

Chanzo cha picha, Shutterstock
- Author, BBC Investigations & Panorama
- Nafasi, BBC
Mwezi Septemba 2019 kipindi cha BBC kiliripoti mkasa wa kushangaza wa Ruja Ignatova, mwanamke wa Bulgaria anayetafutwa na FBI baada ya kuwalaghai wawekezaji kati dola za kimarekani bilioni 4.5, kupitia sarafu yake ya mtandaoni, na kisha kutoweka.
Uchunguzi wa BBC umefuatilia uhusiano wake wa karibu na mshukiwa wa uhalifu huko Bulgaria na madai kwamba mwanamke huyo aliuawa kikatili.
Utapeli wa Ignatova

Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Oxford, Ruja Ignatova, alizaliwa nchini Bulgaria na kukulia Ujerumani, alisoma masuala ya fedha kabla ya kuzindua sarafu ya mtandaoni ya OneCoin mwaka 2014.
Aliwashawishi mamilioni ya watu ulimwenguni kote kuwekeza kwenye OneCoin, akiahidi faida kubwa itapatikana kwa wawekezaji kama ile iliyokuwa ikipatikana mwanzoni mwa Bitcoin.
Ignatova – anayejulikana na wengi kama Dkt Ruja – alikuwa anafanya ulaghai aliouficha kwa uwerevu, bila rekodi za mtandaoni ambazo ndio msingi wa sarafu halali ya mtandaoni kama Bitcoin.
Wachunguzi kutoka Ujerumani na Marekani walipomchunguza Ignatova, Oktoba 2017, alisafari mapema asubuhi kwa ndege ya Ryanair kutoka Sofia, Bulgaria hadi Athens, Ugiriki na hakuonekana tena.
Kuanzia mwaka jana, uchunguzi wa BBC na Panorama umekuwa ukichunguza kuhusu kilichompata, na ikiwa yuko hai. Jambo muhimu ni kujua ni nani aliye karibu naye.
Amekufa au Yu hai?

Chanzo cha picha, Interpol
Mkurugenzi Mtendaji wa sarafu ya OneCoin, Ruja Ignatova, ndiye mwanamke anayesakwa zaidi na FBI. Aliiba mabilioni, kisha akatoweka.
BBC inaelewa kuhusu mwanaume ambaye alikuwa akimlinda Ignatova – Hristoforos Nikos Amanatidis, anayejulikana kama Taki.
“Tuliambiwa, anayedaiwa kuwa mfanyabiashara mkubwa wa dawa za kulevya ndiye aliyekuwa akisimamia usalama wake,” anasema Richard Reinhardt, ambaye alifanya uchunguzi kwa ajili ya Huduma ya Mapato ya Ndani ya Marekani kwa kushirikiana na FBI. Aliyasema hayo katika mahojiano yake ya kwanza tangu kustaafu mwishoni mwa 2023.
“Tuna ushahidi mfanyabiashara huyo, kama sio mfanyabiashara mkubwa zaidi wa dawa za kulevya nchini Bulgaria, alikuwa na uhusiano wa karibu na OneCoin – aliwahi kuwa mlinzi binafsi wa Ruja Ignatova,” anasema Reinhardt.
Kulingana na Reinhardt, Ignatova alikuwa mhalifu mkubwa kuliko watu wengi wanavyofikiria.
Nadharia hii inaonekana kuungwa mkono na nyaraka za Europol zilizovuja, zilizoonekana na BBC, ambazo zinaonyesha – kabla ya Ignatova kutoweka mwaka 2017 – polisi wa Bulgaria walijua uhusiano wake na Taki.
Katika hati hizo, polisi wanashuku Taki alitumia mtandao wa OneCoin kutakatisha fedha za ulanguzi wa dawa za kulevya.
Huko Bulgaria, Taki ni kama El Chapo au Pablo Escobar. Yeye na washirika wake wamechunguzwa kwa wizi wa kutumia silaha, ulanguzi wa dawa za kulevya na mauaji, lakini hajawahi kufunguliwa mashtaka.
Ivan Hristanov, ambaye mwaka 2022 alichunguza madai kwamba Taki aliendesha mtandao wa uhalifu kwa usaidizi wa maafisa wafisadi, anasema:
“Taki ni mzimu. Huwezi kumwona. Utasikia tu habari zake. Anazungumza nawe kupitia watu wengine. Usiposikiliza, utatoweka tu duniani.”
“Mtu pekee anayeweza kumlinda [Ignatova] kutokana na uchunguzi, ikiwa ni pamoja na uchunguzi wa kutoka mashirika ya kigeni ni Taki.”
BBC iliiandikia serikali ya Bulgaria kuhusu madai ya maafisa wafisadi. Lakini haikujibu. Ofisi ya mwendesha mashtaka katika mji mkuu Sofia inasema “haifichi uhalifu na watu ambao wametenda uhalifu.”
Taki sasa anaaminika kuishi Dubai, ambako Ignatova alinunua nyumba ya kifahari na huko ndiko akaunti zake za benki zilipokea mamilioni ya dola kutokana kwenye ulaghai wa OneCoin.
Ingawa haijulikani jinsi Taki na Ignatova walivyokutana, au kama Taki alihusika na OneCoin tangu mwanzo, vyanzo vingi vinasema walikuwa na uhusiano wa karibu na alikuwa mshauri wa binti wa Ignatova.
Chanzo kimoja cha habari cha Bulgaria kilicho karibu na Ignatova kiliiambia BBC huenda alimlipa Taki Euro 100,000 kwa mwezi kwa ajili ya ulinzi.
Inaonekana kuna uhusiano mwingine wa kifedha kati ya Ignatova na Taki.
Nyaraka za Europol zinataja mpango tata wa kuuza kiwanja, katika ufuo wa Bahari Nyeusi nchini Bulgaria, unaohusisha kampuni moja ya Ignatova na mke wa Taki.
Nyaraka hizo za siri za polisi zilipatikana na BBC kupitia Frank Schneider, jasusi wa zamani na mshauri wa Ignatova, ambaye nae baadaye alitoweka.
Alituambia bosi wake wa zamani alikuwa akifanya kazi na mafisadi na majambazi.
Tulipomhoji Schneider nyumbani kwake Ufaransa, alikuwa chini ya kizuizi cha nyumbani, akisubiri kurejeshwa Marekani kuhusiana na kashfa ya OneCoin. Hata hivyo, hakuwa tayari kufichua jina la bosi huyo.
“Sitakuambia ni nani, kwa sababu nina familia. Huu ni uhalifu mkubwa wa kupangwa.”
Ignatova ameuwawa na Taki?

Mwaka 2022, mwanahabari mpelelezi wa kutoka Bulgaria, Dimitar Stoyanov na wenzake katika kituo cha habari cha uchunguzi bird.bg, walikabidhiwa ripoti ya polisi ambayo ilipatikana nyumbani kwa afisa wa polisi wa aliyeuawa Bulgaria .
Katika waraka huo, mpasha habari wa polisi alimsikia shemeji yake Taki ambaye alikuwa amelewa akisema, Ignatova aliuawa kwa amri ya Taki mwishoni mwa 2018, na mwili wake kukatwakatwa na kutupwa kwenye Bahari ya Ionian.
Stoyanov anasema jambo hili linawezekana.
“Ukweli wa hati hiyo ya polisi ulithibitishwa na maafisa wa Bulgaria, na washirika wengi wa uhalifu wa Taki wanaamini ni kweli alimuua,” anasema Stoyanov.
Hata hivyo, BBC imeshindwa kuthibitisha dai hili.
Sababu ni kwamba Ignatova alikuwa mzigo kwa Taki, ambaye alitaka kufuta uhusiano wake na ulaghai wa OneCoin.
Washirika hao wa Taki wanaoamini hivyo ni pamoja na Krasimir Kamenov, anayejulikana kama Kuro, anayesakwa na Interpol kwa tuhuma za mauaji.
Stoyanov anasema Kuro alimwambia, alimsikia Taki akizungumzia biashara yake ya uhalifu mbele ya Ignatova, na baadae Kuro alipomuuliza Taki ikiwa ni salama kufanya hivyo, Taki alimjibu: “Usijali, hatoishi muda mrefu.”
Kuro pia alidai alizungumza na CIA kuhusu Taki, juu ya madai kwamba Taki aliamuru kuuawa Ignatova. Vyanzo vilivyo karibu na Kuro viliithibitishia BBC mkutano huo na CIA ulifanyika mwishoni mwa 2022.
Mwezi Mei 2023, Kuro aliuawa nyumbani kwake Cape Town, Afrika Kusini pamoja na mke wake na watu wengine wawili ambao walikuwa wafanya kazi wake.
Polisi wa Afrika Kusini bado wanawasaka wauaji, lakini naibu waziri wa zamani wa Bulgaria Hristanov anaamini mauaji ya Kuro yanahusishwa na Taki.
“Ilibidi watu fulani wauwawe kwa sababu walijua mengi kuhusu Taki. Yalikuwa ni kama mauaji ya hadharani ili kutoa ujumbe kwa wengine,” alituambia.
Tangu kuchapishwa madai ya mauaji ya Ignatova, mwanahabari Dimitar Stoyanov anasema yeye na wenzake wamekumbana na vitisho vya kuuawa, na hivyo kumlazimu kuondoka kwa muda Bulgaria kwa mara ya nne tangu kuwa mwanahabari.
Taki hajawahi kukamatwa kwa mauaji ya Ignatova. Mwili wake haujawahi kupatikana na wachunguzi wanasema hawana ushahidi wa kutosha wa kumshtaki.

Richard Reinhardt anaamini huenda Ignatova ameshakufa. Ingawa hajaona ushahidi wowote unaohusisha kifo chake. Anasema ni kutokana na namna magenge ya madawa ya kulevya yanavyofanya kazi.
“Ikiwa [Taki] angefikiri Ignatova ni tishio kwake, ni rahisi kumwondoa badala ya kukamatwa.”
BBC iliwaandikia mawakili wa Taki kuhusu madai haya – lakini hawakujibu.
Mwaka 2022, Ignatova aliwekwa kwenye orodha ya Watu Kumi Wanaosakwa Zaidi ya FBI – na bado yupo hadi leo.
Inaweza kuwa uvumi wa kifo chake ni ujanja wa kuwapotezea watu mwelekeo.
Lakini Reinhardt pia anaamini, FBI haiweki watu tu katika orodha kwa kujifurahisha. Wangemwondoa ikiwa kungekuwa na uthibitisho amekufa.
Kwa maana hiyo, kwa sasa malkia wa sarafu ya mtandaoni bado anasakwa.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi