Rosicky ajipigia debe ubosi Arsenal

Prague, Czech. Nyota wa zamani wa Arsenał, Thomas Rosicky amesema haitokuwa jambo la kushangaza yeye kurudi klabuni hapo kama mkurugenzi wa michezo kwa vile yeye ni familia.

Kauli hiyo ya Rosicky imekuja katika muda ambao Arsenal inasaka mrithi wa Edu ambaye Novemba mwaka jana aliamua ghafla kuachana na klabu hiyo baada ya kupata ofa nono kwingine.

Kwa sasa nafasi hiyo ya mkurugenzi wa michezo inakaimiwa na Jason Ayto ambaye alikuwa msaidizi wakati wa Edu huku mchakato wa kumsaka mrithi wa Edu.

Miongoni mwa majina ambayo yamekuwa yakipigiwa upatu ni Rosicky ambaye kwa sasa ni mkurugenzi wa michezo wa Sparta Plague na mwenyewe amesema kuwa hashangai Hilo kutokea kwa vile Arsenal ni nyumbani.

“Uhalisia ni rahisi tu. Muunganiko wangu na Arsenal ni asilia kwa sababu nimetumia miaka 10 pale. Na unapotumia miaka 10 mahali fulani, unatengeneza muunganiko wenye nguvu na imara zaidi.

“Hivyo nina muunganiko imara na Arsenal na nina muunganiko imara na Sparta Prague. Zote ni klabu mbili ambazo nazipenda kimpira kwa sababu nina uhusiano mzuri nazo,” alisema Rosicky.

Rosicky amesema kuwa hakuna mawasiliano yoyote ambayo yamefanyika baina yake na Arsenal juu ya kuchukua nafasi ya Edu.

“Nimeheshimishwa kwa ukweli kwamba nawekwa kipaumbele na uongozi wa Arsenal lakini naweza kusema kwamba sina ofa yoyote ya kwenda Arsenal.

“Kama nilivyosema hapo mwanzo kuwa nafahamu kwamba nipo katika rada zao au mtu aliye katika vipaumbele vyao kwa uwezo fulani lakini sijapokea ofa yoyote,” alisema Rosicky.

Kama Rosicky atapata fursa hiyo, kibarua chake kikubwa kitakuwa ni zoezi la usajili katika dirisha kubwa la usajili la majira ya kiangazi baada ya klabu hiyo kushindwa kufanya usajili katika dirisha dogo la usajili la majira ya baridi.

Arsenal haikusajili mchezaji yeyote licha ya kuwepo kwa kilio kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo wakitaka isajili baada ya nyota wake wa nafasi ya ushambuliaji, Gabriel Jesus, Gabriel Martinelli, Kai Havertz na Bukayo Saka kuumia.