Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera amesema tayari amelielekeza Jeshi la Polisi kuongeza jitihada za kuwatafuta wahusika waliomshambulia kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mdude Nyagali, huku akiahidi Sh5 milioni kwa atakayesaidia kumpata kada huyo alipo akiwa hai au amekufa.
Hata hivyo, amesema pamoja na yeye kutojua tukio hilo, kwakuwa limetokea mkoani kwake akiwa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ameamua kulifanyia kazi kuhakikisha haki inapatikana, huku akilaani na kusikitishwa na tukio hilo.
Mdude anadaiwa kuvamiwa na kupigwa nyumbani kwake jijini Mbeya Mei 2, 2025 na watu waliojitambulisha kuwa polisi, lakini bado haijafahamika hali ya kada huyo na wapi alipo, hivyo kuibua sintofahamu kwa wafuasi wa chama hicho.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera (wa pili kulia) akizungumza jambo alipokutana na viongozi wa Chadema Kanda ya Nyasa ofisini kwake kuelezea hatma ya kada wa Chama hicho, Mdude Nyagali anayedaiwa kuvamiwa na kupigwa nyumbani kwake jijini Mbeya Mei 2, 2025.
Akizungumza leo Jumatatu, Mei 5, 2025 baada ya viongozi wa Chadema mkoani humo na Kanda ya Nyasa kufika ofisini kwake kujua hatua zilizochukuliwa, Dk Homera amesema yupo pamoja na chama hicho kuhakikisha Mdude anapatikana.
Amesema hadi sasa tayari viongozi wa Serikali wapo kazini kufanya juhudi za kupatikana kwa Mdude na kuwasaka waliofanya tukio la kuwachukulia hatua wahusika, akieleza kuwa jambo hilo wanalichukulia kwa uzito kwani linatisha kutokana na damu zilizomwagika.
“Mimi naungana na nyinyi katika hili, wote tupo katika mazingira magumu, inatisha sana ile damu na hata hivyo binafsi sijui ilikuaje lakini nimeshaelekeza Jeshi la Polisi kuongeza juhudi kwenye tukio hili waliohusika wakamatwe na Mdude apatikane.
“Hili jambo linaniumiza naungana na ninyi tujue huyu mtu (Mdude) yuko wapi, viongozi wetu wa juu wameshaelekeza matukio yote yafuatiliwe ikiwamo hili la Mdude na yule Padri Kitima,” amesema Dk Homera.
Dk Homera ameeleza kwa kuwa tayari Jeshi la Polisi nchini limeshatoa maelekezo ikiwamo timu iliyoundwa kuchunguza tukio hilo, watakaobainika na kukiri kuhusika hatua zichukuliwe haraka.
“Kuna mtu anadaiwa kuposti mtandaoni akieleza kuwafahamu waliohusika tukio hilo, sasa kama kuna mtu anafahamu taarifa hizi aje hapa kwangu aniambie ili hatua zichukuliwe,” amesema Mkuu huyo wa Mkoa.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera (wa pili kulia) akizungumza jambo alipokutana na viongozi wa Chadema Kanda ya Nyasa ofisini kwake kuelezea hatma ya kada wa Chama hicho, Mdude Nyagali anayedaiwa kuvamiwa na kupigwa nyumbani kwake jijini Mbeya Mei 2, 2025.
Hata hivyo, amesema kufuatia matukio hayo, anatarajia kukutana na viongozi wa kimila kujadiliana namna ya kukabiliana na sintofahamu hiyo, huku akikiri kuwa hali hiyo inawatisha akitoa matumaini kwa wananchi kuwa mkoa huo utabaki kuwa wa amani.
Makamu mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Nyasa, Frank Mwakajoka amesema wana matumaini ya kupatikana kwa kada wao, akieleza kuwa wanaamini waliomfanyia unyama huo walimtupa moja ya pori mkoani Iringa kisha kuletwa sehemu moja mkoani Mbeya.
“Tuko tayari kumtibu kwa kuwa tunaamini hajafa…huenda wangemtekeleza, imani yetu ni kuwa yuko hai isipokuwa ameumizwa sehemu za kichwa, lazima tujue Serikali haijengwi na chama kimoja,” Mwakajoka
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Kaloli Masaga amemshukuru mkuu wa mkoa huo kwa kuwapokea na kuwasikiliza kilio chao akieleza kuwa wamepata matumaini kwa namna kiongozi huyo alivyoweza kukabiliana na majukumu.
“Mzigo tumekuachia wewe na umeonesha ustahimilivu, kuna polisi wanatupenda, viongozi wa Serikali nao wapo na sisi, hivyo kwa kauli yako hii tumejua mwelekeo mpya na tukuombee utekelezaji mwema katika wajibu wako,” amesema Masaga.
Wakili Philip Mwakilima ameshukuru kikao hicho na kushauri Serikali mkoani humo kuona namna ya kukutana na viongozi na wazee wa kimila ili kubaini na kuondokana na matukio yanayojirudia.
“Yapo mambo tunakuwa hatuyaoni sisi, lakini hao wazee na viongozi wa kimila wanaweza kusaidia namna ya kufanya mkoa huu kuendelea kuwa shwari,” amesema wakili huyo.