Refa England aweka rekodi mechi ya Man United, Chelsea

Manchester, England. Robert Jones ni refa wa Ligi Kuu ya England maarufu kama ‘EPL’ ambaye ameingia kwenye historia ya kuchezesha moja kati ya michezo mikubwa nchini humo ambapo jana alichezesha mchezo kati ya Manchester United dhidi ya Chelsea ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo.

Robert Jones ameingia kwenye historia hiyo baada ya kuchezesha mechi ya wababe hao iliyomalizika kwa sare ya kufunganana bao 1-1.

Kabla ya mchezo wa jana Robert Jones aliwahi kuzichezesha timu hizo kwenye michezo tofauti ya Ligi Kuu England huku Manchester United ikionekana kushinda idadi kubwa ya mechi walizochezeshwa na refa huyo ambapo kati ya mechi tisa walizochezeshwa, walishinda mechi tano, wakatoa sare mechi tatu, na wakapoteza mechi moja.

Kwa upande wa Chelsea Robert Jones amewachezesha mechi nane, wakipata ushindi mechi tatu, sare mbili, na kupoteza mechi tatu.

Kwa upande wa kadi Chelsea wana jumla ya kadi 13 za njano katika mechi nane walizochezeshwa na Robert Jones wakati hali ikiwa mbaya zaidi kwa Manchester United ambao wana jumla ya kadi 26 za njano katika mechi tisa walizochezeshwa ambapo hata kwenye mechi ya jana Man United ndiyo waliongoza kuonyeshwa kadi nyingi za njano wakilambwa sita huku Chelsea wakipata kadi mbili.