Robo fainali daraja la kwanza, ukizubaa tu unaachwa

UKIZUBAA unaachwa. Ndiyo kinachoenda kutokea kwenye michezo ya robo fainali ya Ligi Daraja la Kwanza Dar es Salaam inayoanza kesho kwenye Uwanja wa Don Bosco, Oysterbay.

Kisasi ni cha Chang’ombe Boys kwa Mlimani B.C baada ya kufungwa katika mchezo wa hatua ya makundi kwa pointi 68-57 na zinakutana tena robo fainali.

Kocha wa Mlimani, Abbas Sanawe anajua Chang’ombe imewapania na amesema watakachofanya ni kupiga kwenye mshono na wasitarajie ushindi kwenye mchezo huo utakaoanza saa 2 usiku.

“Tuliifunga Chang’ombe, kweli tufungwe? Itakuwa ni jambo la ajabu sana,” alisema Sanawe na kuongeza wachezaji wameahidi kuivusha timu kutinga nusu fainali ya ligi hiyo kwani kiu yao ni kufika mbali na hadi BDL.

Katika mchezo huo, Mlimani B.C itawategemea nyota Martine Rogers, Baraka Kweka, huku Chang’ombe itakuwa na Jacobu Marenga, Brando Odhuno na Berry Kankonde.

Mchezo huo utatanguliwa na pambano kati ya Polisi na Yellow Jacket, Stein Warriors na Kigamboni Heroes, Kurasini Heat na Mbezi Beach.

Kurasini Yaitisha Mbezi Beach

Naodha wa Kurasini Heat, Dominic Zacharia amesema timu yake  imejipanga kuivuruga Mbezi beach kesho (jumamosi) kutokana na maandalizi waliyoyafanya.

“Tumejipanga kurudisha heshima iliyopotea miaka mitano iliyopita,” alisema Zacharia na kuongeza nyota wake wote watacheza wakiwamo Daud Daud, Haykal Ibrahim na Anaset maliselo.

Mbezi Beach kushusha vyuma

Wakati Zacharia akiwataja wachezaji wake, Mbezi beach inawategemea nyota wake Adam Ramadhani, Jackson Mrisho, Wilson Maketa na Arnold Harry na wanatarajiwa kuibeba timu hiyo kuibuka na ushindi.

Polisi, Yellow Jacket hakuna kulala

Polisi meendelea kujifufua katika fukwe za bahari eneo la Kigamboni, kujiandaa na mchezo dhidi ya Yellow Jacket ambayo nayo inafanya mazoezi Shule ya Sekondari ya Zanaki.

Katika mazoezi hayo, alikuwepo Lawi Mwambasi, Noeli Mwazembe, Augustino Kassimu, Augustino Kassimu, Issa Ismail na Fahmi Hamadi, huku Yellow ikiwategemea Gabriel Gilbert, Omary Njota na George Mwakyanjala.

Vita ya mmoja mmoja

Vita hii ilianzia hatua ya makundi na katika michezo 17waliocheza kuna nyota kadhaa walitupia na sasa wanashikana mashati kutafuta mwamba wao.

Fahm Hamadi wa Polisi alifunga pointi 268, George Mwakyanjala (Yellow Jacket) 235, Lawi Mwambasi (Polisi) 231, Martin Rodgers (Mlimani B.C) 224, Adam Ramadhani (Mbezi beach) 203, Dickson Thomas (Kigamboni Heroes) 192 na Jackson Mrisho (Mbezi beach) 190 hapa watauana.

Vita nyingine ni upande wa wafungaji wa pointi tatu ‘Three points’  mchuano utakuwa kwa Omary Njota wa Yellow Jacketaliyefunga pointi tatu mara 36, Jacob Malenga wa Chang’ombe Boys (34), Dominic Zacharia wa Kurasini Heat (28), Dickson Thomas (Kigamboni Heroes) 28, George Mwakyanjala (Yellow Jacket) 28, Daud Daud (Kurasini Heat) 26 na Abas Omary (Stein Warriors) 20.

Huko kwenye asisti nako ni balaa na watakaokabana koo ni Davis Msham wa Stein Warriors aliyetoa asisti mara 57, Malenga (Chang’ombe Boys) 43, Haykal Ibrahim (Kurasini Heat) 43, Issa Ismail (Polisi) 42 na Gabriel Gilbert (Yellow Jacket) 42.