Real Madrid bado kuna tatizo mahala

MADRID.  Licha ya kuwa na idadi kubwa ya wachezaji wenye majina makubwa akiwamo Kylian Mbappe iliyemsajili katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi, Real Madrid imekuwa katika panda shuka nyingi tangu kuanza kwa msimu huu, huku taarifa zikidai hakuna maelewano baina ya mastaa wa kikosi hicho.

Real Madrid ilikumbana na kichapo cha mabao 3-1 ikiwa nyumbani mbele ya AC Milan ukiwa ni mchezo wa pili mfululizo kupoteza baada ya kuchapwa 4-0 na watani zao, Barcelona katika mechi ya El Clasico.

Vilevile imepoteza mechi mbili kati ya nne katika michuano ya Ulaya ikiwa inashika nafasi ya 17 katika msimamo wa ligi hiyo.

Kwa upande wa La Liga, Madrid inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 24 nyuma ya Barcelona inayoongoza kwa tofauti ya pointi tisa. Inaelezwa moja ya sababu inayochangia matokeo yasiyoridhisha ya timu hiyo ni mpasuko baada ya Mbappe kutua.

Mbappe ambaye alitua Madrid akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na PSG, katika mechi sita za mwisho akiwa na timu hiyo amefunga bao moja pekee.

Karibu mechi zote kocha amekuwa akimchezesha kama mshambuliaji wa kati – eneo ambalo kabla ya kuwasili kwake alikuwa akicheza Jude Bellingham.

Kitendo cha kutolewa eneo hilo na kupangwa Mbappe, staa Bellingham ambaye kwa sasa anacheza akitokea pembeni inadaiwa kumuumiza  na anaamini ndio sababu hafungi, kwani tangu kuanza kwa msimu huu hajafunga hata bao moja wakati msimu uliopita alicheza mechi 42, akafunga mabao 23 na kutoa asisti 13.

Uwepo wa Mbappe pia umechangia kusogezwa nyuma kidogo kwa Vinicus ambaye msimu uliopita muda mwingi alikuwa akisimama mbele kama mshambuliaji namba 10, ambapo sasa anacheza nyuma ya Mbappe eneo ambalo halifurahii.

Wakati Mbappe anasajiliwa, moja ya maswali ilikuwa ni wapi atacheza, na Ancelotti alisema atatengeneza mfumo ambao utawafanya washambuliaji hao watatu wote wacheze kwa pamoja lakini mpango huo kwa sasa unaonekana kutompa matokeo mazuri.

Licha ya taarifa hizo zilizoandikwa katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwamo Daily Mail, Ancelotti amesisitiza hakuna mpasuko wowote katika timu na kila kitu kinakwenda vizuri katika chumba cha kubadilishia nguo.

“Hapana. Ndani ya chumba cha kubadilishia nguo kupo sawa. Kutakuwa na ukosoaji mwingi juu ya timu lakini ni lazima tukubali kwamba hatufanyi vizuri. Tunatakiwa kufanya vizuri zaidi. Kuna nyakati ngumu ambapo unapaswa kuhangaika kupigana, kufikiria nini cha kufanya kwa sababu timu haifanyi vizuri,” alisema Ancelloti baada ya kichapo cha AC Milan.

Madrid imeruhusu mabao tisa katika michezo mitatu iliyopita na Ancelotti anasisitiza wasiwasi wake mkubwa upo kwenye safu ya ulinzi. “Tulikuwa na nafasi nyingi za kufunga, lakini tatizo langu sio hilo. Shida kubwa tunayopaswa kuirekebisha ni jinsi wapinzani wetu wanavyotengeneza nafasi kwa urahisi. Tunapaswa kuwa na wasiwasi kwa sababu timu haichezi vizuri, lazima tuwe imara zaidi, tuwe na nguvu zaidi katika kujilinda. Tumefungwa mabao mengi.”

Timu hiyo ambayo ni bingwa mtetezi wa La Liga na Ligi ya Mabingwa itakutana na Osasuna katika La Liga, Jumamosi wiki hii mchezo ambao inatarajiwa kuutumia kurudisha morali baada ya kupokea vichapo katika mechi mbili zilizopita.