
Jeshi la Polisi Tanzania limethibitisha kumshikilia Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe kwa tuhuma za kuwachafua viongozi wa serikali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amethibitisha Kamwe anashikiliwa kuanzia jana usiku, kwa tuhuma hizo.
Abwao amesema bado Kamwe yuko kizuizini akiendelea na mahojiano juu ya tuhuma hizo na taarifa zaidi zitatolewa baadaye.
“Kweli tunamshikilia msemaji wa Yanga Ally Kamwe kwa tuhuma za kuwachafua viongozi wa serikali,” amesema Abwao.
“Tulimkamata jana saa saba usiku. Kwa sasa tunaendelea na mahojiano naye, tutakapokamilisha tutatoa taarifa zaidi.
Kamwe anashikiliwa kwa madai ya kumchafua Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha kwenye moja ya mikutano yake na mashabiki wa Yanga kabla ya mchezo wa jana kati ya Tabora United dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara.
Mapema jana kabla ya mchezo huo, Chacha alionekana akisalimiana na vizuri na Kamwe kwenye Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi, kabla ya baadaye mambo kubadilika.