
Takriban wanajeshi sita wa Israel wameripotiwa kujiua katika miezi ya hivi karibuni, kutokana na matatizo ya kisaikolojia yaliyosababishwa na vita vya muda mrefu dhidi ya Gaza na Lebanon.
Gazeti la kila siku la Israeli la Yedioth Ahronoth liliripoti Ijumaa kwamba idadi ya watu wanaojiua inaweza kuwa kubwa zaidi ya inayoripotiwa rasmi.
Jeshi la utawala ghasibu wa Isarel hadi sasa limejizuia kutoa idadi rasmi ya watu waliojiua, licha ya kuahidi mara kwa mara kufanya hivyo.
Taarifa za hivi karibuni zinasema kwa akali wanajeshi 10,000 wa utawala haramu wa Israel wamefika katika vituo vya matibabu na kuomba kupatiwa huduma ya afya ya akili.
Ripoti iliyochapishwa na gazeti la Israel la Jerusalem Post mwezi Juni iliangazia hali “ya wasiwasi” wa afya ya akili inayowakabili wanajeshi vamizi wa Israel wanaorejea kutoka Ukanda wa Gaza.
Baadhi ya ripoti zinaeleza kwamba, mamia ya wanajeshi wa utawala haramu wa Israel wamekumbwa na maradhi ya akili tangu vilipoanza vita vya Gaza Oktoba mwaka jana (2023).
Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth limeripoti kuwa, karibu asilimia 80 ya wanajeshi wa Israel waliokwenda kuomba matibabu ya akili kwenye vituo vya matibabu na mahospitali ya utawala wa Kizayuni wamo kwenye orodha ya majeruhi wa vita vya Gaza. Utawala wa Kizayuni ulidhani vita dhidi ya Gaza vingemalizika baada ya wiki kadhaa lakini kufuatia mapambano shupavu ya Wapalestina utawala huo umeshindwa kufikia malengo yake ya kivita.