
MANCHESTER, ENGLAND. Michezo ya mtoano ya kuwania kufuzu kucheza hatua ya 16 bora inaendelea ambapo jana kulikuwa na mechi nne na iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu zaidi ni ile kati ya Real Madrid na Manchester City.
Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Etihad, mtetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid iliibuka na ushindi wa mabao 3-2.
Kwa mechi za jana, Madrid ilikuwa moja kati ya timu kubwa zilizofanikiwa kutanguliza mguu mmoja kwani mbali ya wao, pia PSG iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Brest, Juventus ikiwa nyumbani ikaichapa PSV mabao 2-1 na Borussia Dortmund ikaibamiza Sporting Lisbon mabao 3-0.
Katika mechi ya Real Madrid na Man City, wenyeji walipata mabao yote mawili kupitia kwa mshambuliaji wao nyota, Erling Haaland aliyefunga dakika ya 19 na 80 lililokuwa la penalti, huku ya wageni na washindi wa mchezo huo, yaliwekwa kimiani na Kylian Mbappe dk 60, Brahim Diaz dk 86 na lile la ushindi lilitupiwa kambani na Jude Bellingham dakika ya 90+2, huku pasi za mabao hayo mawili ya mwisho zikipigwa na Vinicius Junior.
Leo, pia kutakuwa na mechi nyingine nne za hatua hii lengo likiwa ni kutafuta timu nane zitakazokwenda kuungana na nane nyingine zilizofanikiwa kufuzu moja kwa moja kucheza 16 bora.
Baada ya jana, timu kubwa na zenye historia ya michuano hii karibia zote kuibuka na ushindi, leo itakuwa ni zamu ya vigogo wengine kuendeleza hilo ambapo AC Milan ambao ni mabingwa mara saba watakuwa ugenini kucheza na Feynoord ambayo imetoka kumfukuza kocha wao Brian Priske aliyechukua mikoba ya Arne Slot, mechi hii itapigwa kuanzia saa 5:00 usiku.
Vilevile Bayern Munich pia itakuwa kule Scottland kuvaana na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini humo katika mchezo ambao utaanza saa 5:00 usiku pia.
Upande mwingine watetezi wa Europa League, Atalanta ya Italia watakuwa ugenini huko Ubelgiji kucheza dhidi ya Club Brugge kuanzia saa 2:45 usiku na mechi nyingine itakuwa kati ya AS Monaco na Benfica. Mechi za mkondo wa pili zinatarajiwa kupigwa kati ya Februari 18 na 19.