Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema hakutoa amri ya kukamatwa makada 20 wa Chadema waliokwenda kuonana naye kupata mrejesho wa uchunguzi wa kupotea kwa Katibu wa Baraza la Vijana wa chama hicho (Bavicha), Amani Manengelo.
Makada hao wa Chadema wamekamatwa kwa muda leo Jumatano, Februari 26, 2025 saa tatu asubuhi wakati wakielekea katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa ahadi ya kukutana na RC Mtanda ili kupata mrejesho kuhusu kutoonekana kwa Manengelo kwa siku 13 sasa.
Walishikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Mwanza kisha wakaachiwa baada ya takribani saa moja na kukamilisha kikao chao na mkuu wa mkoa.
Mtanda amekiri alikuwa na ahadi ya kukutana na baadhi ya viongozi wa Chadema ambao walimuomba, lakini akiwa ofisini kwake alishangaa kuona taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa viongozi hao wamekamatwa na polisi, ndipo akamuuliza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (RPC) kujua nini kinaendelea.

Baadhi ya wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwa wameongozana na askari kwenda kituo kikuu cha Polisi jijini Mwanza kabla hawajaachiwa. Picha na Damian Masyenene
“Kama mimi mkuu wa mkoa mmeniomba appointment (miadi) nikakubali mje, nina haja gani ya kuwaambia polisi wawazuie, sina sababu ya kufanya hivyo, lakini pia nimeshawahi kuwaiteni hapa tukakaa tukazungumza juu ya tukio la Amani Manengelo, linafahamika na lilielezwa kwa kina siku ile, kwa hiyo hakuna sababu yoyote ya Serikali wala Mkuu wa Mkoa kumzuia mwananchi yoyote mkiwemo nyie viongozi wa Chadema, kuja kwenye ofisi za umma,” amesema Mtanda na kuongeza.
“Lakini suala la kuimarisha usalama katika muktadha wa namna hii ni suala la wajibu wa Jeshi la Polisi, lakini sasa pia siwezi kusemea kwa kina kuhusu polisi, kuna baadhi wamepigwa, mimi nimeongea na RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) na nikamwambia Chadema wana ahadi na mimi na hawatakiwi kuzuiliwa.”
“….na hatakiwi mwana Chadema yeyote kukamatwa anapokuja kumuona mkuu wa mkoa na ndiyo maana nikawaambia kama kuna mwana Chadema yuko polisi, wewe kazi yako kumwelekeza ofisi ya mkuu wa mkoa ilipo ni wapi na RPC amewaelekeza na mmekuja hapa na ninaamini hakuna mwana Chadema yeyote aliyewekwa ndani.
“Kama ilitokea wakati huo polisi wanawahoji, wanao wajibu wa kuwahoji ili kujua usalama na kujua kinachoendelea, lakini hawana haki ya kuwapiga kwa sababu hamkuwa na silaha ya aina yoyote na wala hatuna ugomvi. Chadema wana ugomvi gani na Serikali au na polisi? Chadema wanafuatilia tukio la kijana (Amani Manengelo) na sisi majibu tutawapa, mkija leo tutawapa, hata mkisema baada ya wiki moja au kesho, lakini itategemea tukio hili limefikia hatua gani,” amesema Mtanda.
Hata hivyo, Mtanda amesema Jeshi la Polisi lisingeweza kupuuzia tishio la uvunjifu wa amani, ambalo lingeweza kutokea baada ya chama hicho kusambaza barua za kuhamasisha viongozi na wanachama wao popote walipo, kwenda ofisi ya mkuu huyo wa mkoa.
“Katika barua yao moja, maneno yalisema ‘wanachama na viongozi wote wa Chadema kutoka mahali popote mlipo tukutane kwenye ofisi za mkuu wa mkoa, sisi au Jeshi la Polisi hatuwezi kujua ukubwa wa idadi ya wanachama wa Chadema ambao wangeitikia wito, Jeshi la Polisi linao wajibu wa kuimarisha usalama kwenye ofisi za umma, ikiwemo ofisi ya mkuu wa mkoa kwa sababu wasingetake for granted (wasingepuuzia) kwamba wanachama 8,000 au 4,000, hata 500 wakija hali ya usalama itakuwaje,” amesema Mtanda.
Akizungumzia ukamataji huo, Katibu wa Chadema Kanda ya Viktoria, Zakaria Obadi amelaani kitendo cha Jeshi la Polisi kutumia nguvu zisizo za lazima na kuwapiga wanachama wake baada ya kuwafikisha kituoni, licha ya kuonyesha baadhi ya meseji ambazo waliwasiliana na mkuu wa mkoa wa Mwanza akiwaruhusu kwenda kuonana naye.
Amesema alifika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa akiwa na makada wenzake pamoja na Babu yake Amani Manengelo na kaka yake ambao walihitaji kujua hatima ya ndugu yao lakini nao wakakamatwa bila kusikilizwa.

Baadhi ya wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwa wameongozana na askari kwenda kituo kikuu cha Polisi jijini Mwanza kabla hawajaachiwa. Picha na Damian Masyenene
“Tulipofika karibu na ofisi yako tukakutana na maofisa wa ulinzi tukawaeleza tunakwenda kuonana na mkuu wa mkoa hadi tukawaonyesha meseji tulizowasiliana jana na wewe (Mtanda), wakasema hauna appointment (miadi) na sisi, tukawasihi na kuwaomba wakupigie simu, baadaye tukakutana na magari ya polisi yakiongozwa na OCD wa Nyamagana, akasema hawa waende moja kwa moja Central (kituo kikuu),” amesema Obadi na kuongeza.
“Tulipofika kituoni hatukupewa nafasi ya kujieleza, tukaingizwa ndani tukatakiwa kuvua mikanda na kukabidhi mali zetu, tulipojaribu kuomba nyaraka za kusaini kukabidhi vitu vyetu, baadhi yetu wakapigwa na kuumizwa.
“Kwa kweli jeshi letu linatumia nguvu zisizo za lazima, sisi ni raia wa Tanzania tumekuja hapa kwa amani hatujabeba bango tumekuja kwa nia njema,” amesema.
Kikao kati ya RC Mtanda na viongozi wa Chadema Kanda ya Victoria kilichohudhuriwa pia na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Audax Majaliwa kimefanyika kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 7:20 mchana na kukubaliana kuaminiana na kushirikiana katika kumtafuta Manengelo.
Manengelo alipotea tangu Februari 14, 2025 wilayani Misungwi na Chadema wanadai alitekwa na maofisa wa polisi, lakini hadi sasa watu watatu wanashikiliwa kwa mahojiano, akiwemo mwanamke aliyetajwa kwa jina la Pendo ambaye alikuwa mtu wa mwisho kuonana naye.