
Paris, Ufaransa: Baada ya unyonge wa miaka 16, Ligi Kuu ya England (EPL) juzi imeheshimishwa baada ya nyota wa Manchester City, Rodri kuibuka mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or katika hafla ya utoaji wa tuzo hiyo iliyofanyika Paris, Ufaransa.
Tangu Cristiano Ronaldo alipochukua tuzo hiyo mwaka 2008 alipokuwa akiitumikia Manchester United, hakuna mchezaji mwingine anayechezea timu inayoshiriki EPL ambaye aliwahi kutwaa tuzo hiyo hadi juzi Rodri alipofanya hivyo.
Kuanzia 2009 hadi 2023, wachezaji wanaozitumikia timu tofauti zinazoshiriki Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’ walitwaa tuzo hiyo mara 12 tofauti huku wachezaji wa ligi nyingine wakifanya hivyo mara mbili tu.
Mchezaji huyo pia amekuwa raia wa kwanza wa Hispania kutwaa tuzo hiyo baada ya miaka 64 kupita tangu Luis Suarez alipofanya hivyo mwaka 1960.
Rodri aliibuka mshindi wa tuzo hiyo baada ya kuwashinda Vinicius Junior aliyeshika nafasi ya pili na Jude Bellingham aliyemaliza akiwa nafasi ya tatu, wote hao wakiitumikia Real Madrid.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28 ambaye alipoteza mechi moja tu msimu uliopita katika mechi zote alizocheza kwenye klabu na timu ya taifa, ameonekana kubebwa zaidi na mafanikio ya kuiongoza Hispania kutwaa ubingwa wa Kombe la Euro 2024 ambapo alikuwa mchezaji bora wa mashindano lakini pia aliiwezesha Manchester City kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England.
Nyota huyo wa Man City ambaye kwa sasa anauguza majeraha ya goti, alisema kuwa ushindi wake huo una maana kubwa kwa taifa lake na wachezaji wanaocheza katika nafasi yake.
“Ni siku ya kipekee kwangu, familia na nchi yangu. Leo sio ushindi wangu. Ni kwa ajili ya soka la Hispania, kwa wachezaji wengi ambao hawajashinda na walistahili kama [Andres] Iniesta, Xavi [Hernandez], Iker [Casillas], Sergio Busquets,na wengine wengi. Ni kwaq ajili ya soka la Hispania na kwa nafasi ya kiungo,” alisema Rodri baada ya kutunukiwa tuzo hiyo.
Ilikuwa ni hafla iliyoenda sambamba na mshangao uliosababishwa na uamuzi wa Real Madrid kuisusia saa chache kabla ya kufanyika kwake baada ya kile kinachoripotiwa kuwa walivujishiwa taarifa kuwa mshambuliaji wake Vinicius Junior hatoibuka mshindi wa tuzo hiyo ambayo imenyakuliwa na Rodri.
Baadaye klabu hiyo ilitoa taarifa kuwa iliamua kutoshiriki kwa vile waandaji wa tuzo hiyo hawakuiheshimu Real Madrid.
“Kama vigezo vya tuzo havijampa Vinicius kama mshindi, vigezo hivyohivyo vinatakiwa kumuonyesha Carvajal (Dan) kuwa mshindi. Kwa vile hii haikuwa kesi, ni wazi kwamba Ballon d’Or haiiheshimu Real Madrid. Na Real Madrid haiwezi kwenda mahali ambako haiheshimiki,” ilifafanua taarifa ya klabu hiyo.
Hata hivyo, pamoja na kutohudhuria hafla hiyo, Real Madrid iliibuka mshindi wa tuzo ya klabu bora ya mwaka kwa wanaume na kocha wake, Carlo Ancelotti alishinda tuzo ya kocha bora wa mwaka wanaume.
Nyota mwingine wa Real Madrid, Kylian Mbappe alifanikiwa kutwaa tuzo ya mshambuliaji bora wa mwaka ambayo alishinda sambamba na nyota wa Bayern Munich, Harry Kane huku tuzo ya mchezaji bora kijana ikienda kwa Lamine Yamal wa Barcelona.
Kwa mara ya pili mfululizo, Emiliano Martinez aliibuka mshindi wa tuzo ya Yashin inayotolewa kwa kipa bora wa mwaka na kiungo wa timu ya wanawake ya Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Aitana Bonmatí alishinda tuzo ya mchezaji bora wa soka wa dunia wa tuzo hiyo kwa wanawake.
Barcelona ilishinda tuzo ya klabu bora ya soka kwa wanawake huku kocha Emma Hayes akishinda tuzo ya kocha bora kwa soka la wanawake.
Hata hivyo, kumekuwa na hisia na mitazamo tofauti juu ya ushindi wa Rodri kwa tuzo hiyo ambapo baadhi ya mastaa wa soka duniani wamekubaliana na uamuzi wa kumchagua kiungo huyo kuwa mshindi huku wengine wakipinga.
Kiungo wa zamani wa Real Madrid, Clarence Seedorf alisema kuwa Rodri hakustahili kuibuka mshindi wa tuzo hiyo.
“Nadhani kuna matatizo baina ya Real Madrid na Uefa ambayo imeathiri baadhi ya vitu kwenye matokeo. Vinicius Junior ndiye aliyetakiwa kushinda tuzo. Ni aibu,” alisema Seedorf.
Kiungo wa Manchester City, Ilkay Gundogan amempongeza Rodri na kusema amestahili tuzo hiyo.
“Hongera kwa mchezaji mwenzangu Rodri kwa kushinda Ballon d’Or. Kwangu mimi hii imestahili vyema. Nina furaha ya kipekee kwa vile mmoja wa nafasi ya ulinzi ameshinda taji hili na sio kila siku mchezaji wa naafsi ya ushambuliaji,” alisema Gundogan.