976, akiwa na Gor Mahia.