Rekodi zinazotikisa Ligi Kuu

Dar es Salaam. Ni weka niweke katika Ligi Kuu Bara baada ya kubakisha michezo 10 hadi tisa kwa baadhi ya timu kumalizika kwa msimu huu, huku ushindani ukitikisa kwa vigogo wanaowania ubingwa, nafasi nne za juu na kupigania kutoshuka daraja.

Wakati ligi hiyo inayoshika nafasi ya nne kwa ubora Afrika ikiendelea kutikisa na kuteka hisia za mashabiki na wadau wa soka nchini, zipo rekodi mbalimbali zilizojitokeza kuanzia timu zenyewe na hata wachezaji binafsi kama zinavyoelezewa.

CAMARA AFUKUZIA REKODI

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Kipa wa Simba, Moussa Camara amebakisha mchezo mmoja tu kati ya 11 iliyobaki ya kikosi hicho katika Ligi Kuu Bara ili avunje rekodi ya ‘Clean Sheets’, iliyokuwa inashikiliwa msimu uliopita na aliyekuwa nyota wa Coastal Union, Ley Matampi.

Camara amejiunga na Simba msimu huu akitokea Horoya AC ya kwao Guinea, amefikisha ‘Clean Sheets’ 15 sawa na alizoziweka Matampi msimu uliopita, wakati alipojiunga na Coastal Union akitokea Jeunesse Sportive Groupe Bazano ya kwao DR Congo.

Makipa wengine wanaofuatia kwa ‘Clean Sheets’ nyingi msimu huu ni Patrick Munthary wa Mashujaa mwenye 10, Djigui Diarra (Yanga) na Mohamed Mustafa (Azam FC) wenye tisa, huku Yona Amosi (Pamba Jiji) na Yacoub Suleiman Ali (JKT TZ) wakiwa nazo nane.

REKODI YA PENALTI YAVUNJWA

New Content Item (3)
New Content Item (3)

Msimu huu pekee tumeshuhudia zikitokea jumla ya penalti 59, ambapo kati ya hizo zimefungwa 48 na kukoswa 12, ikivuka ile ya msimu wa 2023-2024, ambao penalti 46, zilipigwa, huku katika hizo zilifungwa 35, wakati zile zilizokoswa zilikuwa 11.

Pia rekodi ya penalti msimu huu imeivuka ya msimu wa 2022-2023, ambao jumla ya penalti 57, zilipigwa na kati ya hizo 40, ziliwekwa kimiani na 17, zilikoswa, huku kwa msimu wa 2021-2022 zilipatikana 50 na 32, zilifungwa wakati 18, zilikoswa.

Katika penalti za msimu huu, Simba ndio timu pekee iliyopata nyingi hadi sasa 10, zilizopigwa na mastaa wawili, ambao ni Jean Charles Ahoua na Leonel Ateba waliopiga tano kila mmoja wao, huku kati ya hizo wakikosa moja tu kikosini.

Watani zao wa jadi Yanga, inafuatia kwa kupata penalti nyingi ambapo hadi sasa imepata saba na kati ya hizo imekosa tu mbili ambazo zote ni za kiungo mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Stephane Aziz KI, huku nne alizopiga akiweka kambani.

KMC FC na Pamba Jiji ndio timu mbili pekee kati ya 16, zinazoshiriki Ligi Kuu msimu huu ambazo hazijapata penalti hadi sasa.

ABALKASSIMU KIBOKO

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Wakati zikitolewa kadi nyekundu 18 hadi sasa tofauti ya tatu tu na zile ya msimu uliopita wa 2023-2024, zilipotolewa 21, mshambuliaji wa Pamba Jiji, Abalkassim Suleiman ndiye anayeongoza ambapo ameonyeshwa mbili akizichezea timu mbili tofauti.

Abalkassim alionyeshwa kadi nyekundu akiichezea Fountain Gate ambao timu hiyo ilikubali kichapo cha mabao 3-1, dhidi ya Pamba Jiji Novemba 5, mwaka jana, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, uliopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Babati.

Baada ya hapo, nyota huyo akajiunga na Pamba Jiji dirisha dogo la Januari mwaka huu na kushuhudia tena akionyeshwa kadi nyekundu, wakati kikosi hicho cha jijini Mwanza kilipochapwa mabao 2-0, ugenini mbele ya Mashujaa FC Februari 19, 2025.

Mbali na Abalkassim, nyota wengine walioonyeshwa kadi nyekundu msimu huu ni Cheikh Sidibe (Azam FC), Saleh Masoud, Eric Okutu (Pamba FC), Victor Sochima (Tabora United), Ibrahim Elias, Ismail Mpank (KMC), Denis Richard, Mohamed Bakari (JKT TZ).

Wengine ni Joseph Mahundi (Kagera Sugar), Masoud Abdallah ‘Cabaye’, Zawadi Mauya, Ramadhan Chobwedo (KenGold), Ibrahim Hamad ‘Bacca’ (Yanga), Meshack Abraham (TZ Prisons), John Noble (Fountain Gate) na Derrick Mukombozi wa Namungo FC.

MASEKE MZEE WA KUJIFUNGA

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Kipa wa KMC, Wilbod Maseke ameendeleza rekodi mbaya katika Ligi Kuu baada ya kushuhudia nyota huyo akijifunga bao, ikiwa ni msimu wa pili mfululizo, wakati timu hiyo ya Kinondoni ilipochapwa mabao 2-0, dhidi JKT Tanzania Februari 18, 2025.

