Mamchester, England. Manchester United imeendelea kupata wakati mgumu mbele ya Arsenal baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya England uliochezwa kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Mara ya mwisho United kupata ushindi dhidi ya Arsenal ilikuwa Septemba 4, 2022 ambapo ilishinda mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Katika michezo mitano iliyopita ya Ligi Kuu England, Arsenal imeshinda mechi nne huku United ikitoa sare mechi moja.

Baada ya kufunga bao dhidi ya Arsenal, nyota wa United Bruno Fernandes amehusika katika mabao 25 akifunga 12 na kutoa pasi 13 za mwisho msimu huu.
Declan Rice alifunga bao la kusawazisha katika dakika ya 74 huku golikipa wa Arsenal, David Raya akiiokoa timu yake baada ya kupangua michomo mikali iliyokuwa ikipigwa na United mwishomi mwa mchezo.

United inashika nafasi ya 14 katika msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa na pointi 34 katika mechi 28 ilizocheza wakati Arsenal inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 55.
Liverpool ndiyo inayoongoza Ligi kwa pointi 70 katika michezo 29 iliyocheza huku ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo mmoja peke
Katika michezo mingine iliochezwa jana ni pamoja na ule wa Chelsea dhidi ya Leicester City ambao ulimalizika kwa Chelsea kuchomoza na ushindi wa bao 1-0.
Bao pekee la Chelsea lilifungwa na Marc Cucurella katika dakika ya 60 ambaye aliachia shuti kali lililomshinda kipa wa Leicester, Mads Hermansen.

Katika mchezo huo ambao ulichezwa kwenye Uwanja wa Stanford Bridge ilishuhudiwa mshambuliaji wa Chelsea, Cole Palmer akikosa mkwaju wa penati kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na Chelsea.
Mchezo mwingine ulikuwa kati ya Tottenham dhidi ya Bournemouth ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Tottenham ndiyo ambayo ilitoka nyuma na kusawazisha baada ya kutanguliwa kwa mabao mawili ambayo yalifungwa na Marcus Tavernier katika dakika ya 42.
Huku bao lingine likifungwa na Evanilson katika dakika ya 65 kabla ya Pape Matar Sarr na Son Heung-min kuifungia Tottenham mabao ya kusawazisha.
Ligi Kuu ya England itaendelea tena leo ambapo West Ham United itakuwa nyumbani kuikaribisha Newcastle United saa 5:00 usiku.