Yanga inaingia Uwanja wa Mkapa leo kuvaana na Al Hilal ya Sudan, huku ikiwa na rekodi bora zaidi kwenye michezo ya nyumbani.
Huu utakuwa mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi,katika michezo 17 ya kimataifa ambayo Yanga imecheza nyumbani, imeshinda 12, imepoteza miwili na kutoka sare mitatu, ikiwe ni rekodi ambayo inatakiwa kuiendelea Kwa Mkapa.
Huu ni mchezo wa kwanza wa Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic ambaye tayari amepiga mkwara mzito akisema kwamba kwenye timu yake hataki kuona mpinzani anapumua.
Wakati akitoa mkwara huo, mtihani wake wa kwanza ni leo mbele ya Al Hilal ya Sudan katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika Kundi A utakaopigwa kuanzia saa 10:00 jioni.
Yanga inakwenda kucheza dhidi ya Al Hilal ambayo inafundishwa na Kocha Florent Ibenge ambaye si mgeni katika ardhi ya Tanzania.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Oktoba 8, 2022 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ukiwa ni mchezo wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika kuwania kufuzu makundi uliomalizika kwa sare ya 1-1, ugenini Yanga ikaenda kufungwa 1-0, ikatolewa na kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ilikwenda hadi fainali na kupoteza kwa sheria ya bao la ugenini mbele ya USM Alger, wakati huo ikifundishwa na Nasreddine Nabi.
Ibenge raia wa DR Congo, amewahi kuja nchini Tanzania mara nne akiwa na timu tofauti kucheza mechi za kimataifa zinazosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) lakini kwa bahati mbaya hajaambulia ushindi zaidi ya sare moja na kupoteza tatu.
Katika mechi nne alizokuja akiwa na timu za AS Vita Club (2018-2019 na 2020-2021), kisha 2021-2022 akiiongoza RS Berkane zote alipoteza akicheza dhidi ya Simba, huku 2022-2023 akiwa na Al Hilal alipata sare ya 1-1 dhidi ya Yanga.
Huu ni mtihani wa kwanza kwa Kocha Ramovic tangu akabidhiwe kikosi hicho Novemba 15 mwaka huu akichukua nafasi ya Miguel Gamondi ambaye msimu uliopita aliiwezesha Yanga kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya kupita takribani miaka 25, kisha akaipeleka hadi robo fainali.
Msimu huu kabla Gamondi hajaondoka, ameiwezesha Yanga kutinga tena makundi kwa msimu wa pili mfululizo akiwa kocha wa kwanza kufanya hivyo kikosini hapo, hivyo Ramovic ana kazi ya kufanya kuendeleza rekodi hizo.

Yanga inatakiwa kuwa makini…
Ramovic mbali ya kwamba huu ni mtihani wake wa kwanza katika kuiongoza Yanga, pia ni mgeni katika michuano ya Caf kulinganisha na Ibenge. Rekodi zinaonyesha kwamba, Ramovic raia wa Ujerumani, hii ni mara ya kwanza kuiongoza timu katika michuano hiyo.
Kocha huyo anaiongoza Yanga ambayo imekuwa na rekodi nzuri katika michuano ya Caf inapocheza nyumbani kwani imepoteza michezo miwili tu ukiwemo mmoja wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger ya Algeria katika kipindi cha kuanzia msimu wa 2021–2022 hadi sasa 2024-2025.
Msimu wa 2021–2022, Yanga ilipoteza nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya Rivers ya Nigeria katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kisha haijapoteza tena hadi kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kuanzia msimu wa 2021-2022 hadi sasa 2024-205, Yanga imecheza nyumbani mechi 17 za Caf, imeshinda 12, sare 3 na kupoteza 2, ikifunga mabao 42 na kuruhusu 6.

Hata hivyo, mchezo huu hautokuwa rahisi kwa Yanga kwani Al Hilal ina rekodi nzuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo imecheza fainali mbili za mwaka 1987 na 1992, huku ikifika pia nusu fainali mara tano kuanzia mwaka 1966, 2007, 2009, 2011 na 2015.
Pia imecheza robo fainali mbili, mwaka 1988 na 1990 na kushiriki hatua ya makundi mara nane ikianza mwaka 2008, 2014, 2017, 2019-2020, 2020-2021, 2021-2022, 2022-2023 na 2024-2025 wakati Yanga ikitinga makundi mara tatu 1998, 2023-2024 na 2024-2025.
Rekodi za Chama kiboko
Msimu huu Yanga imetinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kushinda mechi zote nne za mtoano ikifunga jumla ya mabao 17 huku yenyewe ikiwa haijaruhusu nyavu zake kuguswa.
Yanga ilianza kwa kuiondosha Vital’O ya Burundi kwa jumla ya mabao 10-0, kisha ikaichapa CBE SA ya Ethiopia jumla ya mabao 7-0.
Al Hilal yenyewe ilianza kuifunga Al Ahly Benghazi ya Libya jumla ya mabao 2-1, baadaye ikaitupa nje San Pedro ya Ivory Coast kwa jumla ya mabao 3-2.
Wakati Yanga ikifunga mabao 17, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Clatous Chama amehusika kwenye mabao manane, akimfunika Stephane Aziz Ki ambaye amehusika kwenye mabao matano akifunga manne na asisti moja.
Chama kwenye mabao manane aliyohusika nayo, amefunga matatu na kutoa asisti tano ambapo katika ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Vital’O alifunga bao moja na kutoa asisti nne, hivyo alihusika kwenye mabao matano kati ya sita.
Mchezo uliofuata Yanga wakiibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Vital’O, Chama alifunga bao moja ambalo lilikuwa la mpira wa kutenga, kisha akafunga tena dhidi ya CBE SA wakati Yanga ikishinda 6-0 nyumbani ambapo pia alitoa asisti.
