Rihanna anavyocheza na akili za mashabiki

Marekani. Staa wa pop duniani, Robyn Rihanna Fenty maarufu kama Rihanna, 37, huenda akatoa albamu ya tisa mwaka huu baada ya ukimya wa karibu muongo mmoja huku akiendelea na mambo mengine ambayo yamebadilisha historia ya maisha yake. 

Rihanna akiwa na umri wa miaka 18 alitoa albamu ya kwanza, Music of the Sun (2005), lakini mafanikio makubwa yalikuja alipoachia albamu ya tatu, Good Girl Gone Bad (2007) na kushinda Grammy mara ya kwanza.

Baada ya kuachia albamu ya nane, ANTI (2016), Rihanna, bilionea namba tatu duniani upande wa wanamuziki aliamua kuwa mchoyo kwa mashabiki kwa kuwanyima ladha mpya masikioni mwao. 

Hata hivyo, kipindi hicho cha miaka tisa ya uchoyo wa Rihanna kwa mashabiki kimekuwa na maana na faida kubwa kwake kuanzia kazi ya muziki, familia na biashara, hivyo ukimya huo haukuwa bure hata kidogo.

Katika mahojiano na Harper’s Bazaar hivi karibuni, Rihanna anasema amekuwa studio kwa miaka minane akirekodi, lakini kubwa zaidi anashukuru hatimaye ametambua kile anachotaka kisikike katika albamu  mpya.

Anasema muziki wake mpya hautakuwa kitu chochote ambacho mtu yeyote anatarajia na hautakuwa wa kibiashara au wa redio, bali utakuwa muziki ambao sanaa yake inapaswa kuwepo wakati huu.

Mkali huyo wa kibao, Diamonds (2012), anasema lazima mashabiki waione thamani ya kusubiri miaka tisa, huku akitupilia mbali uvumi kuwa albamu hiyo itakuwa ya mahadhi ya reggae kwani muziki wake mpya hauna aina.

Rihanna anasisitiza kuwa mashabiki hawawezi kusubiri kitu chenye kiwango duni, lakini bahati mbaya hakusema ni lini albamu hiyo itatoka na itaitwaje ingawa mashabiki wameshaipa jina la “R9” ktuokana na kuwa na kipindi kirefu.

Hadi sasa albamu alizotoa ni Music of the Sun (2005), A Girl like Me (2006), Good Girl Gone Bad (2007), Rated R (2009), Loud (2010), Talk Talk Talk (2011), Unpologetic (2012) na ANTI (2016) huku saba za awali zikitoa nyimbo 14 zilizoshika namba moja Billboard Hot 100.

Mwaka uliopita Rihanna aliwaweka roho juu mashabiki baada ya kuonekana amevalia tisheti iliyoandikwa “I’m retired” – nimestaafu na wengi wakahisi ameamua kuachana na muziki, lakini ila baadaye alisema ulikuwa utani.

“Ninapenda kuwachukiza mashabiki wangu kidogo. Ni sawa maana na wao kuna muda hunichukiza, kwa hivyo tunalipizana,” alisema Rihanna wakati akizungumza na Entertainment Tonight.

Kauli hiyo ilikuja baada ya mwaka 2019 kuchapisha video Instagram akicheza na mbwa wake na kuandika; ‘Ninasikiliza R9’ hapo tena mashabiki wakawa roho juu na kudhani albamu mpya kutoka kwake ipo mbioni, lakini haikuwa hivyo.

Hatimaye baada ya miaka sita akawapa mashabiki kitu kipya akiachia nyimbo mbili – Born Again (2022) na Lift Me Up (2022) ila hizi zilikuwa ni maalumu kwa ajili ya kutumika katika filamu ya Black Panther: Wakanda Forever.

Lakini, kipindi cha ukimya, yaani uchoyo wa ladha mpya kwa mashabiki wake kilikuwa cha neema kwa Rihanna na ndicho alichotangazwa na Forbes kufikia hadhi ya ubilionea na hadi sasa yupo hapo ‘akilipambania kombe’.

Utajiri wake

Mnamo Agosti 2021 utajiri wake ulikadiriwa na Forbes kufikia Dola1. 7 bilioni na kumfanya kuwa mwanamuziki wa kike tajiri zaidi duniani na wa pili baada ya Oprah Winfrey kama mburudishaji.

Hata hivyo, sio muziki pekee uliompatia utajiri huo, bali chapa yake ya vipodozi, Fenty Beauty anayoimiliki kwa asilimia 50 kwa kushirikiana na LVMH na pia chapa yake ya nguo za ndani, Savage X Fenty anayoimiliki kwa asilimia 28.

Lakini kufikia Oktoba 2024 ambapo utajiri wa Rihanna ulikuwa ameshuka hadi Dola1.4 bilioni, akashushwa hadi nafasi ya tatu na Taylor Swift aliyefikisha utajiri wa Dola1.6 bilioni huku Jay Z akiendelea kuwa namba moja kwa utajiri wa Dola2.5 bilioni.

Ikumbukwe Taylor Swift, mkali wa kibao, Blank Space (2014) ndiye msanii wa kwanza kuwa bilionea duniani kutokana na muziki pekee na alitangazwa kuwa bilionea baada ya mafanikio makubwa ya ziara yake, Taylor Swift: The Eras Tour.

Familia sasa

Baada ya muziki kumpatia umaarufu na utajiri mkubwa, Rihanna aliamua kuazisha familia na mpenzi wake Asap Rocky ambaye tayari wamejaliwa kupata watoto wawili na wote wa kiume. Kuna RZA aliyezaliwa Mei 2022 na Riot aliyezaliwa Agosti 2023. 

Katika mahojiano na Interview Magazine Aprili 2024, wawili hao walieleza mambo mengi kuhusu malezi na familia, huku Rihanna akisema kiu yake ni kupata mtoto wa kike.

“Sijui Mungu anataka nini, lakini ningependa kuwa na watoto zaidi ya wawili. Nijaribu kupata msichana wangu, lakini bila shaka akiwa ni mvulana mwingine, basi ni mvulana wangu mwingine,” alisema Rihanna, mshindi wa Grammy mara tisa.

Kauli ya Rihanna ilikuja baada ya awali Asap Rocky kuulizwa iwapo kuna wimbo wa ushirikiano kati yake na mama watoto wake watautoa na kusema ushirikiano pekee watakaofanya ni kuleta watoto duniani na sio muziki.

Ukaribu wao ulianza kuonekana katika tuzo za MTV VMAs 2012, baadaye Rihanna akaonekana katika video ya wimbo wa Asap Rocky, Fashion Killa (2013), kisha Desemba 2019 wakaibuka pamoja katika tuzo za British Fashion na tangu wakati huo wako wote.