Katika pambano hilo lililopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, kipa huyo alijifunga dakika ya 68 na kuizawadia JKT bao la pili baada ya Hassan Nassor ‘Machezo’ kufunga kwa kichwa akimalizia mpira wa friikii uliopigwa na Najim Magulu dakika ya 10.

Maseke anakuwa kipa wa tatu msimu huu kujifunga kati ya 11 baada ya Daniel Mgore wa Dodoma Jiji na Mohamed Mustafa wa Azam FC, huku wengine waliojifunga ni Fredy Tangalo (KMC), Kelvin Kijili (Simba) na Jackson Shiga wa (Fountain Gate).

Wengine ni Dickson Mhilu (Dodoma Jiji), Lameck Lawi (Coastal Union) Yannick Bangala (Azam FC), Ladack Chasambi (Simba) na Emmanuel Chigozie wa Tabora United na kufikisha 11, ikibaki mmoja kuifikia rekodi ya msimu uliopita walipojifunga 12.

Jambo usilolijua ni kwamba huu ni msimu wa pili mfululizo kwa Maseke kujifunga bao, kwani msimu uliopita alikuwa kipa wa tatu kati ya 12 waliojifunga katika mchezo ambao KMC ilitoka sare ya bao 1-1, dhidi ya Tanzania Prisons, Oktoba 27, 2023.

Msimu huo, Maseke alikuwa ni kipa wa pili kujifunga baada ya Mohamed Makaka wa Mtibwa Sugar aliyejifunga wakati timu hiyo iliposhinda mabao 3-1, dhidi ya Geita Gold, Oktoba 26, 2023, huku timu hizo zote mbili zikishuka daraja msimu uliopita.

KENGOLD YAPATA MATUMAINI

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Sare ya bao 1-1, iliyoipata KenGold dhidi ya Tabora United Februari 14, imeifanya timu hiyo ya Mbeya kuandika rekodi ya kupata pointi kwa mara ya kwanza msimu huu, kwani kabla ya hapo ilikuwa haijashinda wala kutoka sare yoyote ugenini.

Katika mchezo huo ambao KenGold ilitangulia kupata bao la mkwaju wa penalti kupitia kwa Selemani Bwenzi dakika ya 25, kisha Heritier Makambo kuisawazishia Tabora dakika ya 87, uliifanya kuvuna pointi moja ugenini kwa mara yake ya kwanza.

Kikosi hicho kilichopanda Ligi Kuu Bara msimu huu, mchezo wake na Tabora ulikuwa wa 11, kucheza ugenini ambapo kati ya hiyo imetoka sare mmoja na kupoteza 10, ambapo kiujumla imefunga mabao matano na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 25.

KenGold ilianza msimu huu na Kocha, Fikirini Elias aliyekiongoza katika jumla ya michezo mitatu na kuchapwa yote kisha Septemba 17, mwaka jana akaamua kujiweka pembeni mwenyewe, kwa kile alichokieleza kufikia makubaliano ya pande mbili.

Baada ya hapo ikaongozwa na Jumanne Challe aliyeipandisha Ligi Kuu Bara kama kocha wa muda kutokana na kutokidhi vigezo vya kusimamia benchi la ufundi, ambapo alisimamia michezo mitano, akishinda mmoja tu, sare mmoja pia na kupoteza mitatu.

Oktoba 22, 2024, uongozi wa KenGold ukamtangaza, Omary Kapilima kuiongoza timu hiyo ambapo hadi sasa ameisimamia katika jumla ya michezo yake 12, ya Ligi Kuu Bara na kati ya hiyo ameshinda miwili tu, sare mitatu na kuchapwa saba hadi sasa.

Kapilima ameendelea kuiongoza timu hiyo licha ya Januari 18, mwaka huu, uongozi wa timu hiyo kumtangaza Kocha, Vladislav Heric raia wa Serbia, ambaye hadi sasa bado hajapata vibali vya kufanya kazi hapa nchini tangu atue kwenye kikosi hicho.

Heric aliyezaliwa Agosti 29, 1966, amezifundisha timu za Club Africain ya Tunisia, Maritzburg United, Polokwane City, FC Cape Town na Chippa United za Afrika Kusini, huku akikabiliwa na kazi kubwa ya kukinusuru kikosi hicho kisishuke daraja.

Heric ambaye ni mzoefu wa Mpira wa Miguu aliacha kucheza soka la ushindani akiwa na umri wa miaka 21, baada ya kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara, jambo lililomfanya kujikita katika kusomea ukocha kufuatia ndoto zake kufifia mapema tu.

FOUNTAIN GATE HAKIJAELEWEKA

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Baada ya mchezo wa juzi wa Fountain Gate dhidi ya Dodoma Jiji ugenini, kikosi hicho ndio pekee ambacho hakijaonja ladha ya ushindi tangu mwaka 2025 uingie, ambapo imecheza michezo minane ya Ligi Kuu, ikipoteza sita na kutoka sare miwili tu.

Kikosi hicho kinachonolewa wa Mkenya Roberto Matano aliyechukua nafasi ya Mohamed Muya aliyetimuliwa Desemba 29, mwaka jana, mara ya mwisho kushinda ilikuwa ni ushindi wa mabao 3-2, nyumbani dhidi ya Coastal Union, Desemba 13, mwaka jana.

Katika michezo hiyo nane, Fountain Gate imepoteza sita na kutoka sare miwili tu, ambapo safu ya ushambuliaji imefunga mabao mawili tu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 15, ikiwa ni wastani wa kuruhusu mabao mawili kwa kila mechi yake.