RPC KATABAZI : MASHINDANO YA POLISI JAMII CUP YAMEPUNGUZA UHALIFU KWA KIASI KIKUBWA JIJI LA DODOMA

RPC KATABAZI : MASHINDANO YA POLISI JAMII CUP YAMEPUNGUZA UHALIFU KWA KIASI KIKUBWA JIJI LA DODOMA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma SACP George Katabazi amesema uwanzishwaji wa michezo mbalimbali katika Jiji la Dodoma umesaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia na kupungua kwa vitendo vya uhalifu katika jiji hilo.

Kamanda Katabazi ameyasema hayo Mei 19.2025 katika uwanja wa mtekelezo jijini Dodoma ulipochezwa mchezo wa fainali wa mashindano ya polisi jamii cup 2025 dhidi ya timu ya vijana wa Chang’ombe na timu ya vijana wa Mpunguzi ambapo timu ya vijana wa Chang’ombe imeibuka mshindi wa fainali hiyo kwa ushindi wa goli 2-0.

Kamanda katabazi amesema mashindano hayo yaliyojumuisha timu za kata 14 yanalenga kuimarisha ushirikiano wa jeshi la polisi na jamii hususani kundi la vijana katika kuwahamashisha kutojihusisha na vitendo vya uhalifu.

“Kwa kiwango kikubwa michezo imesaidia kupunguza uhalifu katika mkoa wa Dodoma hii ni pamoja na program tuliyo ianzisha kwa vijana wa Dodoma katika kuzuia,kubaini na kutanzua uhalifu,tulianza hii michezo na polisi jamii cup 2024 kwa mkoa mzima ila mwaka huu tumekuja na polisi jamii umoja cup 2025 ambapo imefanyika ndani ya jiji la Dodoma.

“Kwa kiasi kikubwa vijana wametoa taarifa za uhalifu na wahalifu na sisi jeshi la polisi mkoa wa Dodoma tumejitahidi kujikita katika ushirikishwaji wa jamii bila kulisahau kundi la vijana,”amesema SACP Katabazi.

Aidha Kamanda katabazi amesema michezo hiyo imeenda sambamba na kaulimbiu isemayo “Uchaguzi salama kwa maendeleo yetu”inayo lenga kuwahamasisha vijana kujitokeza na kushiriki zoezi la uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Awali mkuu wa mkoa wa Dodoma wa Dodoma Mhe.Rosemary Staki Senyamule amelipongeza jeshi la polisi Dodoma kwa kuanzisha mashindano hayo yaliyowaleta vijana kwa pamoja na kuwahamasisha kutojiingiza katika vitendo vya uhalifu.

Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa Mhe.Senyamule amewahimiza vijana hao kuhakikisha wanashiriki katika zoezi la kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la mpiga kura linaloendelea katika mkoa wa Dodoma na kutarajiwa kukamilika Mei 22 mwaka huu.

“Kupitia michezo hii vijana wameimarisha Afya zao pia wamejiepusha na uhalifu mtaani maana muda ambao wangeutumia kufanya uhalifu ndiyo wanautumia kucheza michezo hii hivyo nilipongeze sana jeshi la polisi kwa kuanzisha michezo hii,”amesema.

Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa michezo hiyo kwa nyakati tofauti wameliomba jeshi la polisi Dodoma kuendelea kuweka mashindano ya michezo mbalimbali ili kuwafanya vijana hao kuwa bize na michezo na kuondokana na hali ya kukaa pasipo kuwa na kazi yeyote jambo ambalo hupelekea wengi wao kujihusisha katika uhalifu.

The post RPC KATABAZI : MASHINDANO YA POLISI JAMII CUP YAMEPUNGUZA UHALIFU KWA KIASI KIKUBWA JIJI LA DODOMA appeared first on Mzalendo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *