RIPOTI MAALUM-1: Anayewafelisha wanamichezo Bongo ni huyu

Umewahi kujiuliza ni kipi hasa kinawafanya wanamichezo wa Kitanzania kushindwa kufanya vizuri hasa mashindano ya kimataifa? Weka kando mchezo wa mpira wa miguu ambao unatajwa kuwa ndiyo unapendwa zaidi nchini na duniani, lakini licha ya kuonekana kuna mwanga wa kufanya vizuri kwa timu, bado siyo kwa kiwango kinachotakiwa.

Sasa njoo upande wa michezo mingine ikiwemo ngumi, riadha, judo na hata kuogelea. Kila tunapokwenda kushiriki mashindano makubwa kama Olimpiki tunarudi kwa aibu kubwa.

Siku kumekuwapo kujificha katika kivuli cha hali ya hewa kuwatesa wanamichezo wanapokwenda kushindana kimataifa, lakini ukweli haupo hivyo. Kuna watu wanahusika moja kwa moja kusababisha hayo.

Michuano ya Olimpiki 2024 iliyofanyika Paris nchini Ufaransa, Tanzania ilitia aibu katika mashindano matatu iliyopeleka washiriki saba. Katika michuano hiyo iliyoshirikisha nchi 204 kukiwa na matukio 329 yaliyokuwa na michezo 32 ikiwahusisha wanamichezo 10,714, Tanzania ilirudi mikono mitupu wawakilishi wake wakiishia hatua za mwanzoni.

Wakati Tanzania ikirudi mikono mitupu, Kenya na Uganda ambazo ni nchi jirani zilibeba medali.

Uchunguzi wa Mwananchi uliofanyika sambamba na kuzungumza na viongozi wa vyama vya michezo, wadau, wanamichezo na viongozi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), umebaini BMT wana mchango katika hilo.

Kwa mujibu wa Sheria Na.12 ya Mwaka 1967 na Marekebisho yake Na. 6 ya 1971 ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kifungu cha 3 (1) Kazi za Baraza zitakuwa (a) Kuendeleza, kustawisha na kudhibiti aina zote za michezo ya ridhaa kitaifa kwa ushirikiano na vyama au vikundi vya michezo vya ridhaa ya hiari kwa kutoa; (a) mafunzo na watumishi wengine, (b) Misaada kwa Vyama au Vikundi vya Kitaifa, (c) Viwanja vya Michezo na fursa nyinginezo, (d) Vifaa vya michezo na vitu vingine ambavyo ni muhimu kwa ajili ya kuendeleza michezo.

Ifahamike kwamba BMT ni Taasisi ya Serikali iliyoundwa na Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa sheria Na. 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake ya sheria Na.6 ya mwaka 1971 na Kanuni za Baraza la Michezo la Taifa na Kanuni za usajili Na.442 za mwaka 1999 na ndio chombo pekee kilichopewa mamlaka na Bunge kusimamia michezo nchini.

Aidha BMT ni Taasisi iliyopo chini ya Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo.

Wakati sheria ikieleza hayo, sera ya maendeleo ya michezo Tanzania imesisitiza hilo kupitia kifungu 5.1.3 inayobainisha Kazi za Baraza la Michezo la Taifa ambapo jukumu kubwa la Baraza ni kuendeleza michezo nchini kwa kushirikiana na vyama vya michezo.

Linapokuja suala la kuwa na miundombinu bora, BMT ikiwa na jukumu la kutoa viwanja vya michezo kama ambavyo sheria ya baraza hilo inavyoelekeza, suala  hilo halifanyiki kwa kiwango kinachoridhisha.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba, kupitia mchezo wa mpira wa miguu ambao ndiyo unapendwa na kupewa kipaumbele zaidi nchini, viwanja vingi vinavyotumika kwa mashindano havina ubora.

Msimu uliopita wa 2023-2024 kwenye Ligi Kuu Bara, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa nyakati tofauti lilivifungia viwanja 10 kati ya 15 kutokana na kukosa vigezo kikanuni na sheria za mpira wa miguu. Miongoni mwa viwanja hivyo ni Uhuru uliopo Dar es Salaam ambao hadi sasa unaendelea kufanyiwa maboresho na hautumiki kwa mechi za Ligi Kuu wala Championship.

Taarifa ya TFF iliyotolewa Desemba 22, 2023, ilieleza: “Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeufungia Uwanja wa Uhuru uliopo Dar es Salaam usitumike kwa mechi za Ligi Kuu kutokana na kukosa vigezo kikanuni na sheria za mpira wa miguu.”

Sera ya maendeleo ya michezo kifungu cha 7 inayozungumzia ujenzi na utunzaji wa viwanja vya michezo imebainisha huduma muhimu za kukuza na kuendeleza michezo ni pamoja na ubora wa viwanja vya michezo.

Katika suala la ubora, viwanja 13 vinavyotumika kwa Ligi Kuu Bara 2024-2025, ni viwili pekee ndivyo vyenye hadhi ya kimataifa vinavyotumika kwa mechi za michuano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sambamba na ile ya Shirikisho la Soka la Kiamataifa (Fifa). Viwanja hivyo ni Azam Complex na Benjamin Mkapa vilivyopo jijini Dar es Salaam.

Mbali na mpira wa miguu, hali ni mbaya zaidi upande wa michezo mingine ikiwemo kuogelea. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tanzania yenye wakazi 61,741,120 (milioni sitini na moja, laki saba, arobaini na moja elfu, mia moja na ishirini) haina bwawa la kuogelea lenye viwango vya Olimpiki linalofikia mita 100.

Machi 18, 2021, Mtandao wa Mwananchi uliandika habari iliyokuwa na kichwa cha habari kilichosomeka; “Mabwawa ya kuogelea yanaitesa Tanzania.”

Kocha wa Mchezo wa Kuogelea ambaye pia ni mwamuzi wa mchezo huo na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Noel Kiunsi, anasema Tanzania inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mabwawa ya kuogelea yenye viwango vya kimataifa.

“Kwa kweli hatuna bwawa letu la mchezo wa kuogelea, hivyo tunalazimika kukodisha au kuomba msaada kwenye shule ambazo zina mabwawa pale tunapokuwa na mashindano,” anasema Kiunsi.

Mdau huyo anasema wanapokodisha wanalazimika kulipa Sh5,000 kwa mtu mmoja na kama ni timu hulipa Sh600,000 kwa siku.

“Ni jukumu la Serikali kujenga bwawa la kuogelea kama ambavyo imefanya Serikali ya Kenya,” anasema Kiunsi.

Gharama za ujenzi wa bwawa moja inayokadiriwa kufikia Sh1.9 bilioni, imekuwa kikwazo huku BMT kupitia Serikali ikiwa katika mikakati ya kujenga lenye hadhi ya kimataifa. Mwaka 2017, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, alitoa ahadi Serikali kujenga mabwawa 10 ya kisasa ya kuogelea.

Taarifa hiyo iliripotiwa na Michuzi Blog iliyoandika kichwa cha habari kilichosomeka hivi; “SERIKALI KUJENGA MABWAWA 10 YA KUOGELEA, TANZANIA YAANZA KWA VISHINDO.” Tangu kutolewa kwa ahadi hiyo, lakini hadi sasa 2025 kuna mchakato wa kujengwa moja.

Katika michuano ya Olympiki iliyofanyika Paris kuanzia Julai 2024 hadi Agosti 2024, Tanzania iliwakilishwa na waogeleaji wawili ambao ni Collins Saliboko upande wa wanaume na mwanamke Sophia Latif.

Waogeleaji hao walishindwa kufanya vizuri mbele ya wapinzani wao huku kilio kikubwa kikiwa ni kukosa maandalizi stahiki kutokana na viwango vya mabwawa ya kuogelea kipindi cha maandalizi tofauti na waliyokwenda kwenye mashindano.

Baada ya kutoa kilio hicho kila mmoja kwa nafasi yake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa alilipokea hilo na kulitolea ufafanuzi.

“Changamoto ya kukosekana kwa mabwawa ya kuogelea yenye viwango vya Olimpiki tumeipokea na tunaifanyia kazi haraka, tukianza na bwana ambalo lipo kwenye ujenzi muda huu katika eneo changamani la Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam,” anasema  Msigwa.

Oktoba 6, 2024, Rais wa Chama cha Gofu Wanawake Tanzania, (TLGU), Queen Siraki akizungumza wakati wa kufunga mashindano ya CDF TROPHY 2024, alibainisha kilio chao katika uchache wa viwanja vya gofu.

Siraki anasema kwamba kuna baadhi ya mikoa hakuna kabisa viwanja vya gofu hali inayowalazimu kutokuwa na wigo mpana wa kuusambaza mchezo huo hapa nchini.

“Kwa mfano tukienda Zanzibar hadi kuufikia ulipo uwanja wa gofu ni mbali sana. Tungependa kiwanja kiwe maeneo ya karibu pengine hata mtu akiwa na ratiba za kusubiri boti basi autumie muda huo kucheza gofu kama sehemu ya kujifurahisha.

