Khartoum. Kundi la wanamgambo wa Jeshi la Msaada wa Haraka (RSF) limeongeza mashambulizi katika Kambi ya Wakimbizi ya Zamzam karibu na El-Fasher, Mji Mkuu wa Darfur Kaskazini, ambayo inakabiliwa na njaa.
Hatua hiyo inadaiwa kuwa sehemu ya juhudi za kundi hilo kuimarisha udhibiti wake eneo la Darfur, ambalo kihistoria limekuwa ngome yake ya kijadi.
Mapigano kati ya RSF na Jeshi la Sudan (SAF) yalianza Aprili 15, 2023, baada ya RSF kuhamasisha majeshi yake katika miji mbalimbali nchini Sudan, ikiwa ni pamoja na Darfur.
Jeshi la Ulinzi la Sudan (SAF) linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan limetangaza RSF linaloongozwa na Muhammed Hamdan Dagalo maarufu Hemedti kuwa ni kundi la waasi.
RSF inahusisha vikundi vya wapiganaji wakiwamo wa muungano wa Janjaweed.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Aljazeera, wakazi na wahudumu wa afya waliripoti kuwa RSF ilishambulia kambi hiyo ambayo imezingirwa mara tatu ndani ya kipindi cha wiki moja.
Mashambulizi haya yanazidisha hali mbaya kwa maelfu ya wakimbizi walioko kambini, huku kukiwa na uhaba mkubwa wa chakula, maji na huduma za afya.
Kwa mujibu wa Shirika la Doctors Without Borders (MSF), takriban watu saba wameuawa wiki hii katika Kambi ya Wakimbizi ya Zamzam.

Shirika hilo pia liliripoti kuwa wahudumu wa afya wamelemewa na hawawezi kufanya upasuaji katika kambi hiyo kutokana na hali mbaya ya usalama.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ((UN), Stephane Dujarric, amesema mapigano hayo mapya yanahusisha matumizi ya silaha nzito na akatoa wito kwa pande zote zinazopigana kusitisha ghasia mara moja.
Jeshi la Msaada wa Haraka (RSF) linadaiwa kujaribu kuimarisha udhibiti wake katika ngome yake ya jadi ya Darfur, wakati likipoteza maeneo kwa Jeshi la Sudan (SAF) katika Mji Mkuu wa Khartoum.
Takriban miezi 22 tangu vita kati ya Jeshi la Msaada wa Haraka (RSF) na Jeshi la Sudan (SAF) vilipoanza, wanamgambo wa RSF bado wanadhibiti sehemu kubwa ya Darfur, magharibi mwa Sudan, pamoja na maeneo mengi ya jimbo jirani la Kordofan.
Wakazi wa maeneo hayo wanasema RSF inatekeleza vitendo vya kikatili dhidi ya raia, ikiwamo uporaji na mauaji, hali inayoongeza hofu na mateso kwa jamii zilizoathirika.
Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu wameendelea kutoa wito wa kusitishwa kwa ghasia na kuruhusiwa kwa misaada ya kibinadamu katika maeneo yaliyoathirika na mgogoro huu.
Jeshi la Sudan lateka maeneo muhimu
Kwa upande mwingine Jeshi la Sudan (SAF) kwa sasa linadhibiti sehemu za Kaskazini na Mashariki mwa nchi na limepata mafanikio muhimu hivi karibuni katika Mji Mkuu wa Khartoum.
Kambi ya Wakimbizi ya Zamzam, inayohifadhi takriban watu 500,000 waliokimbia vita vya sasa na vile vya awali Darfur, inazidi kukumbwa na mashambulizi ya RSF.
Wakati huohuo, El-Fasher, mji ulio karibu, una wakazi wapatao milioni 1.8 na kwa sasa ndiyo ngome kuu ya mwisho inayopinga udhibiti wa RSF Darfur nzima.
Kwa miezi kadhaa, RSF imeizingira eneo hilo, ikidai kuwa Kambi ya Zamzam inatumika kama kituo cha wanajeshi wa Joint Forces, makundi ya waasi wa zamani ambayo sasa yanapigana bega kwa bega na Jeshi la Sudan (SAF).
Baadhi ya wakazi wa Kambi ya Wakimbizi ya Zamzam wamechimba mashimo ardhini ili kujificha na kujilinda dhidi ya mashambulizi yanayoendelea, kwa mujibu wa mmoja wa wakazi na video iliyoshirikiwa na wanaharakati.
“Ndani ya makazi, wanatia hofu, wanaiba na kuua, watu hujificha kwenye mashimo haya wanaposhambuliwa kwa risasi au wanapovamiwa, kwa sababu hakuna sehemu nyingine ya kukimbilia,” mkazi mmoja wa kambi hiyo aliambia Shirika la Habari la Reuters.

Mkuu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Clementine Nkweta-Salami, alieleza kushtushwa na mashambulizi dhidi ya kambi hiyo na kuzuiwa njia za wakimbizi kutoroka.
Alitoa wito wa kusitishwa kwa ghasia na kuruhusiwa kwa misaada ya kibinadamu kwa waathiriwa wa mzozo huu.
Wakati huohuo, RSF imeweka vikwazo dhidi ya juhudi za misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa kambi ya Zamzam, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada.
Agosti, ripoti iliyoungwa mkono na UN ilibaini kuwa kuna uwezekano mkubwa sehemu za Darfur Kaskazini, hasa Kambi ya Zamzam inakabiliwa na kiwango cha juu cha njaa, kinachojulikana kama IPC Phase 5.
IPC Phase 5 ni hatua ya juu kabisa katika Mfumo wa Kimataifa wa Uainishaji wa Usalama wa Chakula, inayoashiria hali; angalau mtu mmoja kati ya watano anakosa chakula cha kutosha, anakabiliwa na njaa kali, umaskini wa kupindukia na hatari kubwa ya utapiamlo mkali na kifo.