
Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limewataka vijana kutumia michezo kama sehemu ya kuhamasisha amani na utulivu katika kuelekea uchaguzi Mkuu Oktoba 2025, huku likionya wavunjifu wa amani.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Benjamin Kuzaga amesema leo Jumamosi Mei 3, 2025, katika viwanja vya Kumbukumbu ya Sokoine baada ya kushiriki mbio za pole ikiwa ni kuelekea mashindano ya mbio “Betika Tulia Marathon 2025”, zinazotarajiwa kufanyika Mei 9 mpaka 10 mwaka huu.
Amesema katika kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 2025, Serikali inahimiza wananchi kushiriki kikamilifu na kuachana na vitendo vya uvunjifu wa amani ambavyo havita vumilika.
“Tunaelekea uchaguzi mkuu jamii inapaswa kushirikiana kikamilifu na Serikali kutumia kama sehemu ya kulinda amani na sio vurugu ambazo hazitavumilika,”amesema Kuzaga.
Katika hatua nyingine, amewataka vijana kuchangamkia fursa ya kushiriki mashindano ya mbio za “Betika Tulia Marathon 2025” kwa lengo la kujenga umoja na mshikamano na kuibua vipaji kutoka Mkoa wa Mbeya.
“Itakuwa aibu sana kwa wananchi wa Mbeya kushindwa kushiriki, badala yake watu kutoka mataifa mengine kuibuka washindi kwa kujinyakulia zawadi,”amesema.
Mratibu wa mashindano hayo, Joyce Mwakifwamba amesema huu ni msimu wa tisa ambao umekuja kitofauti kwa kuongeza mbio za kilometa mbili mpaka tano ambazo zitahusisha watoto, huku watu wazima watakimbia kuanzia mita 100 mpaka kilometa 42 .
“Lengo la kushirikisha watoto katika msimu huu ni kuibua vipaji na kuviendeleza kama njia pekee ya kujiajiri,”amesema.
Meneja wa Taasisi ya Tulia Trust ambao ni waandaji wa mashindano ya mbio hizo, Jackline Boaz amesema leo Jumamosi Mei 3, 2025 wameanza na mbio za awali kwa kushirikisha wadau mbalimbali vikiwepo vyombo vya ulinzi na usalama ambao wamekimbia umbali wa kilometa 10.
“Huu ni mwanzo wa kuelekea mashindano ya mbio hizo ambazo zitashirikisha mataifa mbalimbali ya nje ya Tanzania ikiwepo nchi jirani ya Kenya,” amesema.
Boaz amehamasisha wananchi na wanariadha kujisajili wakiwepo wakazi wa Mbeya kwa kuzingatia riadha ni sehemu ya ajira na kujiajiri.
Ofisa Uhusiano wa Taasisi ya Tulia Trust, Joshua Mwakanolo amesema fedha za ushiriki kwenye mashindano hayo uelekezwa kuchangia miradi ya elimu, afya na kuwezesha kaya zisizo jiweza kiuchumi.