WAPINZANI WENGINE
Mbali na timu hizo, Kundi A la Ligi ya Mabingwa kuna TP Mazembe ya DR Congo na MC Alger ya Algeria.
Makocha wanasemaje…
Akizungumzia mchezo wao dhidi ya Yanga, Ibenge amesema: “Yanga ya sasa na tuliyokutana nayo mara ya mwisho ni vitu viwili tofauti kwa sababu imebadilika kiuchezaji na inajua namna mashabiki na viongozi wao wanataka kutokana na malengo yao, itakuwa mechi nzuri na ya kusisimua kwa pande zote.”
Kwa upande wa Ramovic, amesema: “Yanga ni timu bora sana, lakini tunakwenda kucheza na timu bora pia hivyo tunahitajika tuwe makini sana. Tunapaswa kuwa na utayari kiakili na kisaikolojia kwani tunakwenda kwenye mechi ngumu sana. Hata hivyo ninayo furaha kubwa sana kuiongoza klabu kubwa kwenye mashindano makubwa.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kwenye Ligi ya Mabingwa. Ni jambo la kheri sana kwangu kushiriki mashindano haya nikiwa na timu kubwa kama Yanga. Falsafa yangu kubwa ni nidhamu na kujituma. Napenda kuona wachezaji wakicheza kama timu. Haijalishi unatumia mfumo gani kama wachezaji wako hawana umoja ni ngumu kupata matokeo.
“Sina presha yoyote kutokana na matokeo ya awali. Mipango yangu ni kutazama kilichopo mbele yetu. Nimekuja Yanga kushinda mataji, ndio mpango wangu wa kwanza. Nafahamu klabu hii ni kubwa uwezo wa kubeba makombe kwahiyo nina matumaini hilo linawezekana.”
Mwamuzi kutoka Morocco, Samir Guezzaz ndiye atakayechezesha mchezo wa leo huku rekodi zikionyesha timu za nyumbani zimekuwa na matokeo mazuri tofauti na za ugenini jambo linaloweza kuipa faida zaidi Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Samir amechezesha michezo 11 ya kimataifa ambapo kati ya hiyo timu za nyumbani zimeshinda minane, sare miwili huku zile za ugenini zikishinda mechi moja tu, na kati yake ametoa jumla ya kadi 40, za njano zikiwa 39 na nyekundu ikiwa moja tu.
Kama haitoshi, mwamuzi huyo amekuwa na bahati mbaya anaposimamia mchezo wa Al Hilal kwani timu hiyo kutoka Sudan imekuwa ikipata wakati mgumu wa kushinda ambapo ameweza kusimamia michezo minne na yote imeshindwa kupata matokeo ya ushindi.
Mchezo wa kwanza kuisimamia Al Hilal alikuwa ni mwamuzi wa akiba ‘Fourth Official’ ambapo kikosi hicho kilichapwa mabao 3-1, dhidi ya Etoile du Sahel ya Tunisia, katika mchezo wa robo fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika Aprili 7, 2019.
Samir akaichezesha tena Al Hilal ilipotoka suluhu na TP Mazembe ya DR Congo katika mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika Februari 24, 2021.
Baada ya hapo akasimamia tena timu hiyo katika raundi ya pili ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa ni mwamuzi wa akiba ‘Fourth Official’, ambapo Al Hilal ilitoka sare ya kufungana bao 1-1, dhidi ya Rivers United ya Nigeria Oktoba 17, 2021.
Mchezo wa mwisho kuichezesha Al Hilal ulikuwa wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kati ya timu hiyo dhidi ya Petro Atletico ya Angola ambapo kikosi hicho cha Sudan kilichapwa bao 1-0, mechi iliyopigwa Novemba 25, 2023.
AUCHO, MZIZE HATIHATI
Daktari wa Yanga, Moses Etutu amethibitisha kuwa mastaa wa Yanga, Shadrack Boka, Khalid Aucho, Clement Mzize na Aziz Andabwile wapo nje ya uwanja wanauguza majeraha yao.
Akizungumza na Mwananchi, Etutu alisema Mzize na Aucho ni majeruhi wapya ambao wameongeza idadi sasa kufikia nne huku akiweka wazi kuwa wachezaji hao waliumia wakiwa na timu zao za taifa.
“Aucho aliumia akiwa na timu yake ya taifa Uganda na Mzize aliumia akiwa na Taifa Stars baada ya kurejea kambini tumewafanyia vipimo taarifa ya nini shida zao tutazitoa hivi karibuni,” alisema na kuongeza.
“Kuhusiana na Boka na Andabwile kama taarifa ilivyotolewa awali kuwa wataendelea kuwa nje hadi hapo hali zao zitakapotengamaa na maendeleo yao sio mabaya.
“Ukiachana na hao, wachezaji wengine wote wapo kwenye hali nzuri, kilichobaki ni kupambania pointi tatu muhimu kwenye uwanja wetu wa nyumbani.”
17 ZA YANGA NYUMBANI CAF
Yanga 0-1 Rivers
Yanga 5-0 Zalan
Yanga 1-0 Al Hilal
Yanga 3-1 TP Mazembe
Yanga 2-0 Real Bamako
Yanga 2-0 US Monastir
Yanga 0-0 Rivers United
Yanga 2-0 Marumo Gallants
Yanga 1-2 USM Alger
Yanga 5-1 Djibouti Telecom
Yanga 1-0 Al Merrikh
Yanga 4-0 CR Belouizdad
Yanga 3-0 Medeama
Yanga 1-1 Al Ahly
Yanga 0-0 Mamelodi Sundowns
Yanga 6-0 Vital’O
Yanga 6-0 CBE