Ripota wa Umoja wa Mataifa aishutumu Uingereza kwa kukana mauaji ya kimbari huko Gaza

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu amekosoa matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza kuhusu mauaji ya kimbari yanayofanyika huko Gaza na kusema kwamba anakanusha kutokea jinai hiyo katika eneo hilo la Palestina.

Francesca Albanese  amemtaja Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Lammy kuwa “mkanushaji wa mauaji ya kimbari” na kusema kwamba Uingereza haijafanya “chochote” kuzuia ukatili huko Gaza.

Tovuti ya habari ya Middle East Eye imechapisha matamshi hayo na kuandika kuwa: Mwishoni mwa mwezi Oktoba, Lammy alikanusha mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Gaza.

Amesema, yumkini kauli ya Lammy ilitolewa kwa “maslahi ya kisiasa”, lakini hata hivyo, kauli kama hiyo inaweza kumuarifisha mtu kama “mkanushaji wa mauaji ya kimbari”.

Tarehe 29 Oktoba, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Lammy alisema kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel haufanyi mauaji ya kimbari huko Gaza, kwa sababu idadi ya mashahidi katika mashambulizi yake haifiki mamilioni ya watu!!

Maelfu ya watoto wameuawa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu  anasema, hakujua kuwa Lammy ni wakili, na kuongeza kuwa inashangaza kusikia maoni kama hayo kutoka kwa mtu ambaye anajua sheria.

Karibu Wapalestina elfu khamisini wameuawa shahidi, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, katika mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza. Maelfu ya Wapalestina wengine hawajulikani waliko, na inadhaniwa kuwa wako chini ya vifusi vya maelfu ya nyumba zilizoharibiwa za Ukanda wa Gaza.