
Mwaka 2025 katika mchezo wa ngumi za kulipwa umeanza kwa moto wa kutosha kwa mabondia wa mchezo huo kutokana na kuendelea kuvunja rekodi katika orodha ya viwango vya mabondia bora wa Tanzania yaani ‘Pound For Pound’.
Katika orodha hiyo ya mtandao wa Boxrec ambao umekuwa ukitumika duniani kote kuhifadhi taarifa za mabondia umetoa orodha ya viwango vipya vya mabondia nchini kutoka makundi yote ya uzito na rekodi zao zilivyoweza kusimima katika mwezi huu wa Februari.
Utamu wa orodha hiyo umeonyesha mabadiliko ya kiushindini kwa mabondia wakali watano ambao wote wapo kwenye tano bora ya mabondia bora wa Tanzania kutokana rekodi walizoweka na kuvunja kutokana na matukio yao yaliopita.
Mwananchi inakuchambulia namna mabondia hao walivyoweza kuvunja rekodi pamoja na kuweza kuendelea kubadilisha nafasi katika tano bora hiyo.
Fadhili Majiha
Fadhili Majiha ‘kiepe Nyani’ ameendelea kubakia kuwq Tanzania One kwa mabondia wote yaani namba moja kwa zaidi ya mwaka kutoka na rekodi yake ilivyo kwa sasa.
Bondia huyo kutokea mitaa ya Mburahati, amevunja rekodi ya kufikia hadhi ya nyota nne lakini akipanda katika viwango vya Baraza la Ngumi Duniani WBC kutokana na kushikilia mkanda wa WBC Afrika.
Majiha mwenye rekodi ya kucheza pambano 52, amefanikiwa kushinda 34 kati ya hayo 15 kwa Knockout na amepigwa mara 14 kati hizo tatu kwa Knockout lakini ametoka sare mara nne.
Bondia huyo amekuwa Mtanzania wa kwanza jina lake kuorodheshwa katika mabondia kumi bora duniani wa uzani wa super Bantam wanaotambuliwa na baraza hilo akishika nafasi ya kumi.
Bondia huyo aliingia kwa mara ya kwanza mwaka jana kwa kushika nafasi ya kumi kabla ya kupanda hadi nafasi ya kumi.
Ibrahim Class
Ushindi wa Knockout alioupata mwaka jana dhidi ya Simpiwe Vyteka, umepelekea kuendelea kubakia katika nafasi ya pili kwa kutetea mkanda wake wa TPBRC Taifa.
Class ambaye kwa sasa amefikisha hadhi ya nyota nne kwenye nafasi ya pili, akizidiwa pointi na Majiha, amecheza jumla ya mapambano 39, amefanikiwa kushinda 33 kati ya hayo 16 ni kwa Knockout na amepigwa mara sita kati ya hizo tatu kwa Knockout.
Salmin Kassim
Salmin Kassim ‘Mizinga’ bondia chipukizi wa Mafia Boxing Promotion anayekuja juu kwa kasi kwenye mchezo huo, amevunja rekodi ya katika orodha hiyo ya viwango kutoka na kumshusha bingwa wa WBO Africa, Hassan Mwakinyo kutoka nafasi ya tatu hadi ya nne, mwezi uliopita.
Mizinga amepanda kwenye nafasi hiyo kutoka nafasi ya sita mwaka jana ambaye kwa sasa anashikilia ubingwa wa mabara wa WBF akiwa na rekodi ya kucheza mapambano tisa, akishinda saba kati ya hayo manne kwa Knockout.
Bondia huyo hajawahi kupigwa zaidi ya kutoka sare mapambano mawili peke huku akiwa na hadhi ya nyota tatu na nusu katika nafasi ya tatu nchi nzima.
Ibrahim Mafia
Bingwa wa WBC Afrika akiwa bondia wa pili Tanzania kushikilia mkanda wa WBC Afrika, Ibrahim Mafia ‘Mafia Tank’.
Mafia Tank amekuwa na vita ya nafasi na bingwa wa WBO Afrika, Hassan Mwakinyo kutokana na mwezi uliopita, Mwakinyo kushika nafasi ya nne kabla mwezi huu kushushwa na Mafia hadi nafasi ya tano.
Bondia huyo mwenye rekodi ya kucheza mapambano 13 akifanikiwa kushinda 12 kati ya hayo nane ni kwa Knockout huku akiwa ametoka sare mara moja na akizimiliki nyota tatu na nusu.
Mafia Tank amevunja rekodi nyengine ya kuwa Mtanzania wa pili kutambuliwa na Baraza la Ngumi Duniani WBC baada ya Fadhili Majiha, Mafia kwenye orodha ya viwango hivyo akamata nafasi ya 17 kwa sasa huku nchini akiwa kwenye nafasi ya nne.
Hassan Mwakinyo
Bingwa wa WBO Afrika, Hassan Mwakinyo ‘Champez’ ameshuka nafasi moja kutoka nafasi ya nne mwezi uliopita hadi ya tano katika orodha ya mabondia bora wa Tanzania waliopo kwenye tano bora.
Mwakinyo ambaye kwa sasa anashikilia rekodi ya kucheza mapambano 27 akiwa ameshinda 24 kati ya hayo 17 ni kwa Knockout huku akiwa amepigwa mara tatu.
Bondia huyo aliyewahi kuwa Tanzania, amefikisha hadhi ya nyota tatu na nusu sawa na Salmini Mizinga na Ibrahim Mafia wakiwa na utofauti wa pointi amekuwa Mtanzania wa kwanza kutambuliwa na Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Duniani, WBO ambapo mwaka jana aliingia kwenye 15 bora ya mabondia hao.
Lakini katikati ya mwaka jana Mwakinyo alipanda hadi nafasi ya 13 kabla ya kushuka hadi nafasi ya 14 na sasa amerejea kwenye nafasi yake 15 ambayo aliingia nayo awali.