Ronaldinho, Romario kukipiga dhidi ya Zanzibar Juni

Dar es Salaam. Zanzibar inajiandaa kwa tukio la kihistoria la soka baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kushirikiana na Ubalozi wa Heshima wa Brazil kupanga mechi ya kirafiki kati ya magwiji wa soka wa Zanzibar na wa Brazil itakayopigwa Juni, mwaka huu. 

Mechi hiyo itawaleta mastaa wa zamani wa Brazil, akiwemo gwiji Ronaldinho Gaucho na mshambuliaji matata Romario de Souza, ambao watachuana na wakongwe wa Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo Ijumaa Machi 21, 2025 haikuweka wazi uwanja utakaochezwa mechi hiyo.

“Mechi hii ya kihistoria ya kirafiki kati ya magwiji wa Zanzibar na wa Brazil imepangwa kufanyika Juni 2025 hapa Zanzibar. Mechi hiyo itawakutanisha nyota wa zamani wa soka wa Brazil, akiwemo Ronaldinho Gaúcho na Romário de Souza.” Imeeleza taarifa hiyo.

Gaúcho ni mmoja wa wanasoka wabunifu na wenye vipaji vikubwa waliowahi kutokea duniani, akifahamika kwa mbwembwe zake uwanjani, chenga za maudhi, pasi za ufundi, na uwezo mkubwa wa kufunga mabao.

Staa huyo ametumikia klabu kubwa barani Ulaya kama vile AC Milan, PSG, Barcelona alikoshinda tuzo ya Ballon d’Or (Mchezaji Bora wa Dunia) 2005 kisha kurejea kwao Brazil kabla ya kustaafu rasmi 2018.

Baada ya kustaafu, amekuwa balozi wa soka duniani na anaendelea kushiriki katika mechi za wakongwe, akiwemo mchezo dhidi ya Zanzibar Legends unaotarajiwa Juni 2025.

Naye, Romário anatajwa kuwa mmoja wa washambuliaji bora wa wakati wote katika historia ya soka. Alijulikana kwa uwezo wake wa kufunga mabao kwa ufundi wa hali ya juu.

Staa huyo ametumikia klabu kama PSV Eindhoven, Barcelona, Flamengo, Valencia, Fluminense, na Vasco da Gama.

Gwiji huyo alitangaza kustaafu mwaka 2008 lakini alicheza mechi chache za mwisho kwa Vasco da Gama na America-RJ kabla ya kuachana rasmi na soka mwaka 2009.

Hata hivyo kwa mujibu wa mazungumzo yaliyofanyika Machi 18, 2025, mechi hiyo inalenga kukuza utalii, biashara, na kuiweka Zanzibar kwenye ramani ya kimataifa kupitia diplomasia ya michezo.

Aidha, itatoa fursa kwa wanasoka chipukizi wa Zanzibar na Tanzania kujifunza kutoka kwa mastaa wa dunia na kuimarisha mahusiano kati ya vilabu vya soka vya Zanzibar na Brazil. 

Mkutano wa maandalizi uliofanyika Zanzibar ulihudhuriwa na wawakilishi wa Wizara ya Afya, Habari, Utamaduni na Michezo; Wizara ya Utalii; Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango; Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA); taasisi za michezo; Jeshi la Polisi; Idara ya Uhamiaji; Idara ya Zimamoto na Uokoaji; pamoja na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *