RCC Tanga yabariki mgawanyo majimbo matatu ya uchaguzi

Tanga. Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Tanga (RCC) imeidhinisha mapendekezo ya kugawa majimbo matatu ya uchaguzi ya Kilindi, Muheza, na Handeni Vijijini, kuwa na majimbo mawili kila moja katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, Jimbo la Kilindi litagawanywa na kuongeza Jimbo jipya la Songe.

Handeni Vijijini litakuwa na majimbo mawili, Handeni na Kabuku, huku Muheza ikipendekezwa kuwa na majimbo mawili ya Muheza Mjini na Muheza Vijijini.

Wakati wa kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika leo Jumatatu, Machi 24, 2025 chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian, wajumbe kwa pamoja walikubaliana kuhusu ugawaji wa majimbo husika.

Balozi Batilda alifafanua kuwa majimbo ya Kilindi na Handeni Vijijini yamekidhi vigezo vya ugawaji kutokana na idadi ya watu na mazingira yao. Hata hivyo, kwa upande wa Muheza, idadi ya watu bado haijafikia vigezo vya Tume ya Uchaguzi vinavyohitaji jimbo kuwa na angalau wakazi 400,000.

Kwa sasa, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza ina wakazi wapatao 250,000 na hata kwa makadirio ya ongezeko la watu, bado haifikii watu 300,000. Hivyo, kigezo kinachoweza kuzingatiwa ni idadi kubwa ya kata.

“Kamati ya Ushauri ya Mkoa imepitisha mapendekezo haya, lakini kipaumbele kipo kwa Kilindi kuwa na majimbo mawili, Kilindi, Songe na Handeni Vijijini kuwa na Jimbo la Kabuku. Kwa Muheza, tunaiweka kwa mashaka kwa sababu bado haijafikia idadi inayotakiwa,” amesema Balozi Batilda.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando amesema Jimbo la Handeni Vijijini lina eneo la kilomita za mraba 6,453, jambo ambalo linastahili kuzingatiwa katika ugawaji wa majimbo.

Na amesisisitiza kuwa ukubwa wa jimbo hilo umesababisha changamoto ya upatikanaji wa huduma, hivyo kuligawa kutasaidia kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Idrisa Mgaza akizungumza katika kikao hicho, amesema ongezeko la watu na uhamiaji kutoka Ngorongoro limeongeza mahitaji ya huduma na kwa sasa wilaya hiyo tayari imepokea zaidi ya kaya 100 huku nyumba 1,000 zikiendelea kujengwa.

Hivyo, amesisitiza kuwa kuongeza kata mpya ni hatua muhimu kwa utoaji wa huduma bora za kijamii.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Muheza, Erasto Mhina ametoa hoja ya kuangalia upya mgawanyo wa jimbo hilo kwa sababu lina kata 37 na madiwani 50, wakiwamo wa viti maalum.

Amesema kama majimbo mawili yataanzishwa, mzigo wa kuendesha halmashauri utapungua na ugawaji wa madiwani utawezesha ufanisi zaidi wa utawala.

Wiki iliyopita kikao cha DCC kilichoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Zainab Abdallah  kilijadili mgawanyo  wa maeneo mapya ya utawala kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Muheza yenye Jumla ya kata 37, kati ya hizo 17 ziunde Jimbo la Muheza Mjini na Kata 20 zilizosalia zitaunda Jimbo la Muheza Vijijini.

Pendekezo kwa jimbo la Muheza Mjini  lenye kata 17 litaundwa na Kata  Mbaramo, Tanganyika, Majengo, Genge, Masuguru, Kwemkabala, Kwakifua, Tingeni, Lusanga, Mpapayu, Kilulu, Kicheba, Magila, Mkuzi, Mlingano, Ngomeni na Kigombe.

Aidha, kwa upande wa jimbo la Muheza  Vijijini  litaundwa na Kata 20 za ambazo ni  Amani, Zirai, Mbomole, Kwezitu, Misalai, Kisiwani, Bwembwera, Makole, Kwafungo, Potwe, Songa, Tongwe, Mhamba, Nkumba, Mtindiro, Magoroto, Kwabada, Misozwe, Kwemingoji, na Kata ya PandeDarajani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *