
Dar es Salaam. Baadhi ya vituo vya afya vikilalamika kucheleweshewa malipo na mengine kukataliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), hivyo kuathiri ukwasi na kushindwa kujiendesha, wadau wanapendekeza namna ya kushughulikia changamoto zilizopo.
Kwa mujibu wa wadau waliozungumza na Mwananchi kuna haja ya kupitia sababu za kukataliwa madai na NHIF itoe mrejesho kwa wakati kwa hospitali ili kuepuka makosa kujirudia.
Inapendekezwa kufanyika semina na mafunzo kuhusu taratibu za madai na utoaji huduma na kurekebishwa mwongozo wa matibabu wa Taifa ili kuepusha migongano kati ya madaktari na NHIF kuhusu tiba zinazopaswa kulipwa.
Suala lingine linalopendekezwa ni mtaalamu huru (mrufani) kutumika kusuluhisha migogoro kati ya NHIF na watoa huduma.
Baadhi ya vituo vya afya vya binafsi na vya umma vinalalamikia malipo yao kukataliwa na NHIF, hivyo ukwasi wao kuathiriwa kutokana na kuwapo upotevu wa fedha.
Malipo kukataliwa na NHIF ni miongoni mwa mambo aliyoyabaini Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere katika ripoti iliyotolewa Machi 28, 2024 kuhusu ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Alizungumzia masuala yaliyobainishwa wakati wa ukaguzi wa ufanisi wa mashirika hayo kwa sekta ya afya, yakijumuisha NHIF iliyokataa madai yenye thamani ya Sh11.83 bilioni yaliyowasilishwa na hospitali nne za umma.
Hospitali hizo alizitaja kuwa ni Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).
Si hivyo tu, CAG akiwasilisha ripoti ya ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2023/24 Machi 27, 2025 amesema kuna ongezeko la madai ya hospitali yaliyokataliwa.
“Mfuko ulikataa madai ya Sh11.23 bilioni kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila, sawa na asilimia 16 ya madai yote yaliyowasilishwa kutoka hospitali za rufaa za mikoa na wilaya.
“Madai hayo yalikataliwa kutokana na makosa ya bei, dozi, bidhaa zisizo sahihi na adha zisizotakiwa hali hiyo imeathiri ukwasi wa hospitali hizo kwa kupunguza mapato yaliyotarajiwa,” alisema.
Nini kifanyike
CAG katika ripoti ya mwaka wa fedha 2022/23 alipendekeza kuweka utaratibu wa kupitia sababu zote za kukataliwa na kutoa mrejesho kwa wakati kwa maofisa wanaohusika katika idara na sehemu zote zinazohusika na utoaji wa huduma za afya ili kuzuia au kupunguza kujirudia kwa tatizo katika siku zijazo.
Pia alipendekeza kushauriana na NHIF kwa ajili ya kutoa mafunzo na semina za mara kwa mara kuhusu utoaji wa huduma za afya ambao hautaathiri mahitaji yaliyobainishwa.
“Napendekeza NHIF na hospitali zikae pamoja kupunguza changamoto hizi ambazo zimekuwa zikijirudia,” alisema CAG akiwasilisha ripoti ya ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2023/24 Machi 27, 2025.
CAG amesema kuna ongezeko la madai ya hospitali yaliyokataliwa, akieleza madhara yake kwa ukwasi.
Mtaalamu wa masuala ya bima, Dk Anselmi Anselmi anasema kwa upande wa dawa, NHIF hulipia zile zilizopo kwenye mwongozo wa dawa muhimu na kama aliyopewa mgonjwa haipo kinachofanyika ni kutafuta dawa mbadala ambayo atapewa.
Kuhusu ngazi za utoaji wa uamuzi wa tiba anasema: “Hapa daktari anakuwa wa kwanza mwenye haki, anamuona mgonjwa ana kwa ana, ameangalia vipimo lakini upande wa pili kutokana na miongozo na matakwa ya sheria wanaangalia mwongozo unasemaje.”
Dk Anselmi anapendekeza ili kuondoa changamoto, mwongozo wa matibabu wa Taifa uangaliwe.
“Kuna kitu kinaitwa ‘mrufani’ ambaye anakuwa mtaalamu nje ya mfuko, huyu anaweza kutumika panapokuwa na misuguano baina ya mteja na NHIF,” anasema.
Mtaalamu wa afya ya umma, Dk Ali Mzige anasema ili kuondokana na changamoto zilizopo, maboresho ya sheria ni muhimu lakini zaidi ni kuhakikisha nafasi za uongozi zinashikwa na wenye ujuzi wa taaluma husika.
Tayari Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni Februari 14, 2025 katika mkutano wa 18 wa Bunge la 12.
Miongoni mwa marekebisho yanayopendekezwa ni kurekebishwa kwa kuondoa sharti la mfuko kuthibitisha watoa huduma za afya, badala yake kuwatambua wanaothibitishwa na Wizara ya Afya. Lengo la marekebisho ni kuondoa sharti la uthibitishaji ambalo lipo nje ya wigo wa sheria hiyo.
Pia, inapendekezwa marekebisho ili kutoa masharti ya malipo ya fedha kwa huduma zinazotolewa na mtoa huduma za afya kuhamishwa moja kwa moja kwenye akaunti ya mtoa huduma badala ya malipo kuhamishiwa kwenye akaunti ya mfuko wa huduma za afya ili kuwezesha madai kulipwa kwa wakati na mfuko kwa ajili ya utoaji wa huduma za afya kwa ufanisi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Aphtha, Dk Samwel Ogillo anasema changamoto kubwa kwa pande zote ni kile kinachotajwa kuwa udanganyifu ambao mara nyingi haupo.
Anasema iwapo dawa itaandikwa na kukosewa hata code number (namba ya utambulisho wa bidhaa) NHIF huhesabu kama udanganyifu na hakuna nafasi ya kujieleza.
Dk Ogillo anasema mtoa huduma alikutwa na udanganyifu NHIF huanza kumkagua na kuhitaji risiti, ambazo hutokea changamoto kutokana na nyingi za kielektroniki (EFD) hufutika, hivyo wengi hushindwa kutoa ushahidi wa risiti za mwaka mmoja au mitatu nyuma.
Ili kutatua hilo, anashauri Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) wasikilize upande wa pili. Kwa kuwa awali hapakuwa na msuluhishi.
Amesema kwa sasa Tira inasimamia masuala ya bima, hivyo yeyote anayetoa huduma ya bima anatakiwa kujisajili kwa mamlaka hiyo.
Mkurugenzi wa Tira, Dk Baghayo Saqware amesema tayari wameanza kushughulikia malalamiko tangu Januari 2025.
“Tumeshapokea malalamiko ya hospitali kadhaa tunayashughulikia, wengine tumeshawasuluhisha. Kama kuna mtu mwenye matatizo anatakiwa kuandika barua aeleze changamoto yake ama afike ofisini kwetu tutampa utaratibu au aangalie website zetu,” amesema.