“Lakini pia mikoa mingine tungependa kuwepo kwa hivi viwanja isiwe tu Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro na Morogoro, hata Mwanza kuwe na kiwanja sambamba na mikoa mingine kwani itasaidia katika kuueneza mchezo huu na kuukuza zaidi,” anasema Siraki.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa BMT, Najaha Bakari anasema: “Tumekuwa tukisisitiza katika kila halmashauri au mkoa kuwe na viwanja vile ambavyo vimetengwa na Serikali basi waendelee kushirikiana na hizo Serikali zilizopo katika ngazi zao kuviendeleza ikiwemo vile viwanja vya shule kuviweka katika mazingira salama ili watoto waweze kucheza na wadau mbalimbali wanaopenda maendeleo ya michezo wavitumie hivyo viwanja, ili tuweze kufikia katika hali nzuri ya miundombinu ya michezo.

“Kama tunavyojua Serikali peke yake haiwezi, hivyo kuwe na ushirikiano mzuri na wadau mbalimbali ili kuwekeza katika miundombinu hiyo katika kuiboresha.”

VIFAA NA MISAADA

Katika ishu nzima ya utoaji wa vifaa vya michezo na misaada kwa vyama, BMT imekuwa ikisuasua.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Pooltable Tanzania, Wilfred Makamba, wanapopitia changamoto ya vifaa na maandalizi pindi wanapokuwa na shughuli za mchezo huo hawasiti kupiga hodi BMT kuomba msaada.

Hata hivyo, kiongozi huyo anabainisha kwamba, kubwa zaidi wanalopata ni mwongozo wa kwenda sehemu kupata msaada zaidi wa kifedha.

“Kiukweli kwa namna moja ama nyingine BMT wanatusaidia na tunashirikiana nao vizuri, pale tunapokwama kwenda kuomba msaada ikiwemo kifedha kwa ajili ya kufanya mashindano, wanatuandikia barua ambayo inatupa mwongozo wa kwenda popote kuomba udhamini,” anasema Makamba.

Ofisa Habari wa BMT, Bakari alipozungumza na Mwananchi anasema: “Kwa mwaka hatuna kikomo maalumu tunatamani kuona labda mkoa fulani unakuwa tayari kwa ajili ya mafunzo unatupa taarifa, huku wakiwa wamewaandaa watu wao kwa ajili ya kupokea hayo mafunzo, sisi tupo tayari muda wowote tunaenda.”

MATOKEO YAKE

Kukosekana kwa miundombinu bora sambamba na vyama kukosa msaada wa vifaa vya michezo kunasababisha wanamichezo kushindwa kufikia kiwango cha juu cha ushindani, hivyo kupunguza uwezo wao katika michezo wanayoshiriki.

Lakini pia wanamichezo wanaposhindwa kupata mazingira bora ya kufanya michezo, ushiriki wao unashuka. Hii inapelekea kukosekana kwa vipaji vipya michezoni.

Katika hatua nyingine, Tanzania inakosa nafasi nzuri katika mashindano ya kimataifa kwa sababu ya wanamichezo kukosa fursa ya mafunzo bora na vifaa vya kisasa. Michuano ya Olimpiki iliyofanyika 2024 Paris, Tanzania iliwakilishwa na wanamichezo saba pekee wakiwemo wanariadha wanne, waogeleaji wawili na mmoja judo. Kati ya hao hakuna aliyefanya vizuri.

Majirani Kenya walipeleka washiriki 81 wakarudi na medali 11 huku Uganda wakiambulia mbili kati ya washiriki 24 waliokwenda kuwakilisha taifa hilo.

Hii ni ishara kwamba unapopeleka wanamichezo wengi katika mashindano ni njia mojawapo ya kujiwekea nafasi ya kupata ushindi lakini uchache wa washiriki suala la ushindi linachukua nafasi finyu. Katika Olimpiki mwaka 2024, michezo 32 ilifanyika ikiwemo Wushu, Judo, Riadha, mpira wa wavu, mpira wa miguu, kuogelea, kunyanyua vitu vizito, tenisi, karate, kuendesha baiskeli na mingineyo. Orodha hiyo ya michezo inatoa majibu kwamba kama kungekuwa na wanamichezo wengi Tanzania isingetoka patupu ingawa wakati mwingine inaweza kutokea bahati kukawa na mshiriki mmoja na ndiye akafanya vizuri. Bado Tanzania inasaka medali za olimpiki, rekodi zinaonyesha kwamba, Tanzania ina medali mbili pekee za olimpiki ambazo zote ni za fedha walizoshinda mwanariadha wa mbio za mita 5000, Suleiman Nyambui na Filbert Bayi katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi, hiyo ilikuwa mwaka 1980 jijini Moscow, Russia.

ITAENDELEA KESHO