
SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT) imeweka wazi itashirikiana na mwanariadha Gabriel Geay kuhakikisha mashindano ya mbio za nyika aliyoyaanda nyota huyo yanafanyika kwa ubora mkubwa.
Geay mwenye rekodi ya Marathoni ya taifa kwa muda wa 2:03:00 aliyoiweka mwaka 2022 kupitia mbio za Valencia Marathon zilizofanyika Hispania ameandaa mbio za Nyika za Km 2, Km 4, Km 6 na Km 10 zitakazofanyika Februari 8 mwaka huu wilayani Babati mkoani Manyara.
Mbio hizo ambazo zinajulikana kama Madunga Cross Country zinatazamiwa kushirikisha zaidi ya wakimbiaji 300 kutoka ndani na nje nchi wakiwemo wanariadha wa kimataifa wa Kenya.
Katibu wa RT, Jackson Ndaweka ameiambia Mwanaspoti katika kuhakikisha mbio hizo zinafanyika kwa ubora mkubwa na kuibua vipaji vingi vya vijana wataongeza nguvu hili kufanikisha hilo.
“Kwanza nimpongeze Geay kwa hatua hii licha ya kuwa ni staa lakini haya mafanikio ambayo amevuna ameona si vibaya pia kuwa daraja la vijana kutimiza ndoto zao,” alisema Ndaweka.
Aliongeza kama shirikisho kwao ni furaha kuona nyota wakubwa ambao wamefankiwa kupitia mchezo huo kama Geay na Alphonce Simbu ambaye amekuwa akiandaa mbio za Mampando Festival zinazofanyika kila mwaka mkoani Singida wanapambana kuibua vipaji.
“RT tutatoa ushirikiano mkubwa wa kutosha kwanza kuhakikisha mashindano yanafanyika kwa ubora lakini pia kuangalia vijana wenye vipaji,” alisema Ndaweka, huku Geay aliyeandaa mbio hizo akishirikiana na taasisi ya Posso Sports anayoisimamia alisema mashindano hayo yanalenga katika kukuza na kuibua vipaji mbalimbali za vijana hususani katika maeneo ya vijijini.
Aliweka wazi anaamini mbio hizo zitakuwa ni fursa kwa vijana kuonyesha vipaji vyao na kupata nafasi ya kupata wafadhili ambao watawashika mkono ambayo itawafanya kutimiza ndoto zao kupitia mchezo wa riadha.
“Madunga ni sehemu ambayo nimezaliwa hivyo nimeona kwa kuanza mbio hizi nianze nao hili kuweza kuwahamasisha vijana kushiriki katika mchezo wa riadha ila mbio hizi zitakuwa zinazunguka,” alisema Geay aliyeweka bayana ishu za zawadi akisema zitakuwa za fedha kwa washindi ambapo pia kutakuwa na zawadi za viatu ambayo itatolewa na kampuni vifaa vya michezo ya Asics kutoka Japan.
Katika hatua nyingine mwanariadha huyo ameiomba serikali kuhakikisha inaunga mkono juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali katika kuibua vipaji vinavyoweza kuleta heshima kwa Taifa.