Ronaldo aiongoza Ureno kutwaa taji la pili la Nations League

Katika mchezo huo wa fainali uliopigwa Jumapili, Ureno ililazimika kurejea mchezoni mara mbili baada ya Hispania kutangulia kufunga. Martin Zubimendi aliipatia Hispania bao la kwanza dakika ya 21, kufuatia mkanganyiko langoni mwa Ureno.

Hata hivyo, Ureno ilisawazisha haraka kupitia kombora la Nuno Mendes dakika ya 26, akiweka mpira kona ya mbali na kumpita kipa wa Hispania.

Hispania ilirejea mbele dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza, ambapo Mikel Oyarzabal alifunga kwa shuti lililotikisa nyavu kwa ustadi mkubwa.

Lakini, Cristiano Ronaldo alihakikisha Ureno hairudi nyuma kwa muda mrefu. Alifunga bao la pili kwa Ureno kwa mkwaju wa karibu dakika chache baada ya saa kamili ya mchezo, na kufanya matokeo kuwa 2-2.

UEFA Nations League 2024/25 | Fainali | Portugal vs. Spanien
Licha ya Uhispania kutangulia kufunga mabao, haikufanikiwa kutwaa taji lake la tatu mfululizo.Picha: /Florian Wiegand/Eibner-Pressefoto/picture alliance

Katika dakika ya 88, Ronaldo mwenye umri wa miaka 40 alitolewa nje na kocha wake, akiwapisha wachezaji wapya katika dakika muhimu za mwisho.

Muda wa nyongeza haukuzaa mabao, na hivyo mshindi akaamuliwa kwa mikwaju ya penalti. Kipa wa Ureno, Diogo Costa, aling’ara kwa kuokoa penalti ya Alvaro Morata wa Hispania.

Hatimaye, Ruben Neves alifunga penalti ya tano ya Ureno, na kuipatia nchi hiyo ushindi wa 5-3 kwenye mikwaju ya penalti — ushindi uliowafanya kunyakua taji la Nations League kwa mara ya pili, baada ya lile la mwaka 2019. Kwa Ronaldo, ni taji lake la tatu la kimataifa akijumuisha pia Euro 2016.

Kwa upande mwingine, Ufaransa ilijipatia nafasi ya tatu kwa kuifunga Ujerumani mabao 2-0 mjini Stuttgart, huku Kylian Mbappé akiongoza mashambulizi yaliyowapa ushindi huo.

Kwa Hispania, kipigo hiki kinakatisha ndoto yao ya kushinda taji la tatu mfululizo, baada ya mafanikio kwenye Nations League ya 2023 na Euro 2024.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *