Ripoti: Askari wasiopungua sita wa jeshi la Israel wamejiua katika miezi ya karibuni

Askari wasiopungua sita wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel wameripotiwa kujiua katika miezi ya hivi karibuni, kutokana na matatizo ya kisaikolojia yaliyosababishwa na vita vya muda mrefu dhidi ya Ghaza na Lebanon.

Gazeti la kila siku la Israel la Yedioth Ahronoth limeandika katika toleo lake la jana Ijumaa kwamba idadi ya askari hao wa Kizayuni wanaojiua inaweza kuwa kubwa zaidi ya iliyoripotiwa.

Jeshi la utawala wa Kizayuni hadi sasa limekataa kutoa takwimu za idadi rasmi ya askari wake waliojiua, licha ya kuahidi mara kadhaa kuwa litafanya hivyo.

Ripoti ya Yedioth Ahronoth imeeleza kuwa, maelfu ya askari wanatafuta msaada katika kliniki za tiba ya matatizo ya akili, huku karibu theluthi moja ya walioathirika wakionyesha dalili za ugonjwa wa mfadhaiko wa baada ya kupatwa na kiwewe.

Ripoti ya gazeti hilo imeongeza kuwa, idadi ya wanajeshi wa Israel wanaopata matatizo na athari za kisaikolojia inaweza kuzidi wale walio na majeraha ya kimwili yaliyotokana na vita.

Tangu Oktoba 7, 2023 jeshi la utawala wa Kizayuni limeanzisha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza, kwa malengo yanayodaiwa kuwa ni kuiangamiza Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS na kuwakomboa mateka wa Kizayuni wanaoshikiliwa na Muqawama wa Palestina huko Ghaza.

Licha ya kila aina ya vitendo vya kishenzi na kinyama ulivyofanya katika eneo hilo tangu wakati huo hadi sasa, yakiwemo mauaji ya kimbari ya zaidi ya Wapalestina 44,000 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, utawala ghasibu wa Israel mpaka sasa hivi haujaweza kufikia hata moja kati ya malengo hayo…/