Ripoti: Washington inapuuza kesi 500 za Israel kuwadhuru raia wa Gaza kwa silaha za Marekani

Serikali ya Washington imebaini takriban ripoti 500 za raia wa Ukanda wa Gaza kujeruhiwa na kuuawa na vikosi vya jeshi la Israel kwa kutumia silaha zinazotolewa na Marekani, lakini imeshindwa kuchukua hatua yeyote.

Hayo yamo katika ripoti ya gazeti la Washington Post na shirika la habari la Reuters iliyosema Jumatano wiki hii kwamba matukio hayo yamekusanywa tangu Oktoba 7, 2023 na Mwongozo wa Kukabiliana na Matukio ya Madhara ya Kiraia wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, ambacho ni chombo rasmi cha kufuatilia na kutathmini utumiaji mbaya wa silaha za Marekani.

Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje wamekusanya matukio kutoka kwa umma na vyanzo vingine, ikiwa ni pamoja na ripoti za vyombo vya habari, mashirika ya kiraia na mawasiliano ya serikali ya kigeni.

Akijibu maswali kuhusu suala hilo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Matthew Miller amesema utawala wa Rais Joe Biden unakiri kwamba ni jambo la busara kusema Israel imekiuka sheria za kimataifa katika vita vya Gaza lakini kutathmini matukio ya mtu binafsi ni “kazi ngumu sana.”

Maelfu ya watoto wameuawa kwa silaha za Marekani katika Ukanda wa Gaza

John Ramming Chappell, mshauri wa sheria na sera anayezingatia usaidizi wa usalama wa Marekani na mauzo ya silaha katika Kituo cha Raia katika Migogoro, ameiambia Washington Post kwamba maafisa wa serikali ya Marekani “wanapuuza ushahidi wa kuwepo madhara makubwa kwa raia na ukatili ili kudumisha sera ya kutuma silaha bila masharti” kwa utawala wa Israel.

Ikiungwa mkono na kusaidiwa na Marekani na washirika wake wa Magharibi, Israel ilianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, na hadi sasa imeua karibu Wapalestina elfu 50 na kujeruhi wengine zaidi ya laki moja.