
Manchester, England. Magwiji wa soka la Ulaya Rio Ferdinand na Robbie Savage wamemponda kipa wa Man United, Andre Onana na kusema hakuwa na mawasiliano mazuri na Patrick Dorgu wakati Ipswich Town ikifunga bao la kwanza kwenye Uwanja wa Old Trafford jana.
Katika mchezo huo, United ilishinda mabao 3-2, lakini mastaa hao wa soka wa zamani wamesema kuwa bao la kwanza la Ipswich lililofungwa na Jaden Philogene ni uzembe wa kipa huyo raia wa Cameroon ambaye kwa siku za hivi karibuni amekuwa na makosa mengi.
Ushindi huo umeisaidia United kutoka nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi Kuu England na kusogea hadi ya 14, ikiwa na pointi 33 baada ya kucheza michezo 27.
Katika bao hilo, Onana alitoka langonin kuufuta mpira lakini kabla hajaufikia Dorgu aliugonga akiwa na nia ya kumpasia kipa huyo, lakini akapishana nao.
“Sawa heshima anatakiwa kupewa Jaden Philogene, kutokana na juhudi ambazo alizionyesha, lakini napata shida kwanini Onana alitoka langoni wakati mpira alikuwa akimiliki beki wake na kulikuwa hakuna shida hata kidogo.
“Kwangu naamini kuwa alikuwa sahihi sana kama angebaki kwenye eneo lake kuliko kuja kwenda kuufuata mpira ambao hana uhakika nao, naamini haya ni makosa yake,” alisema Savage staa wa zamani wa Man United, Leicester City na Blackburn Rovers.
Hata hivyo, Ferdinand ambaye amekuwa havutiwi na kipa huyo kutokana na makosa mengi ya kujirudia alisema naye anaunga mkono kuwa bao hilo limesababishwa na kipa huyo.
“Ipswich wameanza vizuri, sifikiri kama Dorgu alimuangalia kipa wake amekaa wapi wakati anapiga mpira, lakini kwangu naamini Onana alitakiwa kubaki langoni mwake, beki wake alikuwa tayari ameumiliki mpura bila shida yoyote, alikuwa anaweza kumpasia na kuomba tena ule mpira.
“Kila siku huwa namwambia Andre ni kipa mzuri sana, Ulaya nzima inamtambua, lakini kwenye Premier League hajafanya vizuri, kiwango chake siyo bora, anatakiwa kubadilisha haya makosa, kama mambo hayatakwenda vizuri nafikiri Juni kutakuwa na jambo lingine,” alisema Rio ambaye ni beki wa zamani wa Man United.