Ripoti yabaini 2024 ulikuwa mwaka wenye joto zaidi, wadau wachambua

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitangaza mwaka 2023 kuwa wenye joto zaidi, lakini rekodi hiyo imevunjwa tena.

Kwa mujibu wa ripoti yao mpya, The 2024 Annual Climate Statement for Tanzania, mwaka 2024 ulikumbwa na joto lililozidi wastani wa kawaida na kuufanya kuwa mwaka wenye joto zaidi tangu 1970, ukipita rekodi ya awali ya mwaka 2023.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wastani wa joto nchini kwa mwaka 2024 ulikuwa nyuzi joto 24.3, ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 0.7 juu ya wastani wa muda mrefu wa miaka 1991-2020. Ongezeko hilo la joto lilikuwa kati ya nyuzi joto 0 na 1 za sentigredi katika maeneo mengi ya nchi, huku maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria yakishuhudia viwango vya juu zaidi vya ongezeko, kati ya nyuzi joto 1 na 2 juu ya wastani.

Miezi iliyorekodi viwango vya juu zaidi vya joto ni Mei, Juni, Julai na Novemba. Sambamba na hali hiyo, kiwango cha mvua pia kiliweka rekodi, kulirekodiwa milimita 1,307.6 za mvua, ikiwa ni milimita 285.2 zaidi ya wastani wa muda mrefu. Sehemu kubwa ya nchi ilipata mvua zilizozidi kiwango cha kawaida, zikifikia kati ya asilimia 125 na 150 ya wastani.

Hata hivyo, maeneo ya Bonde la Ziwa Victoria, pwani ya kaskazini, nyanda za juu kaskazini-mashariki na ukanda wa magharibi yalipata mvua za kawaida.

Ripoti hiyo ilibainisha kuwa mwaka 2024 ulikuwa wa nne wenye mvua nyingi zaidi tangu 1970 na mwaka ulioshuhudia mvua nyingi zaidi katika miongo miwili iliyopita.

Wadau wachambua, washauri

Kutokana na mabadiliko haya, wataalamu wa mazingira wanashauri hatua za pamoja zichukuliwe ili kuzuia hali hii kujirudia, zikiwemo juhudi za upandaji miti na kupunguza matumizi ya magari yasiyokidhi viwango.

Mtaalamu wa Mazingira na mdau wa Maendeleo, Dk Aidan Msafiri amesema mabadiliko haya yanatokana na shughuli za binadamu, hususan ukataji miti kwa ajili ya mkaa.

Amenukuu Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira Nchini ya mwaka 2019, ambayo inaonesha kila mwaka zaidi ya hekta 469,420 za misitu zinaharibiwa kwa matumizi ya kuni na mkaa.

“Kila mtu anataka kumiliki gari, hata mabovu. Magari chakavu yanayoondolewa kwenye nchi nyingine yanaletwa huku na kutumika, hali inayoongeza uzalishaji wa hewa ya ukaa, ambayo inaathiri mazingira,” amesema Dk Msafiri.

Amesema joto kali lililoshuhudiwa sasa ni matokeo ya uharibifu wa mazingira uliofanyika kwa kipindi cha miaka 40 iliyopita.

Amebainisha kuwa uwezo wa nchi kuondoa hewa ya ukaa ni mdogo ukilinganisha na kiasi kinachozalishwa.

“Ukataji wa mkaa umeongezeka na miti haioteshwi. Tuna sera ambazo hazilingani na ukubwa wa tatizo. Hakuna tatizo linaloweza kutatuliwa kwa makaratasi pekee, bali kwa mabadiliko ya tabia na hatua za kila siku,” amesema.

Mdau wa mwingine wa Mazingira, Shamim Nyanda amesema ukataji holela wa miti na shinikizo katika bahari ni miongoni mwa vyanzo vya ongezeko la joto.

“Bahari husaidia kunyonya hewa chafu angani, lakini baadhi ya nchi zinatumia teknolojia kunyonya hewa hiyo na kuizika baharini ili kupunguza joto. Tanzania inapaswa kuwekeza kwenye tafiti zitakazotuelekeza jinsi ya kupunguza joto. Tafiti hizi zinahitaji wataalamu wabobezi wenye uwezo wa kubuni mbinu madhubuti,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Nipe Fagio, Ana Rocha amesema Tanzania haiwezi kukabiliana na changamoto hii peke yake, bali inahitaji ushirikiano wa kimataifa. “Tunahitaji kuzuia hewa chafu kupitia usimamizi bora wa taka. Taka zinapaswa kutenganishwa, kutengenezwa kuwa mbolea, kurejewa, na zingine zisizalishwe kabisa. Asilimia 60 hadi 70 ya taka zinazozalishwa Dar es Salaam ni mabaki ya vyakula. Zikikusanywa kiholela, huzalisha gesi hatari kwa mazingira,” amesema.

Kwa mujibu wa Ripoti ya UNEP Emissions Gap 2019, ili kudhibiti ongezeko la joto lisiwe zaidi ya nyuzi joto 1.5, uzalishaji wa gesi chafu unapaswa kupunguzwa kwa asilimia 7.6 kila mwaka hadi kufikia mwaka 2030. Hatua nyingine muhimu ni kuhifadhi na kuboresha maeneo ya asili ardhini na majini ili kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa.

Ripoti hiyo pia inasisitiza kupunguza uzalishaji wa gesi ya methani, ambayo ina mchango mkubwa katika ongezeko la joto duniani. Inaelezwa kuwa zaidi ya asilimia 75 ya gesi hiyo inaweza kupunguzwa kwa kutumia teknolojia za kisasa. Na hadi asilimia 40 inaweza kupunguzwa bila gharama yoyote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *