
Mtandao wa habari wa lugha ya Kiebrania wa Kan umedai kuwa Qatar imewaambia viongozi wa kisiasa wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS kwamba “hawatakiwi tena” katika nchi hiyo ya Ghuba Uajemi.
Mtandao huo umedai, uamuzi huo wa serikali ya Doha umefikishwa kwa viongozi wa Hamas katika “siku za hivi karibuni”.
Imedaiwa kuwa, baadhi ya maseneta wa chama cha Republican nchini Marekani wiki hii waliiandikia barua serikali ya Biden kuiomba ibadilishe sera yake kuhusiana na Qatar.
Wakiongozwa na maseneta Roger Wicker na Jim Rish ambao ni wajumbe waandamizi katika kamati za Seneti za Huduma za Silaha na Masuala ya Kigeni, maseneta hao 12 wamesema ni wakati mwafaka wa kuzizuia mali za viongozi wa Hamas wanaoishi Qatar na kiongozi mwandamizi wa harakati hiyo Khalid Mash’al kuchukuliwa hatua za kisheria.
Sehemu moja ya barua ya maseneta hao inasema: “kuishinda Hamas kunakaribia kufikiwa, na kuondoa eneo salama la kuupa hifadhi uongozi wake ambalo unanufaika nalo ughaibuni ni muhimu sana kwa ajili kuishinda”…/