Ricardo Momo atia neno ishu ya D Voice kumuibia wimbo Meja Kunta 

Ricardo Momo atia neno ishu ya D Voice kumuibia wimbo Meja Kunta 

Dar es Salaam. Meneja na msemaji wa wasanii wa Lebo ya WCB, Mohamed Salum ‘Ricardo Momo’ amezungumzia sakata la mwanamuziki wa singeli Meja Kunta kudai kuvujishiwa wimbo D Voice na kumpatia Jux.

Akizungumza na Mwananchi, Momo amesema D Voice siyo msanii wa kwanza kulalamikiwa kufanya hivyo.

“Kuna vitu vingine inakuwa ni makubaliano kati ya msanii na msanii. Mara nyingi sisi tupo huru sana na wasanii wetu kwenye kufanya kazi. Msanii anaruhusiwa kufanya kazi na mtu yeyote anayemtaka. 

“Kwa hiyo msanii kulalamika ni kitu cha msingi na tunaangalia ulalamikaji wake unaathari kiasi gani. Ni vitu vya kawaida kwa msanii kulalamikiwa masuala ya nyimbo kwa sababu hakuanza D Voice wasanii wengi wakubwa katika nchi wamewahi kulalamikiwa kukopi ama kuiba nyimbo za watu,”amesema Momo.

Amesema hiyo ndiyo biashara kwa hiyo hakuna hatua yoyote waliyoichukua dhidi ya malalamiko ya Meja Kunta.

“Kuna vitu vina nguvu zaidi. Haya mambo yangekuwa menejimenti imeshirikishwa kabla ya kupeana huo wimbo au wanaandikiana kungekuwa na mikataba. Lakini ni jambo ambalo limeonekana la msanii kwa msanii. Kwa hiyo wanatakiwa kuvimaliza wenyewe kwa wenyewe. 

“Cha muhimu ni kufanya kazi, Meja Kunta anapokuwa na wimbo wake anaamini una mada nzuri basi ahakikishe anautoa kwa nyakati sahihi. 
Asisubiri kupata komenti kwa wasanii wengine. Mara nyingi mtu anamsikilizisha mwenziye wimbo ambao unakaribia kutoka asichukue muda kutoa wimbo ambao amemsikilizisha msanii mwengine,” amemalizia Momo.

Ikumbukwe kupitia ukurasa wa Instagram wa Meja Kunta amemlalamikia D Voice kwa kukopi wimbo wake na kumpatia Jux. Katika malalamiko hayo Meja ameambatanisha wimbo waliofanya awali na mpya aliofanya Jux ambao D Voice anatuhumiwa kupatia msanii huyo.

“D Voice inawezekana kwenye hii game nikawa mtu wa kwanza mwenye ukaribu na wewe kutokana na ukaribu wa familia zetu. Inawezekana nikawa ndiye mtu niliyekufungulia milango mingi kwenye maisha yako tulipofanya wimbo wa pamoja ulifanya vizuri sana.

“Hii inaonesha kiasi gani wewe ni mdogo wangu wa rohoni kabisa nina mapenzi makubwa na wewe. Ila hiki unachofanya kina tafsiri mbili, dharau, kunitumia. Tunawasiliana kila siku tunakutana kila siku sidhani kama natakiwa kulipwa hiki,” ameandika Meja.

Hata hivyo, Mwananchi imefanya juhudi za kumtafuta D Voice na Jux bila mafanikio. Juhudi hizo zinaendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *